Marais wa EAC watoa mwelekeo soko huru

Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na baadhi ya viongozi wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wawakilishi wakati wa wimbo wa Taifa wa Afrika Mashariki kwenye ukumbi wa Mikutano wa AICC jijini Arusha kabla ya kuanza kwa kikao cha wakuu hao wa nchi. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wametoa mwelekeo kuimarisha soko huru la jumuiya hiyo, wakitaka kuboreshwa miundombinu, uzalishaji na kuoanisha sera ili kuondoa vikwazo vya kibiashara.
Dar es Salaam. Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wametoa mwelekeo kuimarisha soko huru la jumuiya hiyo, wakitaka kuboreshwa miundombinu, uzalishaji na kuoanisha sera ili kuondoa vikwazo vya kibiashara.
Mapendekezo ya wakuu hao wa nchi yalitolewa juzi katika mkutano wa 22 wa jumuiya uliolenga kujadili uimarishaji wa soko la pamoja, ikiwa ni miaka 11 tangu kuanzishwa kwa soko hilo.
Soko hilo linalenga kutoa uhuru wa kibiashara baina ya mataifa husika, kuoanisha sera, kanuni na taratibu ili kuwezesha ufanyikaji biashara katika ukanda huo.
Katika mapendekezo yake, Mwenyekiti wa EAC, Rais Uhuru Kenyatta alisema ili kuwa na soko la pamoja unahitajika uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Bila ya kutekelezwa hilo, alisema EAC itabaki kuwa soko la bidhaa zinazozalishwa na mataifa ya nje kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mataifa wanachama wa jumuiya hiyo.
“Nje ya EAC wanatamani tuendelee kuwa wategemezi, ndiyo maana kila tunachofanya, ikiwemo kuwekeza kwenye miundombinu wanalalamika kwamba tunatumia fedha nyingi. Hawataki tuendelee,” alisema.
Kenyatta ambaye pia ni Rais wa Kenya, alizungumzia rasilimali za nchi wanachama akisema iwapo hakutakuwa na umakini nchi hizo zitaendelea kuwa masikini wakati malighafi zake zinazotumiwa kutajirisha nchi nyingine duniani.
“Kwa nini bidhaa hizi ziendelee kutengenezwa nje ilhali malighafi zinatoka kwetu, tunapaswa tuwe na uwezo wa kusambaza wenyewe,” alisema.
Uzalishaji katika kilimo
Mbali na Kenyatta, Rais Samia Suluhu Hassan alisema soko hilo litatokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo mara mbili au zaidi ya inavyozalishwa sasa.
Alisema inawezekana nchi za EAC kuwa kitovu cha uzalishaji, kwani zina ardhi nzuri ya kilimo, lakini akashauri maboresho katika utumiwaji wa ardhi hiyo, ili kuzalisha kama inavyokusudiwa.
Ufikiwaji wa mitaji kwa wakulima ni jambo lingine alilosema linahitaji kufanyiwa kazi, ili sekta hiyo itekelezwe vema.
Hata hivyo, alisema uhifadhi wa chakula baada ya mavuno ni jambo muhimu linalopaswa kushughulikiwa kwa maslahi ya kuongeza uzalishaji katika kilimo.
Samia aliongeza kuwa ni muhimu kuboreshwa miundombinu ya kuchakata, ili kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na hatimaye mataifa hayo kunufaika.
“Soko ni eneo lingine, maana tunapaswa kujua baada ya kuzalisha wapi tutapelekea. Hayo ndiyo maeneo ambayo yanaweza kuifanya jumuiya kuwa mzalishaji mkubwa wa mazao,” alisema.
Suala la kuzigeuza changamoto kuwa fursa ni jambo lililoelezwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuwa msingi wa nchi hizo kujitegemea na kuingiliana.
Alisema ili kufanikisha hayo kunahitajika sera zitakazowezesha nchi hizo kuingiliana badala ya kuweka vikwazo.
Baada ya janga la Uviko-19, alisema Taifa lake walianza utafiti wa chanjo ambao kwa sasa upo hatua ya tisa na ikipitishwa itatumika. Mbali na hilo, alisema walishaanza kutengeneza magari ya umeme kuepuka changamoto ya bei ya mafuta na kinachofanywa sasa ni kuboresha kiwanda husika.
Rais wa Burundi, Evarist Ndayishimiye alisema hatua ya uhuru wa kutembea kutoka nchi moja kwenda nyingine miongoni mwa wanachama wa jumuiya hiyo ni ishara nzuri kwa uimara wa EAC.
“Tunakwenda vema kwa sababu kuna uhuru wa kutembea kwa watu wote, jambo tunalopaswa kuboresha ni mawasiliano. Tunapaswa kuchukulia kwamba kila nchi mwanachama ni familia,” alisema.
Pia alipendekeza kuondolewa kwa vikwazo vya usafiri wa anga baina ya nchi wanachama, jambo litakaloruhusu mwingiliano wa kibiashara na soko la pamoja.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Jean-Michael Sama alisema katika taifa hilo kumekuwa na changamoto za kuisalama kutokana na makundi ya ugaidi yenye silaha.
Waziri Mkuu wa Sudan Kusini, Abdalla Hamdok, alisema Taifa hilo limeanza kujifunza Kiswahili ikiwa ni sehemu ya lugha za familia.
Mbali na hilo, alisema wanawake 2,000 wa nchi hiyo wamehitimu mafunzo ya biashara na wanafanya ujasiriamali nchini Uganda kila siku.
“Hata ukija Juba siku moja ukakuta nyanya kutoka Uganda usishangae, watu wanazunguka,” alisema.