Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama adaiwa kuua kichanga, azika kichwa, aficha kiwiliwili

Rombo. Mkazi wa Kijiji cha Nayeme wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Melania Tarimo anatuhumiwa kumuua mtoto wake anayekadiriwa kuwa na miezi miwili au mitatu kwa kumchinja na kutenganisha kichwa na kiwiliwili.
Melania (32), anatuhumiwa kufanya mauaji hayo akishirikiana na Priscus Daniel, maarufu Mtivei, aliyekuwa akiishi naye ambaye si baba wa mtoto huyo.

Mauaji hayo yanadaiwa kufanyika Mei, mwaka huu na kubainika Julai 7, mwaka huu.
Inadaiwa baada ya kumuua walizika kichwa kwenye eneo la nyumba hiyo na kiwiliwili kilikutwa kimefichwa katikati ya magodoro yaliyokuwepo katika chumba walichokuwa wakiishi.

Pia inadaiwa walizika kwenye eneo la nyumba walikokuwa wakifanya kazi ambayo mmiliki wake anaishi mkoani Arusha.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema baada ya kupokea taarifa walianza uchunguzi na Julai 6, mwaka huu waliwakamata watu wawili ambao ni mke na mume.

Amesema walipata taarifa kutoka kwa jirani kwamba mtoto wa Melania ambaye ni wa kike amekuwa haonekani na hajulikani.

Kamanda Maigwa amesema walifanya uchunguzi na kubaini mtoto huyo alishafariki dunia na kuzikwa bila kushirikisha viongozi wa kijiji, ndugu, majirani wala mmiliki wa eneo alikozikwa.

Amesema waliwakamata watuhumiwa na baada ya kupata kibali na kufukua kaburi walikuta mabaki ya fuvu la kichwa na vipande vya nguo.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Deogratius Maruba alisema mwili wa mtoto huyo ukiwa umeharibika ulipokewa na kuhifadhiwa katika kituo cha afya Karume.

"Julai 8 mwaka huu katika kituo chetu cha afya Karume tulipokea mwili wa mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi miwili mpaka mitatu ambao ulikuwa umeharibika," amesema.

Amesema walitoa taarifa kituo cha polisi Usseri kwa hatua nyingine.
Tukio lilivyobainika.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kitakura, Eva Moshi aliyekuwa miongoni mwa waliobaini tukio hilo amesema akiwa kwenye majukumu yake ya kazi alipigiwa simu na kuelezwa kuwa Melania hajaonekana kuwa na mtoto kwa muda mrefu, ndipo alipomtafuta ili kupata ukweli.

“Julai 5, mwaka huu nilienda kwa mama huyo nikamuuliza mtoto yuko wapi, akaniambia yupo nyumbani, nikamwambia twende ukanionyeshe.
“Nilipofika nyumbani kwake akaniambia mtoto yupo kituo cha watoto yatima cha Ngaleku, hapo nikaanza kupata wasiwasi," alidai Eva.
Alieleza baada ya kumtaka waende kwenye kituo hicho, alikataa na kumtaka amweleze ukweli.

“Aliniambia mtoto aliugua akampeleka hospitali, jioni waliporudi alizidiwa akafariki dunia na kwamba walimzika yeye na mume wake,” alidai.
Mwenyekiti huyo alieleza aliingiwa wasiwasi, ndipo alipokwenda kutoa taarifa kituo cha polisi.

"Ilibidi nichukue bodaboda kwenda naye kituo cha polisi. Tulipofika nikaeleza hali ilivyo, askari walimbana ikabidi aseme ukweli wa tukio lilivyokuwa, alikiri kuzika mtoto huyo na mumewe na kwamba walimuua," amedai.

Amedai kichwa cha mtoto kilipatikana kikiwa kimechimbiwa ndani ya geti la nyumba ya bosi wake na kiwiliwili kilikutwa kimefunikwa katikati ya godoro.
Ameeleza baada ya Melania kupata mwanaume mwingine walioshirikiana kufanya mauaji, walikuwa wakigombana kuhusu mtoto huyo na kuna wakati walimtupa.

“Mara kadhaa wamekuwa wakirushiana mtoto, mwanaume alikuwa akimwambia sio wake ndiyo maana wakaamua kumuua ili wazae mwingine," amedai.
Peter Tesha, mkazi jirani na nyumba kilikozikwa kichwa cha mtoto huyo alisema aliitwa eneo la tukio akiwa mkazi wa jirani polisi walipokwenda kufukua.

Tesha amesema mwenye nyumba hakuwepo, lakini alipopewa taarifa alifika na kwenda kuripoti polisi na baada ya uchunguzi walibaini kiwiliwili kilichokuwa kimefichwa kwenye magodoro.