Makonda awaonya wabunge, wawakilishi wasiojituma

Muktasari:
- Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda ameanza ziara ya mikoa 20 kukagua uhai wa chama hicho na kusikiliza changamoto za wananchi akisema CCM haitawavumilia wabunge, wawakilishi madiwani wasiotimiza wajibu wao.
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema wabunge, wawakilishi na madiwani wasiotimiza wajibu wao wasitarajie kuteuliwa tena kupeperusha bendera ya chama hicho katika chaguzi zijazo.
Amesema chama hicho kina timu ya kutosha ya kuchukua taarifa na kuzifikisha kwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua zaidi.
"Tutamwambia tu mwenyekiti wetu Taifa (Rais Samia Suluhu Hassan) kwamba tukienda na huyu tutapigwa, yapo mambo mengi yaliyotekelezwa na Serikali lakini sauti zinazosikika ni chache, wakati kazi ya mbunge ni kupambania mgawanyo wa keki ya Taifa," amesema Makonda.
Makonda ameeleza hayo leo Ijumaa Januari 19, 2024 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Bunju akiwa njiani kuelekea Bagamoyo mkoani Pwani, kuanza ziara ya mikoa 20 iliyopewa jina la 'back 2 back'.
Katika ziara hiyo yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi, Makonda atatembelea mikoa mbalimbali ikiwemo Pwani, Tanga, Arusha na Kilimanjaro.
Kazi ya mbunge
Makonda amesema kazi ya mbunge akiwa bungeni mkoani Dodoma ni kuhakikisha anaipambania keki ya Taifa sambamba na kulipambania jimbo lake ikiwemo kufanya mikutano na kukaa na wananchi wanaowaongoza kupokea changamoto zinazowakabili.
"Nilishasema sitabeba mzigo, kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe kama mbunge. Wajibu wa CCM ni kutatua kero za wananchi, kama hatutatui hatuna haki, ni jukumu letu kupunguza changamoto hizi, kama kuna mbunge au diwani tutawapima kwa kazi, sio maneno au kugawa kanga wakati wa uchaguzi ili kuwarubuni wajumbe na kujipendekeza wa viongozi.
"Tukienda kwa wananchi wakisema naam, mbunge wetu ndio aliyepambania barabara au shule ikajengwa, kauli hizi ni kigezo kimojawapo cha kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM," amesema Makonda.
Amesema CCM itahakikisha inawapata wabunge waadilifu ili kuwa sauti ya wananchi wanaowawakilishi kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika majimbo yao.
Kauli hiyo Makonda ni kama amepigilia msumari maelezo yaliyotolewa na Januari 17 na mwenyekiti wake Rais Samia aliyesema matendo ya wabunge na wawakilishi wanaoisaidia Serikali kutatua changamoto za wananchi yatakuwa ni kipimo cha kuwapata wanaostahili katika chaguzi mwakani.
Samia alitoa kauli hiyo katika ziara yake kichama katika mikoa minne ya Zanzibar huku akionya tabia ya viongozi na wawakilishi kutoa zawadi za khanga, vitenge na fedha unapokaribia uchaguzi ili kushawishi wanachama wawachague, akisema hiyo ni ishara kuwa anayefanya hivyo hajatekeleza wajibu wake kikamikifu.
Katika hatua nyingine, Makonda ameendelea kupinga maandamano yaliyoitishwa na Chadema Januari 24 akiwataka wakazi wa Dar es Salaam, kutojihusisha nayo, akidai yanapotosha umma.
Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza maamuzi ya kamati kuu aliyoyaita vuguvugu la kudai haki, litakaoambatana na maandamano ya amani ili kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau demokrasia ya vyama vingi kuhusu miswada mitatu ya sheria za uchaguzi na hali ngumu ya maisha.
Baada ya kutangaza hatua hiyo, Makonda aliwataka viongozi hao kukaa meza moja katika mdahalo ili Watanzania kuchagua kama wataendelea na maandamano au maridhiano.
Hata hivyo, Chadema ilitoa masharti matano likiwemo la Serikali iondoe kwanza miswada mitatu waliodai ni mibovu bungeni inayohusu sheria za uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa.
Pia, Chadema iliitaka Serikali ianzishe mara moja mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 na iwasilishe bungeni muswada wa Sheria ya kukwamua mchakato wa Katiba mpya ukiwa na jibu la lini nchi itapata Katiba mpya.
Masharti hayo yalikataliwa na Makonda kidai kuwa utekelezaji wake utavunja sheria za nchi.
Pia alisema hatua Chadema kuweka masharti hayo ni kujitoa kwenye mdahalo aliouihitisha.
"Ndugu wananchi muulizeni kaka yangu Mbowe, Mnyika (John) na Tundu Lissu mbona wanamkimbia Makonda kwenye mdahalo? Ninawaita kwenye mdahalo kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kwa Watanzania," amesema Makonda.