Maji ya mvua yajaa mgodini, wawili wahofiwa kufa

Vipande vya dhahabu
Muktasari:
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema tayari askari wa uokozi wako eneo la tukio kusaidiana na vikosi vingine vya uokoaji vilivyopo eneo hilo.
Bunda. Wachimbaji wawili wanahofiwa kufariki dunia baada ya maji kujaa ndani ya mgodi dhahabu wa Kunanga ulioko eneo la Kinyambwiga Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano, wtu hao ambao bado hayajatambuliwa wamekubwa na janga hilo katika tukio lililotokea Oktoba 17, 2023.
‘’Watu hao waliingia mgodini kama kawaida lakini wakati wanaendelea na shughuli zao, mvua ilianza kunyesha na maji kuingia ndani ya shimo la mgodi,’’ amesema Dk Naano alipozungumza na Mwananchi leo Oktoba 19, 2023.
Amesema vikosi vya uokoaji kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo chimbaji vinaendelea na juhudi za kuwaokoa watu hao ambao matumaini ya kuwaokoa wakiwa hai yanazidi kufifia kutokana na muda waliokaa tangu maji ya mvua yalipojaa mgodini.
‘’Juhudi za kuvuta maji kutoka mgodini zinaendelea tangu jana lakini hadi sasa maji bado yanaonekana yako mengi mgodini na kwa bahati mbaya mashine za kunyonya maji zinazotumika zinazidiwa kutokana na wingi wa maji,’’ amesema Mkuu huyo wa wilaya
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema tayari askari wa uokozi wako eneo la tukio kusaidiana na vikosi vingine vya uokoaji vilivyopo eneo hilo.
Kwa mujibu wa Dk Naano, shimo la mgodi walimoingia watu hao inakadiriwa kuwa na kina cha zaidi ya mita 150.