Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mamlaka kuanzisha maabara mipakani kudhibiti viuatilifu bandia

Mtaalamu  wa Viuatilifu kutoka  Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu  Tanzania, Dk.Mohamed Mpina

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja kufuatia mamlaka hiyo kudai bado kuna changamoto ya viatilifu bandia kuingia nchini kupitia maeneo ya mipakani na njia za panya.

Dodoma. Katika kukabiliana na changamoto ya viuatilifu bandia, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania (TPHPA) inatarajia kuanzisha maabara ndogo kwenye vituo 17 vya ukaguzi mipakani.

Hatua hiyo imekuja kufuatia mamlaka hiyo kukiri bado inakabiliwa na changamoto ya viatilifu bandia kuingia nchini kupitia maeneo ya mipakani na njia za panya.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Machi Mosi, 2023 na mtaalamu wa viuatilifu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania, Dk Mohamed Mpina wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita.

Dk Mpina alipewa nafasi hiyo na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Profesa Joseph Ndunguru baada ya waandishi wa habari kuhoji ni mkoa gani kinara wa utengenezaji wa viuatilifu bandia.

Mtaalamu huyo amesema ni ngumu kuutaja mkoa ila bado maeneo ya mipakani yanachangamoto ya uingizaji wa viuatilifu hivyo kutokana na kusajiliwa katika nchi zinazotoka.

“Pia kuna njia za panya ambazo zinatumika kuingiza ila kuna watu na makampuni tumeyakamata na kesi zipo maana kisheria ni kosa kufanya hivyo,”amesema mtaalamu huyo kutoka Idara ya Viuatilifu.

Kwa upande wake, Prof Ndunguru amesema jumla ya viuatilifu vipya 409 na kampuni za ufukizaji 198 vilisajiliwa katika maeneo mbalimbali nchini na mamlaka imeendelea kufanyika kaguzi ili kupunguza uwepo wa viuatilifu bandia.

Amesema uchunguzi wa sampuli 103 za shehena za mimea zilifanyika katika maabara na vitalu nyumba ambapo jumla ya maombi 762 ya vibali vya kuingiza vipando nchini Tanzania yalipokelewa.

“Tumefanya ukaguzi zilifanyika katika karantini za wazi, miwa na viazi mviringo na matunda ya Sapodilla. Vipando vyote kwenye karantini hizo vilikidhi matakwa ya afya ya mimea ya Tanzania,”amesema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Prof Ndunguru amesema mamlaka imeweza kukusanya jumla ya sampuli 400 za nasaba za mimea ya aina mbalimbali na kuhifadhi katika benki ya mbegu.

Katika kukabiliana na viwavi jeshi, Kaimu Mkurugenzi huyo amesema jumla ya lita 81,563 za Profenofos zimesambazwa katika halmashauri 57 za mikoa lengo likiwa ni kudhibiti uharibifu katika mazao ya nafaka.

Ameitaja mikoa hiyo ni Lindi, Pwani, Morogoro, Tanga, Geita, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Dar es Salaam, Katavi na Arusha.

Prof Ndunguru amesema mamlaka imekagua tani 5,343,380.59 za mazao ya nafaka, bustani, mizizi, mbegu za mafuta katika vituo vya mipakani, bandari na viwanja vya ndege.

Amesema jumla ya vyeti 29,033 vya usafi wa mimea kwa ajili ya kuruhusu mazao kusafirishwa nje ya nchi na vyeti 3,359 vya kuruhusu mazao kuingia nchini vimetolewa.

Amesema mamlaka imedhibiti ndege aina ya kwelea kwelea milioni 227.4 na kufanikiwa kuokoa tani 1,056.3 za mazao ya nafaka.

Ameyataja malengo yao ni kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara viuatilifu kwa watengenezaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji ili kupunguza athari ya kuwepo kwa viuatilifu bandia.

Hata hivyo, amesema wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa wakulima na wadau wengine juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja na uwepo wa wauuzaji wa viuatilifu na mazao ya mimea wasio waaminifu.