Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wapata sekondari Musoma

Profesa Sospeter Muhongo (t-shirt jeupe) akiwa na baadhi ya watu kwenye ukaguzi wa majengo ya shule

Muktasari:

Kilio cha muda mrefu cha kukosa shule ya sekondari ya kata katika Kata ya Ifulifuli Wilaya ya Musoma Vijijini kimesikika ambapo ujenzi wa shule umeanza na hadi kufikia Julai 2022 wanafunzi wanatarajiwa kuanza masomo.

Dodoma. Kilio cha muda mrefu cha kukosa shule ya sekondari ya kata katika Kata ya Ifulifuli Wilaya ya Musoma Vijijini kimesikika ambapo ujenzi wa shule umeanza na hadi kufikia Julai 2022 wanafunzi wanatarajiwa kuanza masomo.

 Ifulifuli ndiyo kata pekee kati ya 21 zinazounda jimbo la Musoma Vijijini ambayo haikuwa na shule ya sekondari katika vijiji vyake vitatu vya Kabegi, Kiemba na Nyasaungu.

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na sekondari walikuwa wakisoma katika Kata za Nyakatende na Mugango ambako ni mbali na hivyo kusababisha baadhi yao kuishia njia bila kumaliza masomo ya kidato cha nne.

Akizungumza leo Ijumaa Machi 11, 2022 Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospiter Muhongo amesema tayari Wilaya hiyo ilishapokea Sh470 milioni na kuzikabidhi katika uongozi wa Kata na shughuli ya ujenzi inakwenda kwa kasi zaidi.

Profesa Muhongo amesema kwa sasa jimbo hilo linakuwa na jumla ya Sekondari 22 ikiwamo 2 za binafsi na hivyo suala la maboresho ya elimu kwa watoto ni ajenda iliyokamilika kulingana na malengo yao.

“Tulipatia fedha hizo kupitia Mradi wa Secondary Education Quality Improvement Programme (SEQUIP), tutasimamia kukamilika,” amesema Profesa Muhongo.

Amesema kuwa ujenzi wa sekondari hiyo ulianza Juni 2017 lakini umekuwa ukienda kwa kusuasua kutokana na ukosefu wa fedha za ujenzi hivyo kiasi hicho kinakwenda kumaliza na kuruhu shule ifunguliwe Julai 2022.

Waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini amesema kuna baadhi ya Kata zinahitaji kuwa na shule zaidi ya moja kutokanana jiografia ya makazi ya watu hivyo kwa kushirikiana na wananchi wake baadhi ya maeneo wameshaanza ujenzi wa shule zingine.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kabegi, Charles Choto amesema usimamizi wa majengo hayo unakwenda vizuri ambapo wananchi kwa kushirikiana na viongozi wamewekeana malengo kuwa haitazidi Julai mwaka huu shule kuwa imefunguliwa.

Choto ametaja kazi zinazofanyika ni umaliziaji wa madarasa na jengo la utawala ambayo baadhi yalianzishwa kwa nguvu ya wananchi miaka mitano iliyopita pamoja na kuongeza miundombinu mingine.

Ofisa Elimu wa Kata hiyo, Beatrice Ndossi amesema idadi ya majengo yanayojengwa katika shule hiyo, yanatosheleza kuingiza watoto wote ambao wamepangiwa shule za jirani na kuwa na ziada ya madarasa.

Mwalimu Ndossi amesema shule hiyo inajengwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya sasa na baadae hivyo akataka wananchi wasiwe na hofu juu kuanza uchangishaji wa majengo mengine shuleni hapo kwa miaka ya hivi karibuni.