Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo manne yanayomsubiri Rais Samia Morogoro

Rais wa Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, wageni mbalimbali pamoja wananchi mara baada ya kuzindua rasmi miundombinu ya reli na huduma za usafiri wa reli ya kisasa (SGR) jana Agosti Mosi, 2024. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Rais Samia ameanza ziara ya siku sita leo Agosti 2, 2024 katika Mkoa wa Morogoro. Kwenye ziara hiyo, Rais Samia atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kwenye maeneo atakayopita.

Morogoro. Changamoto ya miundombinu, upatikanaji wa maji safi na salama, migogoro ya wakulima na wafugaji na kero ya uchafu sokoni ndiyo mambo yanayotarajiwa kujitokeza zaidi kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Morogoro.

Rais Samia ameanza ziara ya siku sita leo Agosti 2, 2024 katika Mkoa wa Morogoro. Kwenye ziara hiyo, atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo sambamba na kuzungumza na wananchi kwenye maeneo atakayopita.

Katika ziara yake hiyo, pamoja na mambo mengine, migogoro ya wakulima na wafugaji ni jambo linalotarajiwa kujitokeza kwenye ziara hiyo, kwa kuwa ni suala linalowasumbua wengine, yeye akiwa mwathirika katika hilo.

Rais Samia aliwahi kueleza machungu wanayokutana na wakulima wa mazao yao kuliwa na mifugo na majibu ya dharau aliyopewa na mfugaji baada ya mifugo kula mpunga kwenye shamba lake, eneo Dutumi mkoani Morogoro.

Mkuu huyo wa nchi alijenga hoja hiyo wakati akizungumzia madhara ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambapo watu wamekuwa wakipigwa, kuuana na mazao yao kuliwa na mifugo. Rais Samia alitumia nafasi hiyo kuwaomba machifu nchini kukemea hali hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi, wakazi wa Morogoro wamesema wanamsubiri kwa hamu Rais Samia ili kufikisha changamoto hizo, kwa lengo la kupata ufumbuzi.

Changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji hasa katika Wilaya ya Mvomero imeleta madhara kwa wananchi, katika ziara yake, Rais Samia anatarajiwa kuzindua rasmi kampeni ya ‘Tutunzane Mvomero’ inayolenga kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaishi kwa amani na kutegemeana bila migogoro.

Kampeni hiyo inalenga kuleta uelewa wa pamoja na ushirikiano baina ya makundi hayo mawili muhimu kwa maendeleo ya eneo hilo.

Mmoja wa wakulima wa Mvomero, Said Mussa amesema wiki kadhaa zimepita tangu wafugaji kuachia mifugo yao kwenye mashamba, hivyo amemwomba Rais Samia kutilia mkazo suala hilo.

“Migogoro imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo yetu, kama mtakumbuka wiki kadhaa zilizopita, mifugo iliachiwa na kuingia kwenye mashamba yetu, licha ya mkuu wa wilaya kupiga kelele, tunamwomba Rais Samia akemee hili kwa ukubwa unaostahili,” amesema Mussa.

Naye, Saruji Olesabae, mfugaji wa Mvomero, amesema baadhi ya wafugaji bado si waelewa, hivyo anafurahi kusikia Rais Samia atazindua kampeni ya “Tutunzane Mvomero” ambnayo amesema itaongeza uelewa na kukuza ushirikiano pamoja na mapato katika wilaya hiyo.

“Kampeni hii itaongeza ushirikiano na kutatua migogoro yetu, maana miongoni mwetu wamo ambao sio waelewa, bado wanaendelea kuachia mifugo kwenye mashamba licha ya uboreshwaji wa maeneo ya kunyweshea mifugo,” amesema Olesabae.

Mbali na hilo, mkazi wa Lukobe katika Manispaa ya Morogoro, Asha Hamis amesema kwa muda mrefu kilio chao cha ubovu wa miundombinu ya barabara, hali inayosababisha usumbufu na adha ya usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Ujio wa Rais Samia utakuwa na baraka na huenda kero hii ikatapata ufumbuzi, tumekuwa tukiteseka na ubovu wa barabara hasa kutoka ya Mazimbu hadi Lukobe. Barabara hii ina umuhimu mkubwa katika kuinua uchumi wetu.

“Miundombinu bora inawezesha usafiri, inachochea maendeleo ya kiuchumi, kipindi cha masika Lukobe hapitiki, tutamweleza hili Rais Samia tukipata fursa,” amesema Asha.

Wakati Asha akieleza hayo, mkazi wa Nanenane, Juma Hassan amesema kwa muda mrefu  kumekuwa na changamoto ya kupata maji safi na salama kwenye maeneo yao, hivyo amemwomba Rais Samia kulichukulia suala hilo kwa uzito wa pekee.

Hassan amesema baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Morogoro yakiwemo ya Nanenane, Tubuyu, Tungi, Mji Mpya, Mindu na Mkundi bado yanakabiliwa na changamoto ya maji, hali inayosababisha magonjwa na usumbufu mkubwa katika shughuli za kila siku za wananchi.

“Tatizo la maji limekuwa changamoto kubwa, huku kwetu tunakaa hadi siku 14 bila kupata huduma hii, halafu tupo katika manispaa, tunaamini Rais Samia ana uwezo wa kumaliza changamoto hii,” amesema Hassan.

Kwa upande wake, Fatuma Mussa, mkazi wa Mkundi amesema katika eneo hilo kuna tanki la maji lililojengwa kwa muda mrefu na kuna shida ya maji, anaamini ujio wa Rais Samia utawapa ufumbuzi kwenye kero hiyo.

“Matumaini yetu wananchi wa Kihonda yapo kwa Rais Samia, akifika tutaomba na hili la maji asiliache, tatizo hili lipate ufumbuzi wa kudumu,” amesema Mussa.

Katika hatua ya nyingine, wafanyabiashara wa soko kongwe la Mawenzi, wamesema ujio wa Rais Samia utawawezesha kueleza kero ya uchafu katika soko hilo pamoja na miundombinu mibovu ya ndani na nje ya soko hilo.

“Soko hili ndilo linaloulisha mji wa Morogoro lakini halithaminiwi, ikifika masika hatuwezi kufika kirahisi kutokana na ubovu wa barabara ambazo ni tope, tutamwomba Rais Samia atusaidie ujenzi wa barabara za lami ili wateja wafike kwa urahisi.

“Soko letu ni chafu hili nalo tutamwambia Rais Samia kinagaubaga ili ajue shida tunazopata kwenye soko letu,” amesema Amina George ambaye ni mfanyabiashara kwenye soko hilo.