Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Changamoto watoto kutopitia elimu ya awali

Mwalimu wa darasa la kwanza shule ya msingi Mwere Manispaa ya Morogoro akimuelekeza mwanafunzi, Doreen Felix namna ya kuumba herufi. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Watoto wanaoanza darasa la kwanza bila kupitia elimu ya awali wametajwa kuwa changamoto katika ufundishaji.

Morogoro. Ikiwa ni siku ya kwanza kwa wanafunzi wa darasa la kwanza kuingia darasani, baadhi ya walimu mkoani hapa wameeleza changamoto ya wanafunzi wanaoingia elimu ya msingi kutokuwa na uelewa wa mambo ya msingi kwa kukosa elimu ya awali.

Akizungumza leo Januari 9 na Mwananchi, mmoja wa walimu wanaofundisha darasa la kwanza shule ya msingi Mwere, Aisha Kibiki amesema sehemu kubwa ya wanafunzi hao wanajua kusoma na kuandika, lakini baadhi yao hawawezi kwa kutohudhuria elimu ya awali.

"Kwa wastani mtoto anatakiwa asome elimu ya awali kwa miaka miwili, lakini pia inategemea na shule aliyosoma, kwani shule nyingi za awali zipo kibiashara hapo ndio utakuta mtoto anasoma miaka hiyo miwili lakini hajui kusoma vizuri wala kuandika," amesema Mwalimu Kibiki.

Aidha ametaja sababu nyingine ya baadhi ya watoto kutokuwa na uelewa wa kutosha, ambapo amesema kuwa wazazi nao wamekuwa wakichangia hasa wanapong'ang'ania watoto wao kuanza darasa la kwanza wakiwa na umri mdogo ama bila ya kupitia elimu ya awali.

Akizungumzia idadi ya wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la kwanza Mwalimu Kibiki amesema kuwa ni 74 ambapo wasichana ni 43 na wavulana ni 31.

Mmoja wa wazazi wenye watoto walioanza darasa la kwanza Chifu Chewe amewaomba askari wa usalama barabarani kujenga utaratibu wa kuwavusha wanafunzi hasa wa darasa la kwanza kwenye vivuko vya barabara kwa ajili ya usalama wa watoto hao.

"Shule nyingi za hapa mjini zinapitiwa na barabara kubwa zenye magari, bodaboda na vyombo vingine vya moto, leo watoto hawa tumewaleta shule na mchana tutawafuara sasa baada ya leo itabidi waje wenyewe shule na warudi wenyewe nyumbani sasa usalama wao ukoje wakiwa barabarani," amehoji Chewe.