Mara kuanza msako wa wanafunzi, idadi ya walioripoti ikisuasua

Wanafunzi wakiwa darasani wakifuatilia wanachofundishwa na mwalimu. Picha na maktaba
Muktasari:
Mkoa wa Mara ulitarajia kuandikisha wanafunzi 74,234 kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza na hadi juzi jumla ya wanafunzi 67,061 sawa na asilimia 90.3 walikuwa wamekwisha andikishwa na kuanza masomo.
Musoma. Asilimia 61 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za Serikali mkoani hapa, wameripoti katika shule hizo hadi kufikia Januari 17, 2024.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda, leo Ijumaa Januari 19, 2024 amesema kuwa jumla ya wanafunzi 32,212, kati ya 52,784 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali mwaka huu tayari wameripoti shuleni na kuanza masomo.
Kwa upande wa shule za msingi, Mtanda amesema mkoa huo ulitarajia kuandikisha wanafunzi 74,234 kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza na hadi juzi jumla ya wanafunzi 67,061 sawa na asilimia 90.3 walikuwa wamekwisha andikishwa na kuanza masomo.
Amefafanua kuwa kati ya hao wanafunzi walioandikishwa, 173 ni wenye mahitaji maalumu.
Kuhusu elimu ya awali, Mtanda amesema mkoa umefikisha asilimia 78.7 ya maoteo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
"Tulitarajia kuandikisha watoto 82,679 kwa madarasa ya awali na hadi juzi tayari tuna watoto 65,067 shuleni na kati yao wapo 111 wenye mahitaji maalumu", amesema.
Kufuatia hali hiyo Mtanda amesema tayari amewaagiza viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi vitongoji kufanya msako na kuhakikisha kila mtoto anayepaswa kuwa shule awe ameripoti na kuanza masomo.
Ameongeza kuwa tayari alikwisha toa maelekezo kwa walimu wakuu pamoja na wakuu wa shule kuwapokea wanafunzi katika hali yoyote wakiwamo wasiokuwa na sare za shule ili waendelee na masomo, wakati wazazi wakiendelea na utaratibu wa kuwanunulia mahitaji.
"Kama kuna mtoto amerudishwa nyumbani kuwa hana sare au mahitaji mengine naomba nipate hiyo taarifa kwa sababu anayehusika na manunuzi ya mahitaji sio mtoto ni mzazi, hivyo kukataa kumpokea mtoto ni kumuonea, narudia tena watoto wote wapokelewe bila kujali waana mahitaji au la,” amesema.
Wakizungumza na Mwananchi dijital baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema zipo sababu kadhaa za watoto kuchelewa ama kutokuripoti kabisa kwenye shule walizopangiwa.
"Ni vigumu kwa watoto wote kuripoti kwenye shule walizopangiwa, wapo waliopelekwa kwenye shule binafsi kwa hiyo sio kwamba hawapo shuleni ila wapo shule tofauti na walizopangiwa", amesema Antonia Martin.
"Mimi sijampeleka mwanangu kwa sababu shule aliyopangiwa kwa kweli sijaikubali licha ya kuwa alipata ufaulu mzuri, hapa najiandaa nimpeleke shule binafsi nilikuwa nimepungukiwa ada lakini wiki ijayo atakuwa shuleni ila sio shule ile aliyopangiwa", amesema Stella Mkama
"Ni kweli Serikali imesema mtoto aende shuleni hata kama hana sare lakini kiuhalisia ni vigumu mzazi kumruhusu mtoto kwenda shule na nguo za nyumbani, ina maana kwa sasa wazazi wanapambana wawanunulie watoto mahitaji ili waanze shule rasmi," amesema Steven John.