Manyara yaandikisha wanafunzi wapya 72,717

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Tenisia Katukuru (katikati) akiandika maelezo ya mzazi Sofia Ally aliyemleta mwanaye darasa la kwanza kwenye shule hiyo, Juma Ally. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Jumla wanafunzi 72,717 wa darasa la awali na darasa la kwanza wameandikishwa mkoani Manyara katika muhula mpya unaoanza leo Januari 9.
Babati. Jumla wanafunzi 72,717 wa darasa la awali na darasa la kwanza wameandikishwa mkoani Manyara katika muhula mpya unaoanza leo Januari 9.
Ofisa elimu wa mkoa wa Manyara, Halfani Masukira ameyasema hayo leo wakati akizungumzia juu ya uandikishwaji wa wanafunzi wa shule ya awali na darasa la kwanza kwa shule za msingi.
Masukira amesema uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la awali ulitakiwa kuanza Oktoba mwaka jana mpaka Desemba 31 kwa mujibu wa muongozo uliotolewa ila uandiikishaji utaendelea ili wazazi waandikishe watoto wote.
Ameeleza kuwa malengo ya mwaka huu 2023 yalikuwa kuandikisha wanafunzi wa darasa la awali 46,494 wa kiume 23,726 na wa kike 22,768 na darasa la kwanza kuandikisha wanafunzi 57,176 ambapo wa kiume 29,227 na wa kike 27,949.
Amesema mpaka sasa mkoa umeishaandikisha wanafunzi wa darasa la awali 29,072 wa kiume 15,151 na wa kike 13,921 sawa na asilimia 63.
"Darasa la kwanza maoteo ni kuandikisha wanafunzi 57,176 wa kiume 29,227 na wa kike 27,949 ila tumeandikisha wanafunzi 43,645 wa kiume 22,762 na kike 20,963 sawa na asilimia 76.33," amesema Masukira.
Ofisa huyo wa elimu amesema kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, mzazi au mlezi anayeshindwa kumuandikisha mtoto shule anaweza kuchukuliwa hatua ikiwemo kifungo, kulipa faini au vyote kwa pamoja.
Pia, ameeleza kuwa elimu ya awali inamuandaa mwanafunzi kwenda elimu ya msingi na kila shule inatakiwa kuwa na darasa la awali.
Mwalimu wa darasa la awali wa shule ya msingi Dudumera iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Babati, Jemima Njidile akizungumzia uandikishwaji, amesema wanafunzi wa awali wakiandikishwa mapema inasaidia kuzoea mazingira na ndiyo wanakuwa wazuri zaidi.
Njidile amesema inawarahisishia kazi walimu na wanafunzi wanaoneshwa mahali vyoo vilipo na kuelekezwa njia ya kurudi nyumbani kwao.
Mkazi wa Mtaa wa Mruki Hassani Omari amesema kuandikisha wanafunzi mapema ni vizuri kwa kuwa inasaidia mzazi kujua mahitaji yanayotakiwa na kujipanga.