Maji yaongezeka Ziwa Victoria, wananchi watahadharishwa

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Mhandisi Gerlad Itimbula akionesha kipimo cha maji kilivyo ongezeka Ziwa Victoria. Picha na Saada Amir

Muktasari:

 Imeelezwa kuwa, hata mwenendo wa mtiririko wa maji katika mito mkubwa ndani ya Bonde la Ziwa Victoria pia umeongezeka

Mwanza. Wastani wa usawa wa maji katika Ziwa Victoria umeongezeka kutoka milimita 1134.00  za wastani wa kina kutoka usawa wa bahari kwa mwaka  2023 hadi kufikia usawa wa maji  milimita 1134.86 kwa vipimo vya Aprili 24, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bonde la Ziwa Victoria jijini Mwanza leo Aprili 26, 2024, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Gerald Itimbula amesema huo ni usawa mkubwa zaidi kufikiwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50 sasa.

“Wingi huu wa maji unavunja rekodi iliyowekwa Mei 2020, wingi ulikuwa 1134.84 wastani wa kina kutoka usawa wa bahari,”amesema.

Amesema hata mwenendo wa mtiririko wa maji katika mito mkubwa ndani ya Bonde la Ziwa Victoria pia umeongezeka.

Amesema kituo cha Mto Kagera kinaonesha wastani wa mtiririko wa maji umeongezeka kutoka 198.28 mita za ujazo kwa sekunde mwaka 2023 (Januari hadi Machi) hadi 325.19.

Amewataka wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji na wanaofanya shughuli zao katika mialo na kandokando ya vyanzo vya maji na wenye miundombinu kwenye maeneo hayo, kuchukua tahadhari juu ya ongezeko hilo.

“Utabiri unaonesha mvua zinaendelea kunyesha, hivyo kuna uwezekano wa maji kuongezeka zaidi,”amesema Itimbula.

Mmiliki wa boti katika jiwe la Bismark lililopo Kamanga Mwanza, Revocatus Matias amesema wanashangazwa na uongezeko la maji katika ziwa hilo akidai sio lakawaida.

"Maji yameongezeka sana mpaka yameanza kumega barabara hii sio kawaida mfano bustani ya hapa Kamanga yote saizi imemezwa na maji mpaka vijana waliokuwa wamejiajiri hapa wameondoka baada ya maji kujaa," amesema Matias.

Mmliki wa Bustani katika jiwe la Bismark, Christopher Pangani akiunga hoja hiyo ametoa wito kwa wadau wa mazingira na mamlaka za mazingira kuzidi kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi.