Makandarasi wazawa waonywa, Takukuru watia mguu

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati akifungua mkutano wa 32 wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) jijini Arusha.
Muktasari:
- Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaonya makandarasi wazawa waache kutekeleza miradi ya ujenzi chini ya viwango kwa kuwa wanaitia hasara Serikali lakini wanajiweka katika hali ngumu ya kupata kazi nyingine.
Arusha. Serikali imeagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia na kuchukua hatua stahiki makandarasi wazawa wanaojenga miradi chini ya kiwango na wale wanaoitelekeza.
Maagizo hayo yametolewa jana Alhamisi, Novemba 30, 2023 jijini Arusha na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akifungua mkutano wa 32 wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET).
Amesema inasikitisha kuona na kusikia baadhi ya makandarasi wazawa kushindwa kutekeleza miradi kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuendekeza vitendo vya rushwa vinavyoisababishia Serikali hasara.
"Kiukweli tujitathmini na tusaidie Serikali katika utekelezaji wa miradi katika maeneo mbalimbali, tuna changamoto ya baadhi ya miradi kutekelezwa chini ya kiwango na kusababisha upotevu wa fedha za umma," amesema na kuongeza;
"Lazima tuwalaumu nyie makandarasi wazawa na kusababisha kazi nyingi ziende kwa makandarasi wa nje. Naomba muwe walinzi wa kwanza wa rasirimali hizi za nchi, Takukuru pia mkamate wanaohusika na ujenzi wa miradi chini ya kiwango ili wawe mfano kwa wenzao."
Rais wa IET, Dk Gemma Modu ameshukuru Serikali kwa kuongeza kuwapa kazi wahandisi wazawa kwenye miradi ya kimkaakati inayoendelea nchini.
"Hali hii ikiendelea itasaidia kufungua kiwango cha kazi kwa wahandisi wazawa pamoja na kuwainua kiuchumi pamoja na kuongeza ajira kwa wengine, ukizingatia wahandisi wa mchango mkubwa wa kuleta maendeleo endelevu nchini," amesema Rais huyo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa taasisi hiyo ya makandarasi, Asa Mwaipopo amesema mkutano huo wa siku tatu umeshirikisha wahandisi zaidi ya 800.