Marekani yatumia Sh97 trilioni vita dhidi ya Iran
Muktasari:
- Fedha hizo zimejumuisha matumizi mbalimbali ya kijeshi yanayohesabiwa hadi mwisho wa mwaka wa fedha.
Dar es Salaam. Ndani ya miezi mitano ya vita dhidi ya Iran, Marekani imetumia Dola 37.5 bilioni (zaidi ya Sh97 trilioni), kiwango ambacho ni zaidi ya mara moja na nusu ya bajeti ya Tanzania ya 2026/27.
Bajeti ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2026/27 ni Sh62.33 trilioni.
Hata hivyo, gharama za vita hiyo zinatabiriwa zitakuwa kubwa zaidi, kwa kuwa ndani ya muda mchache, Marekani imetumia fedha nyingi. Vita kati ya mataifa hayo, ilianza Februari 28, mwaka huu.
Taarifa ya gharama hizo, imetolewa jana Jumanne, Julai 21, 2026 na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, akidokeza huenda gharama halisi zikawa kubwa zaidi.
Ingawa gharama zinatabiriwa zitaongezeka zaidi, bado hazijafikia kiwango kinacholingana na vita nyingine ambazo Marekani imewahi kupigana katika miongo ya karibuni, hususan Afghanistan na Iraq.
Katika vita yake dhidi ya Afghanistan, Marekani ilitumia Dola trilioni 2.31. Vita hiyo ilidumu kwa zaidi ya miongo miwili, kuiondoa Taliban madarakani na kuuvunja mtandao wa Al-Qaeda ulioongozwa na Osama bin Laden.
Gharama kubwa pia, zilitumika katika vita dhidi ya Iraq mwaka 2003. Ilitumia Dola za Marekani 2.2 trilioni. Gharama hizo zimehusisha pia na mgogoro wake dhidi ya kundi la Islamic State (ISIS) lililokuwa limeteka maeneo nchini Iraq na Syria.
Alichosema Hegseth
Akizungumza mbele ya Kamati ya Matumizi ya Seneti ya Marekani jana, Hegseth amesema sehemu ya fedha hizo imejumuisha matumizi mbalimbali ya kijeshi yanayoendelea kuhesabiwa hadi mwisho wa mwaka wa fedha.
Baadhi ya gharama, amesema zinahusisha mahitaji ya kawaida ya wanajeshi, ikiwemo chakula, usafiri na shughuli nyingine za uendeshaji wa operesheni za kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kauli hiyo imekuja wakati mjadala kuhusu gharama za vita na mkakati wa Marekani dhidi ya Iran ukiendelea kuibua maswali kutoka kwa wabunge wa vyama vyote viwili nchini humo.
Akizungumzia usalama wa njia ya bahari ya Hormuz, Hegseth amesema operesheni ya jeshi la Marekani ya kusindikiza meli iliendelea kwa siri hata baada ya kutangazwa rasmi Mei mwaka huu.
Amedai operesheni hiyo imewezesha kusafirishwa kwa hadi mapipa milioni 500 ya mafuta kupitia njia hiyo muhimu kwa biashara ya nishati duniani.
Hegseth, amesema Marekani imeendelea kudhibiti usalama wa eneo hilo licha ya mashambulizi yaliyofanywa na Iran dhidi ya meli na miundombinu mingine ya usafirishaji.
Azishutumu China, Russia
Katika hotuba yake hiyo, Hegseth amesema mataifa ya China na Russia yanaisaidia Iran kwa viwango tofauti, ingawa hakutoa maelezo ya kina kuhusu aina ya msaada huo.
Amesema Marekani ina mbinu mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo, lakini ukubwa na undani wa hatua zinazochukuliwa ni masuala ya siri ya kiusalama.
Hegseth, pia aliulizwa kuhusu uwezo wa jeshi la Marekani kushambulia kituo kinachoshukiwa kuhusika na shughuli za nyuklia chini ya mlima unaoitwa Pickaxe Mountain.
Alikataa kufafanua uwezo huo akisema sehemu kubwa ya teknolojia na uwezo wa kijeshi wa Marekani ni siri za Taifa.
Kauli hiyo imekuja siku ambayo Rais Donald Trump, amesema Marekani inaweza kulenga eneo hilo hivi karibuni, jambo lililoongeza taharuki kuhusu hatua inayoweza kufuata.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Dan Caine, amesema ataendelea kumpatia Rais Trump chaguzi mbalimbali pamoja na tathmini ya hatari zinazoweza kujitokeza.
Amesema kila uamuzi wa kijeshi huzingatia athari zake kwa binadamu na kwamba suala hilo ni miongoni mwa mambo makuu yanayowasilishwa kwa Rais.
Kikao hicho pia kiligeuka kuwa uwanja wa mabishano makali kati ya Hegseth na baadhi ya maseneta wa Chama cha Democratic.
Seneta wa Michigan, Gary Peters, alimkosoa Hegseth vikali na kumtuhumu kushindwa kuonyesha uongozi unaotakiwa katika kusimamia vita dhidi ya Iran.
Peters pia, amehoji mkakati wa utawala wa Trump, akitaka maelezo zaidi kuhusu malengo ya vita na namna vitakavyomalizika.
Mvutano mwingine ulijitokeza wakati Seneta wa New York, Kirsten Gillibrand, alipouliza msingi uliotumika kuhalalisha kuanzishwa kwa vita hivyo.
Gillibrand, amemshutumu Hegseth kwa kuupotosha umma kuhusu madai ya Marekani kuharibu uwezo wa Iran wa kurusha makombora.
Hata hivyo, Hegseth amejibu kwa kumtuhumu seneta huyo kutumia kikao hicho kwa masilahi ya kisiasa na kutafuta hoja za kampeni.
Habari hii imeandikwa kwa msaada wa mitandao