Geita yashindwa kufikia lengo uandikishaji darasa la kwanza

Paulo Marwa Mkazi wa Geita akimpeleka shule mwanae Elizabeth anaeanza darasa la kwanza katika shule ya msingi Mseto iliyopo mjini Geita.
Muktasari:
- Mkoa wa Geita umeshindwa kufikia lengo la kuwaandikisha wanafunzi 168,422 wa darasa la kwanza na awali waliolengwa kuanza masomo mwaka 2023 baada ya mkoa huo kuandikisha wanafunzi 139,371 sawa na asilimia 82.75 ya lengo.
Geita. Ikiwa ni siku ya kwanza ya wanafunzi wa darasa la kwanza na awali kuanza shule, Mkoa wa Geita umeandikisha wanafunzi 139,371 kati ya wanafunzi 168,422 waliotarajiwa kuandikishwa kwa mwaka 2023 sawa na asilimia 82.75.
Mkoa huo ulitarajia kuandikisha wanafunzi 66,137 wa darasa la awali na hadi kufikia desemba 31 ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya uandikishaji walikua wameandikisha wanafunzi 55,857 sawa na asilimi 86.
Akizungumza na mwananchi Ofisa Elimu mkoa, Antony Mtweve amesema kwa darasa la kwanza mkoa huo ulilenga kuandikisha wanafunzi 102,285 na hadi desemba 31, 2022 wameandikisha watoto 83,514 sawa na asilimia 86 ya lengo.
Kwa mujibu wa ofisa elimu huyo amesema licha ya awali kutangazwa mwisho wa kuandikisha ni Desemba 31 lakini bado uandikishaji unaendelea na halmashauri zimehimizwa kuandikisha kwa asilimia 100.
“Changamoto tunayoiona ni wazazi kuona watoto kama sehemu ya nguvu kazi na sehemu ya kujiongezea kipato kwenye familia hivyo wanawaacha nyumbani badala ya kuwapa fursa ya elimu tunawahimiza wazazi wenye watoto wa miaka mitano hadi sita wahakikishe wanawaandikisha,” amesema Mtweve.
Ili kuhakikisha malengo yanafikiwa Maofisa Watendaji kwa kushirikiana na walimu wakuu na Maafisa Watendaji wa Vijiji pamoja na mabalozi wameagizwa kupita nyumba kwa nyumba kuangalia watoto wenye umri wa kuanza shule na hawajaandikishwa ili waweze kuandikishwa.
Akizungumza na Mwananchi, Veronica Abel ambae ni mzazi amesema amefanikisha kumuandikisha mwanaye shule ya msingi Geita bila kudaiwa michango yoyote na kuwaomba wazazi kutoa ushirikiano ili watoto wadogo walioandikishwa waweze kupata uji shuleni.
“Hakuna mchango tuliodaiwa ila Mwalimu Mkuu ameomba tuchangie 5,400 kwa mwezi kwa ajili ya watoto kupata uji kwa kweli mimi naona ni sawa na ninawaomba wazazi wenzangu tuunge mkono hili ili watoto waweze kula shuleni sio hawa tuu hata wa madarasa mengine,” amesema Abel.