Makonda aanza makeke Arusha, akemea wanaojipendekeza

Muktasari:
- Akiwa na siku 12 tangu alipoanza kazi ya ukuu wa Mkoa wa Arusha, Makonda amewaonya watumishi wa Serikali wanaopenda kusifia viongozi, akiahidi kuwapima kwa utendaji wa kazi.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema kumekuwa na watendaji wengi wenye kasumba za unafiki na kujipendekeza tena wasioweza kazi, bali wanachoweza kufanya ni kusifia viongozi pekee.
Alitoa kauli hiyo leo Aprili 21, 2024 wakati akizungumza na viongozi na watendaji wote wa mkoa huo katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).
Akiwa na siku 12 tangu kuanza kuongoza rasmi Arusha, Makonda amesema aliamua kukutana na viongozi hao ili watu alionao katika utumishi wajue aina ya mtu anayewaongoza ili wakikanyagwa mahali wasilie.
Kwanza ameanza kwa kumkosoa mshereheshaji ambaye awali alimsifia kwa kusema kuwa ameanza kazi apigiwe makofi.
“MC (mshereheshaji) nimemsikia anasema baba baba tumpigie makofi ameanza kazi, kazi yenyewe sijaanza ndiyo kwanza bado najifunza makofi ya nini, kupambana pambana huku ndiyo kunatufanya tuishi maisha tofauti na wananchi tunaowaongoza,” amesema Makonda.
Amesema hali hiyo imekuwa ikiwafanya wananchi wanaoongozwa kuwatazama viongozi kwa jicho la tofauti na viongozi kuhisi wako katika dunia yao tofauti jambo linalofanya wananchi kushindwa kujivunia uwepo wao.
“Hivyo kitu namba moja lazima tukubaliane, hakuna sababu yoyote ya kusifiana sifiana acha kazi ziongee, tunahitaji kufanya kazi kama timu, timu ya mpira inapopata matokeo mazuri kila mtu anatambua nafasi ya mwenzake, hivyo ni muhimu mkoa wetu hadi ngazi ya kata na mitaa tukajenga tabia ya kufanya kazi kama timu,” amesema Makonda.
Katika hilo aliwaomba watumishi wa umma msamaha kwa kile alichoeleza kuwa, kasi na kibano watakachokipata kwenye ofisi zao zitawataka kufanya kazi kwa kujituma huku akiwaonya waliozoea kujikongoja.
“Kama umezoea kwenda taratibu halafu ukategemea tutachukuliana poa, hiyo hapana, nakuomba radhi mapema sana wewe na familia yako ya kwamba kitakachokukuta nilishakuomba msamaha.
“Sitaweza kumvumilia mtu mzembe, asiyewajibika, mwenye kila sababu ya kushindwa kufanya kazi huku akiwa amekaa kwenye kiti cha uongozi wa kufanya maamuzi.
"Mimi nataka kuweka alama sio kulinda kiti, ndio maana kuna watu wamekaa kwenye madaraka muda mrefu lakini ukimuuliza anasema nilikuwa pale nikatoka nikaenda pale nikatoka, nikaenda pale lakini ukimuuliza umeacha nini ulipotoka na hapo unapoenda unatarajia kuacha nini majibu yanabaki kuwa hakuna,” amesema Makonda.
Amesema yeye ni tofauti na watu wengine ambao Mungu amewapa neema ya kuwatengeneza watu na badala yake yeye anataka mtu aliyekamilika.
“Habari ya kwamba tutavumiliana au labda utaimarika huko mbele ieleweke huo muda kwangu haupo, kuna muda watu wengine wanasema twende nao taratibu mbele ya safari anaweza kuwa sawa, yaani kuvumilia hiyo hasara mpaka mbele ya safari mimi sina kwa sababu mimi mwenyewe napimwa kwa siku, kwa hiyo siwezi kukubali leo unatoa taarifa hii na kesho unakuja unatoa taarifa ile,” amesema Makonda.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha, Suleimani Msumi amesema mwaka 2022/23 moja ya mradi uliofanyika ni wa shule ya sekondari mpya ambayo imegharimu Sh500 milioni na sasa kinachomaliziwa ni maabara za sayansi.
“Shule hii imepunguza umbali waliokuwa wakitembelea wanafunzi tofauti na sasa, pia imesaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi na kuzuia utoro,” amesema Msumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha, Justine Rujomba amesema kwa sasa uhitaji wa maji ni lita milioni 123 kwa siku huku uzalishaji ukiwa zaidi ya lita milioni 200.
meisema kupitia mradi mkubwa uliotekelezwa, visima 56 vya maji vilichimbwa vilivyozalisha maji, mtandao wa majisafi wenye zaidi ya kilometa 200 ulijengwa huku matanki na wateja wapya wakiungwa.
“Kabla ya mradi mkubwa tulikuwa na wateja 40,000 lakini hadi sasa wateja zaidi ya 124,000 huku upatikanaji maji ukiwa asilimia 99,” amesema Rujomba.
Kikao hicho kilichodumu kwa takribani saa tano pia kilisikiliza ripoti kutoka kwa watendaji mbalimbali huku kikiambatana na uchukuaji wa hoja na maswali mbalimbali kutoka kwa wananchi.
Kufuatia suala hilo na mikanganyiko ya taarifa iliyokuwa ikitolewa na watendaji kikaoni, Makonda alisema katika kile kilichofanyika, hajaridhishwa na uwezo wa watendaji wa mkoa huo.
Amesema kama ni asilimia hazijafika hata 50 na badala yake wako katika asilimia 30 huku akiwaomba radhi kwa kile alichokieleza kuwa hajui kupindisha maneno.
Amesema utendaji uko chini ya kiwango ukilinganishwa na ule ambao viongozi wa juu wanautegemea huku akilinganisha na baadhi ya maeneo ambayo amewahi kupita huku alipokutana na vijana wadogo ambao wanakuwa na taarifa za kina.