Wazazi wakumbushwa kuwa karibu na watoto wao

Mwalimu anayefundisha Darasa la Kwanza Shule ya Msingi Kambarage Halmshauri ya Mji wa Kibaha Mkoani Pwani Amina Kijuu,Picha na Sanjito Msafiri
Muktasari:
- Wazazi na walezi nchini wamekumbusha kuwa karibu na watoto wao kwa kuwafanyia maandalizi ya shule katika hatua zote ikiwemo kuwaogesha hali itakayowawezesha kutambua maendeleo yao kiafya na usalama.
Kibaha. Wazazi na walezi nchini wamekumbusha kuwa karibu na watoto wao kwa kuwafanyia maandalizi ya shule katika hatua zote ikiwemo kuwaogesha hali itakayowawezesha kutambua maendeleo yao kiafya na usalama.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu January 9, 2023 na Mwalimu wa darasa la kwanza shule ya msingi Kambarage ya wilayani hapa, Amina Kijuu baada ya kukamilisha shughuli ya kuwaandikisha wanafunzi wanaoanza Shule mwaka huu.
Amesema kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaachia wafanyakazi wa ndani jukumu la kuwaandaa watoto wao kwa kisingizio cha kuwa na majukumu ya kazi jambo ambalo limekuwa likiwaletea shida.
"Sasa hivi dunia imeharibika, kuna baadhi ya watoto tumeona wamekuwa na tabia hata ya kuingiliana wao kwa wao hasa wa kiume hivyo kama wazazi hawatakuwa makini wanaweza kusababisha hatari.
"Ni lazima wazazi watambue kuwa wanachokipanda leo ndicho watakachovuna kesho hivyo ni vema wakawa karibu na watoto wao Ili kupata viongozi bora wa baadaye," amesema.
Baadhi ya wanafunzi walioanza darasa la kwanza katika shule hiyo wameahidi kujikita kusoma ili kupata mafanikio ya maisha.
"Napenda kusoma naamini kuwa nikisoma nitapata maisha mazuri baadaye," amesema Mathayo Msafiri.
Naye Nassibu Masasa amesema kuwa maisha bila kusoma hayawezi kuwa mazuri hivyo atahakikisha anafanya juhudi katika masomo Ili kutimiza ndoto zake.