Marufuku kupanda basi, daladala bila barakoa

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Stephen Kagaigai amepiga marufuku abiria wanaoingia ndani ya daladala na mabasi yaendayo mikoani kutoruhusiwa kuingia bila kuvaa barakoa ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amepiga marufuku abiria wanaoingia ndani ya daladala na mabasi yaendayo mikoani kutoruhusiwa kuingia bila kuvaa barakoa ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Agizo hilo amelitoa leo Julai 29, 2021 mkoani hapa huku akiwataka madereva wa mabasi pamoja na daladala kuhakikisha abiria hawasimami ndani ya gari pamoja na kuhakikisha abiria wote wanakaa.
“Ni lazima anayeingia kwenye mabasi awe amevaa barakoa, lakini pia hakuna kusimamisha abiria lazima wakae ‘level seat’ na nimeshamwelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro amwagize kamanda wake wa kikosi cha usalama barabarani wawe makini kwenye hilo,”amesema Kagaigai.
“Dereva atakayekwenda kinyume na hilo na kuondoka stendi na abiria ambaye hajavaa barakoa lazima wafauatiliwe na hatua zichukuliwe na hii tunafanya kwa nia nzuri kwa ajili ya kutunza afya za wananchi wetu, Serikali inapenda wananchi wake wawe na afya njema ili waweze kuzalisha,”amesema Kagaigai.
“Tunamshukuru sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutupigania na kutuletea chanjo, lakini wakati huu tukisubiri kwenye maeneo yetu tuletewe chanjo endeleeni kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wizara ya afya,”amesema.