Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makonda asikiliza kero tisa kwa siku tano

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akisukuma mkokoteni wenye ndizi kuashiria ujio wake katika wilaya ya Hai, kabla ya kwenda Arusha.

Muktasari:

  • Kila jambo na mtu wake, ndivyo unavyoweza kusema kuhusu ziara ya siku tano aliyoifanya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda katika mikoa ya Tanga, Pwani na Kilimanjaro, ambapo zaidi ya kero tisa zilizokuwa zikiwasumbua wananchi wa mikoa hiyo zimepatiwa dawa.

Moshi. Ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda katika mikoa ya Tanga, Pwani na Kilimanjaro, amesikiliza zaidi ya kero tisa zilizokuwa zikiwasumbua wananchi wa mikoa hiyo.

Miongoni mwa changamoto hizo zilizowasilishwa kwa nyakati tofauti kwa Makonda na kupatiwa ufafanzi, ni pamoja na huduma mbovu katika hospitali na vituo vya afya, kutokamilika kwa wakati na stendi ya mabasi ya Ngangamfumuni, kuchelewa kwa ujenzi wa soko la samaki Manyema na huduma za maji.

Changamoto nyingine ni malalamiko ya kodi kubwa katika maduka yaliyopo stendi kuu ya mabasi Moshi, ujenzi wa soko, uvamizi wa wanyamapori waharibifu na malipo ya fidia kwa waathirika wa wanyama hao.

Makonda alizipokea na kujibu kero hizo wakati mwingine hadi usiku, huku nyingine akiwaachia mzigo wakuu wa mikoa na wilaya kuzitatua na kumpa mrejesho.

Makonda yupo katika awamu ya pili ziara ya mikoa 20 iliyopewa jina la 'back 2 back' inayolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa mikoa mbalimbali sambamba na kuangalia shughuli za utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25.

Ziara hiyo ilianzia Bagamoyo mkoani Pwani  Januari 19, 2024  kisha kuingia Tanga Januari 20, 2024 ambapo alikutana na kero ya maji katika mji wa Mkata, wilayani Handeni ambapo Makonda alimtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kujibu kero hiyo, ambaye aliwaagiza watalaamu kushughulikia suala hilo kwa haraka.

Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja Lamore Tanga mjini, Makonda alitoa mrejesho wa tatizo hilo la maji kupatiwa ufumbuzi na kwamba wakazi wa Handeni wataanza kupata huduma hiyo, huku akimpongeza Aweso kwa jitihada hizo.

Kero nyingine iliyokuwa ikisumbua ni huduma za afya katika Hospitali ya mkoa wa Tanga - Bombo, ambapo alisema: "Ninazo taarifa hapa Tanga, watu wananyanyasika, wanateseka, hawapati huduma, wajawazito wanajibiwa vibaya na vifaa vya hospitali vimeharibika watu wanakosa huduma.”

Baada ya maelezo hayo, Makonda alimtaka Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Japhet Simeo kushughulikia changamoto ya zahanati, vituo vya afya vilivyobaki ili kuboresha huduma za afya mkoani Tanga.

"Wako baadhi ya watumishi katika zahanati au kituo cha afya hawatoi huduma muda wote wapo na simu wanachati, wengine wanauza dawa, nimeyabaini haya kaka (Dk Simeo) nipo 'serious' simamia hili," alisema Makonda.

Akijibu hilo, Dk Simeo alisema "Kuanzia Jumatatu (Januari 22, 2024), Bombo itakuwa na uongozi mpya utakaosaidia kubadilisha safu nzima ya utendaji kazi wa hospitali hii," amesema.

Akiwa katika maeneo ya Himo, Hedaru, Same, Mwanga na Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro wananchi walijitokeza wakiwa na mabango yaliyoandikwa kero mbalimbali wakiomba Makonda kuwasaidia kupata ufumbuzi.

Akiwa katika mkutano wa hadhara katika maeneo ya stendi kuu ya mabasi katika Manispaa ya Moshi, Makonda alipewa changamoto kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa stendi ya kisasa ya Ngangamfumuni.

Baada ya kero hiyo, Makonda alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe kujibu ambapo alisema: “Mkandarasi alicheleweshewa malipo toka wizarani, sasa baada ya changamoto hiyo, tumeona Manispaa tuwe na bajeti katika mapato yetu ili pale wizara inapochelewa kulipa, tulipe sisi ili mkandarasi asikwame, tunaomba tupewe miezi sita baada ya mkandarasi kurudi eneo la kazi  tukamilishe," alisema.


Kodi maduka ya stendi

Baadhi ya wafanyabiashara wa Moshi walilalamikia kutozwa kodi kubwa katika maduka ya stendi, wakimuomba Makonda kuingilia kati kutatuta changamoto hiyo, ambapo aliagiza Baraza la madiwani la manispaa hiyo kuketi mara moja kujadili suala hilo na kutoa majibu papo hapo.

Baada ya kukaa kwa muda mfupi Meya wa Manispaa hiyo, Zuberi Kidumo alitoa taarifa kuwa: "Tumekaa hapa kama ulivyotuagiza, awali kodi ilikuwa Sh1 milioni tukashuka hadi Sh450,000, lakini kwa mujibu wa sheria, bajeti ikishapitishwa na Bunge huwezi kuibadilisha hadi upate kibali kutoka kwa Katibu Mkuu," amesema.

Zubeir amesema wamekubaliana na madiwani wenzake kwenda kubadilisha kwenye bajeti inayokuja, kwa kuondoa Sh50, 000 kwa kila eneo kuanzia sakafu ya chini hadi ile ya pili.

Katika mkutano huo pia wananchi waliwasilisha malalamiko ya kutojengwa kwa soko la samaki wabichi la Manyema, licha ya kuahidiwa mara kadhaa na viongozi wa CCM na Serikali waliokwenda wilayani hapo.


Akijibu malalamiko hayo, Nasombe alisema eneo hilo la soko lilikuwa ni la wazi, lakini kwa sasa wameomba kibali cha kubadilisha matumizi yake  ili ujenzi huo uanze.

Baada ya majibu hayo, Makonda alipiga simu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi, Anthony Sanga kutaka kujua mchakato wa kibali hicho umefikia wapi ambapo mtendaji huyo aliahidi kukitoa ndani ya siku mbili.


Uvamizi wa tembo na kero ya maji

Kuhusu changamoto ya maji katika Wilaya za Same na Mwanga, Makonda alipiga simu kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na kumuelekeza kuhakikisha mradi mkubwa wa maji, Same-Mwanga-Korogwe unakamilika kwa wakati ili wananchi wapate maji.

Makonda pia alipiga simu kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki akimtaka awaeleze wananchi mpango wa kushughulikia changamoto ya uvamizi wa tembo kwenye makazi ya watu, pamoja na suala la kifuta machozi.


Akijibu kero hiyo, Waziri Kairuki alisema mbali na mpango wa kujenga vituo vya kudhibiti wanyama hao katika maeneo ya Mwanga na Same, pia wamejipanga kupeleka ndege dogo ili kuwafukuza na kuwadhibiti kuingia katika makazi ya wananchi.

“Kuhusu kifuta jasho na kifuta machozi kwa sasa Mwanga tunafanya uhakiki, Same tayari tumeshafanya na kuwasilisha maombi Wizara ya Fedha, mwezi huu tukipata fedha, tutalipa madai ya watu wa Same ambayo ni takribani Sh243 milioni," alisema Kairuki.

Aidha, mmoja wa wakazi wa Moshi, Ndeinengo Mushi amesema bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili wananchi, huku akidai sababu ni tabia ya kutotafuta ufumbuzi inayoonyeshwa na baadhi ya viongozi kuanzia ngazi ya chini.

Kwa upande wa Jones Mola ambaye pia ni mkazi wa Moshi amesema: “Kuna wananchi wanaumizwa na kuonewa katika jamii lakini hawana pa kusemea, ndiyo maana jana katika mkutano wa Moshi hadi  usiku wananchi walikuwa wanawasilisha kero na hawataki mkutano uishe, hili ni tatizo na linaonyesha mahali kuna shida kwa viongozi wetu wa chini," amesema.

Leo Jumanne Januari 23, 2024 Makonda na msafara wameanza ziara katika Mkoa wa Arusha akitarajiwa kuhitimisha kesho Januari 24, 2024n kabla ya kuelekea mkoani Manyara.