Majukumu mapya kwa Pindi Chana katika urais mkataba wa Lusaka

Waziri wa maliasili na utalii, Balozi Pindi Chana akipokea makabrasha ya Ofisi ya urais mpya wa Baraza la uongozi la nchi wanachama wa mkataba wa Lusaka kutoka kwa waziri wa wanyamapori Kenya Rebecca Miano
Muktasari:
- Balozi Pindi Chana amekabidhiwa jukumu hilo rasmi leo Mei 8, 2025 kwenye mkutano wa 14 wa Baraza la Uongozi la Nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka, uliofanyika kwa siku tatu jijini Arusha.
Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana amekabidhiwa jukumu la kuongoza mapambano ya kudhibiti na kukomesha uhalifu wa kimazingira unaovuka mipaka, ikiwemo biashara haramu ya nyara, wanyamapori na mazao ya misitu.
Jukumu hilo limeanza leo Mei 8, 2025 baada ya kukabidhiwa rasmi jukumu la kuongoza Baraza la Uongozi la Nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka.
Dk Chana anachukua nafasi ya Waziri wa Wanyamapori wa Kenya, Rebecca Miano, aliyemaliza muda wake wa uongozi wa miaka miwili kuanzia mwaka 2022.
Mkataba wa Lusaka ni makubaliano ya kikanda yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika, katika kudhibiti na kukomesha uhalifu wa kimazingira unaovuka mipaka, ikiwemo biashara haramu ya nyara, wanyamapori na mazao ya misitu.
Dk Chana atahudumu katika nafasi hiyo kuanzia mwaka huu 2025 hadi 2027, ambapo atakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa Mpango mpya wa Mkakati wa Miaka Mitano (2025–2030), uliolenga kuimarisha vita dhidi ya uhalifu wa mazingira unaovuka mipaka kwa ushirikiano na wadau wa kitaifa, kikanda na kimataifa.
Mpango huo umetayarishwa katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Uongozi la Nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka uliofanyika jijini Arusha kwa siku tatu, na sasa unasubiri kuidhinishwa rasmi na Baraza ili uanze kutekelezwa.
Pamoja na hilo, Dk Chana pia atakuwa na jukumu la kuongoza vikao vya maamuzi ya juu, kuratibu utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na uhalifu dhidi ya wanyamapori na kuhakikisha nchi wanachama zinatekeleza kwa ufanisi maazimio ya mkataba huo.
Ushirikiano na wadau wa kimataifa pia utakuwa jukumu lake muhimu ya majukumu yake mapya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, aliyekuwa Rais wa Baraza, Rebecca Miano, ameeleza kuwa wahalifu wa mazingira wanaendelea kubadilika na kutumia teknolojia mpya kila mara, hivyo akahimiza uongozi mpya kuweka kipaumbele katika ubunifu wa kiteknolojia kama njia ya kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu huo.
Alizitaka pia nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano na mshikamano wa pamoja ili kukomesha biashara haramu ya nyara, wanyamapori na mazao ya misitu inayovuka mipaka.
“Ushirikiano na ubunifu wa kiteknolojia vitakuwa nyenzo muhimu katika kukabiliana na vita hii. Maamuzi yetu ya leo ndiyo yatakayoamua mustakabali wa vizazi vijavyo,” amesema Miano.
Akizungumza mara baada ya kupokea nafasi hiyo, Dk Chana amesema ni heshima kubwa kwa Tanzania kuaminiwa kuongoza nafasi hiyo muhimu na akaahidi kuitumikia kwa uadilifu na dhamira ya kweli katika kulinda rasilimali za utalii na mazingira barani Afrika.
“Ishara ya mshikamano wa mataifa ya Afrika katika kukabiliana na vitisho vya kimataifa dhidi ya bayoanuwai yetu, uchumi wetu na hata uhuru wetu, naahidi kuwatendea haki kwa kushirikiana nanyi wote pamoja tutashinda,” amesema.
“Tunapozungumzia ushirikiano, tusisahau wajibu wetu wa kuchangia ubunifu, si tu katika teknolojia, bali pia katika mifumo ya utawala inayowawezesha wananchi, kuwakwamisha wahalifu na kuwatambua wanaojitolea kwa ajili ya uhifadhi.”
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkataba wa Lusaka, Edward Phiri amesema kuwa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2025–2030) tayari umewasilishwa kwa Baraza la Uongozi kwa ajili ya kuidhinishwa.
Ameeleza kuwa mpango huo unaweka dira mpya ya kupambana na ujangili na uhalifu wa kimazingira kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa.
“Mpango huu unalenga kuimarisha utekelezaji wa sheria kwa kutumia teknolojia ya kisasa, kuendeleza ushirikiano wa kijasusi, kukuza uwezo wa taasisi na kuimarisha mshikamano wa kikanda kupitia jumuiya kama EAC, SADC na Ecowas,” amesema Phiri.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka nchi wanachama kuhakikisha kuwa Kikosi Kazi cha Mkataba wa Lusaka kinadumu na kinakuwa na nguvu inayoongoza barani Afrika, katika mapambano dhidi ya uhalifu wa wanyamapori na misitu.