Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama ajifungua sakafuni, kichanga chafariki

Muktasari:

Adai chanzo cha kifo cha mwanaye ni wauguzi waliokuwa wakisema anawasumbua na kusababisha ajifungulie sakafuni

Hai. Mkazi wa Wilaya ya Hai, Happiness Massawe (39), amegoma kuchukua mwili wa kichanga hospitalini kwa wiki moja akidai kifo cha mtoto wake kimetokana na uzembe wa baadhi ya wauguzi.

Happiness, aliyejifungua katika Hospitali ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro alisema Oktoba 31 mwaka huu alipohisi dalili za uchungu alikwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua na alipofika alipokewa na wauguzi.

Hata hivyo, alisema alipopata uchungu hakupewa ushirikiano badala yake alijifungulia sakafuni.

Juzi, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Hai, Itikija Msuya alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo akisema ameunda kamati ya kuchunguza ili kubaini kilichotokea siku hiyo.

“Kwa taarifa nilizopewa mtoto alizaliwa zero beating (akiwa amekufa) japo kuna dalili za uzembe ulifanywa na watoa huduma. Nimeunda kamati kuchunguza na watakaobainika hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema Dk Msuya.

Akizungumzia hali ilivyokuwa, Happiness alisema baada ya kupokewa hospitalini hapo alifanyiwa vipimo vyote ikiwamo ultra sound na kuambiwa itabidi alazwe asubiri wiki moja iishe kama hatojifungua kawaida, basi atafanyiwa upasuaji.

Hata hivyo, alisema Novemba 2 mwaka huu hali ilipobadilika alitoa taarifa kwa muuguzi aliyekuwa zamu, alimpima na kumjibu hasikii mapigo ya moyo ya mtoto na kumpeleka kwenye chumba cha ultra sound tena.

“Tulipofika huko yule muuguzi alimwambia mwenzake nisaidie kumpima huyu mama kwa kuwa sisikii mapigo ya mtoto na ana dalili za kujifungua. Akamjibu mnasumbua; huyu jana si alikuja hapa na nilimpima,” alisimulia Happiness.

Alidai muuguzi aliyempeleka akamwambia, “wewe mpime nataka uhakika, ndio yule muuguzi akanipima huku akisema mnasumbua. Akamuita (muuguzi) njoo usikilize si mtoto anacheza na unasikia mapigo yake. Yule (muuguzi) niliyeenda naye akaniambia nifanye mazoezi ya kutembea, nikawa nafanya hivyo, baadaye hali ikabadilika damu zikawa zinatoka mabongebonge huku nikiwa na uchungu mkali.”

Alisema alipoona hali hiyo alikwenda chumba cha kujifungulia na kumwambia muuguzi aliyekuwepo kuwa anasikia kusukuma mtoto na anatokwa damu nyingi.

“Yule muuguzi alinijibu umeweka pamba usije chafua kitanda, nikamwambia ndio nimeweka pamba lakini akaniambia niache kusumbua niendelee kutembea.”

Alisema wakati anarudi wodini kwenye kitanda alichokuwa amelala alishindwa kutembea na kumlazimu kukaa chini huku akiomba msaada kwa kuwa alikuwa akisikia dalili zote za mtoto kutoka na damu ziliendelea kumtoka.

“Manesi walikuja wakaanza kuniambia sukuma huku nikiwa chini sakafuni, nilijitahidi lakini nikawa nasikia nguvu zinaniishia, mmoja wa wauguzi akawa anamwambia mwenzake pokea mtoto si unaona kichwa kile pale.

“Mwenzake akamjibu hapana huyu hasukumi napokea nini? Nikiwa nimelala pale chini wao wako kwa pembeni wananiangalia huku wakiniambia sukuma kwa zaidi ya nusu saa nikajitahidi mtoto akatoka akaanguka chini ndipo wakamnyanyua na kuniwekea kifuani huku wakiniambia niheme kwa kuwa mtoto hakulia alivyotoka ila alianguka chini sakafuni.”

“Baada ya dakika tano bado nikiwa chini sakafuni wakaenda kumuita daktari, huku wanaendelea kumkagua yule mtoto baada daktari kuja ndio akawambia wanitoe pale chini ndipo wakaniweka kitandani na kuanza kunifanyia usafi.”

Mwanamke huyo aliiomba Serikali kuwachukulia hatua wauguzi hao akidai kifo cha mwanaye ni uzembe wa wakunga na angepewa msaada wangeokoa mtoto huyo.