Marufuku watoto chini ya miaka 9 kupanda bodaboda Tanga

Muktasari:
- Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Safia Jongo amepiga marufuku bodaboda kubeba watoto chini ya miaka tisa ili kuwakinga watoto hao na ajali za barabarani.
Tanga. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Safia Jongo amepiga marufuku bodaboda kubeba watoto chini ya miaka tisa ili kuwakinga watoto hao na ajali za barabarani.
Akizungumza jijini Tanga leo Aprili 4, 2022 Kamanda huyo amesema kumekuwa na tabia ya wakazi wa Tanga kutumia bodaboda kama basi la shule kitu ambacho hakikubaliki kisheria.
Amesema kisheria mtoto wa chini ya umri wa miaka mitatu hadi tisa haruhusiwi kupanda pikipiki. “Lakini sasa sio mtoto mmoja tu wanapakiza zaidi ya mtoto mmoja, watatu hadi wanne,” amesema
Kamanda jongo amesema Polisi Tanga wameandaa mkakati wa kupeleka askari wa usalama barabarani katika shule zote za jijini hapo ili kubaini watoto watakaopelekwa na bodaboda wazazi watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake mkazi wa jiji la Tanga, Elizabeth Kabage amesema wana wanatumia bodaboda kwa sababu wanabebwa na mtu wanayemfahamu hivyo wahukakika na usalama wa watoto wao.
“Sisi ambao hatuna magari au hatuna uwezo wa kulipia basi ya shule, suala hapa ni usalama wa watoto. Mtoto akipakia bodaboda una uhakika kuwa atafikishwa shuleni kwa sababu anapakizwa na mtu unayemfahamu na kurudishwa salama. Hakuna wasiwasi wa suala la kuvuka barabara,” amesema Kabage.