Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majanga tena Kariakoo

Moto ukiungoza jengo katika eneo la Karikoo, jijini Dar es Salaam jana Jumapili, Oktoba Mosi, 2023. Picha na Michael Matemanga

Dar ea Salaam. Zilikuwa saa sita za mshikemshike wa watu kuokoa maisha na mali zao, kudhibiti moto ulioanzia eneo la Mnadani Kariakoo na kusambaa katika majengo mengine jirani, ikiwemo migahawa na fremu za maduka na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.

Pia, kwa muda huo Barabara ya Msimbazi ilifungwa kupisha shughuli za uokoaji na kuzima moto huo uliokuwa ukisambaa kwa kasi katika majengo kwenye makutano ya mitaa ya Msimbazi Mafia, Mkunguni, Congo na Nyamwezi.

Moto huo kwa mujibu wa mashuhuda ulianza saa 12 asubuhi katika eneo la Mnadani, ambalo ni maalumu kwa biashara ya vipuri vilivyotumika vya magari na vyuma chakavu.

Wakati moto unatokea, baadhi ya wamiliki wa maduka na wafanyabiashara walikuwa wamefunga maduka yao kwa kuwa ama ilikuwa mapema asubuhi au Jumapili, siku ambayo huwa hawayafungui.

Ingawa, wengi wao walifika haraka kunusuru bidhaa zao zisiteketee, si wote waliofanikiwa kuziokoa, hivyo baadhi yao kujikuta wakibubujikwa na machozi baada ya kukuta zimetetekea.

Ilikuwa ni kupigiana simu kujulishana kuhusu moto ambao kadri muda ulivyozidi kwenda ulikuwa ukisambaa katika maeneo mengine mapya huku juhudi za kuudhibiti zikiendelea

Pamoja na kuwepo magari ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wakazi wa eneo hilo na baadhi ya wafanyabiashara walitaka kutumia mbinu mbalimbali za kuokoa mali bila mafanikio kutokana na moto kusambaa kwa kasi.

Moto huo ulisambaa hadi katika Jengo la Big Bon lenye ghorofa tatu, ambalo liliungua upande wake lakini tawi la Benki ya Afrika (BoA) lililoko chini halikuathirika zaidi.

Mashuhuda walisikika wakisema moto huo ungesababisha madhara makubwa zaidi iwapo kituo cha mafuta cha Big Bon kilichokuwa katika eneo hilo kisingehamishwa wiki kadhaa zilizopita.

Hadi saa sita mchana sehemu kubwa ya moto huo ulikuwa umedhibitiwa.

Zimamoto waudhibiti

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Ilala, Mrakibu Mwandamizi Elisa Mugisha alisema, “tulipata taarifa saa moja asubuhi hadi kufika eneo la tukio tulitumia dakika mbili kwa kuwa ofisi yetu iko jirani na eneo la tukio.”

Hata hivyo, alisema kutokana na changamoto ya ufinyu wa njia za kupita moto huo ulisambaa kwa kasi.

Mugisha aliyesema chanzo cha moto kilikuwa hakijafahamika, alibainisha kuwa walilazimika kuomba magari ya maji kurahisisha shughuli ya uzimaji, kwa kuwa kitendo cha kwenda kujaza na kurudi moto ungekuwa umeanza upya.

Alisema licha ya kuwa na vituo vya maji kwa ajili ya tahadhari vipo karibu na eneo hilo, kwa jana maji hayakuwa na presha, hivyo ikawalazimu kwenda kuchota kwenye kituo cha Zimamoto maarufu kama eneo la Fire.

Kamanda huyo alisema baada ya kuzima moto huo, wangefanya uchunguzi kubaini chanzo na kuchukua tahadhari ya matukio mengine kama hayo yasijirudie.


Msimbazi yafungwa

Tukio hili lilisababisha usumbufu baada ya Barabara ya Msimbazi kufungwa kwa muda mrefu kupisha shughuli za uokoaji.

Kutokana na hali hiyo, vyombo vya usafiri vililazimika kutumia njia mbadala, baada ya barabara hiyo kufungwa kwa utepe mwekundu na magari ya polisi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo-Kaskazini, Konde Mketwa alisema kufuatia tukio Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, walikuwa bega kwa bega pamoja na wananchi katika jitihada za kudhibiti moto huo.

“Kwa hapa tunalo tatizo, hawa wanaojenga haya majengo, kuna nafasi zinazotakiwa kuachwa wazi baina ya nyumba na nyumba ili tatizo la moto linapotokea lizimwe kwa urahisi,” alisema Mketwa.

Hata hivyo, Mketwa alisema shughuli za kuuzima zilikuwa zikiendelea vema.

Kilio cha wafanyabiashara Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Matilda Kalonga alisema tukio hilo limewaathiri kwa kiasi kikubwa na wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia namna ya kuwasaidia.

Alisema miongoni mwa walioathirika ni pamoja na mama lishe, wauzaji wa vipuri, fremu za nguo na biashara nyingine mbalimbali, akidai watu zaidi ya 1,000 wamekumbwa.

Mtendaji Mkuu wa Kariakoo Auction Mart (Mnadani) Salehe Omary Msuka alisema moto huo umewaathiri na wamepata hasara kubwa kutokana na uwepo wa vibanda 550 vilivyoteketea kwa moto ndani ya eneo hilo.

Msuka alisema asilimia kubwa ya biashara inayofanyika Mnadani hapo ni uuzaji wa vitu vilivyotumika huku wachache wakiweka vitu vipya.

“Taarifa za moto nilizipata saa 12 asubuhi na nilipofika eneo hili nilikuta baadhi ya vifaa vimeungua na vingine vikiwa vimetolewa nje kabla ya moto kusambaa kote,” alisema Msuka.

Alisema moto huo pia umeleta hasara kwa wafanyabiashara wanaozunguka eneo hilo kwa kuunguza maduka zaidi ya 10 na majengo ya jirani.

“Niwape pole wafanyabiashara wote akiwemo Big Bon na (Ahmed) ambao magorofa yao yamepata misukosuko ya moto na mengine kuteketea,” alisema.

Hata hivyo, Msuka aliwaomba wafanyabiashara kuwa watulivu wakati wakisubiri kauli ya Serikali kuhusu moto huo ambao chanzo chake hakuijafahamika.

Msuka alisema sehemu kubwa ya wafanyabiashara wa eneo hilo ni wa vipato vidogo na moto huo umewaaongezea machungu zaidi.

Mmoja wa wamiliki wa majengo jirani na eneo la tukio, Ally Rubea alisema wapangaji wake wanne wameathirika na moto huo na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) na Mnazi mmoja kwa ajili ya matibabu.

“Wapangaji wangu wanaoishi ghorofa ya pili walikuwa jirani na sehemu ulipoanzia moto na waliathirika kutokana moshi uliosababisha giza, hivyo wamepata madhara ya moshi na mvuke,” alisema Rubea.

Alisema licha ya kuwepo wapangaji hao pia katika jengo lake kuna Benki ya Baroda ambayo imepata hitilafu kwenye jenereta lililopo nyuma ya jengo hilo.

Mlinzi wa zamu wa Benki ya Baroda aliyejitambulisha kwa jina moja la Kimaro alisema aliona moshi ukiwa unatokea nyuma ya jengo analolinda saa 12 asubuhi na kuamua kupiga simu Zimamoto.

“Nilipiga simu Zimamoto, kisha nikawataarifu viongozi wangu na wahusika wa majengo ili waweze kuona namna wanavyoweza kutoa msaada kuuzima moto na kuondoa familia zao,” alisema Kimaro.

Mkazi mmoja wa kati ya mtaa wa Mafia na Msimbazi, aliyejitambulisha kwa jina la Sultan alisema watoto wake walijeruhiwa katika harakati za kuwaokoa, pale alipo warusha kutoka upande mmoja wa ghorofa kwenda upande mwingine.

“Kutokana na taharuki sikuona sababu ya kubaki kwenye jengo, niliamua kuwaokoa watoto, nikaamua kuwarusha upande wa pili. Mmoja ameumia usoni na yupo Muhimbili," alisimulia Sultan ambaye alirejea kwenye tukio kuhakikisha usalama wa mali zake.


Hakuna aliyepoteza maisha

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema katika tukio hilo, hawajapokea taarifa za mtu yeyote kupoteza maisha au kujeruhiwa, isipokuwa mishtuko ya kawaida.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wamiliki walisaidiana kuokoa baadhi ya mali na kuudhibiti moto huo.

“Hasara itakuwepo kwa wenye mali kwanza ni kwa majengo yenyewe lakini pia mali, lakini taarifa zaidi tutaendelea kufahamishwa kadri jitihada za kuzima moto zinavyoendelea,” alisema.

Chalamila alisema alichokibaini katika tukio hilo ni njia kati ya jengo na jengo kuzibwa, hivyo ni wakati mwafaka wa kuzifungua ili kunapotokea majanga ya moto watu waweze kupita na kufanya uokoaji.

“Baadhi ya vichochoro tumebaini vimetengenezwa kwa mbao ambavyo vimekuwa kichocheo cha moto, nilipongeze Jeshi la Zimamoto kwa umahiri wao lakini pia kwa vyombo vingine vya ulinzi na usalama,” alisema.

Kuhusu madai ya wananchi kuwa Zimamoto wamechelewa, Chalamila alisema ajali inapotokea siku zote haina taarifa.

“Ni kitu kisichowezekana ajali itokee halafu hapohapo ikajiwasha yenyewe kama jenereta, kilichofanyika kuudhibiti moto usienee kwenye majengo mengine na kuendelea kuuzima ni jambo kubwa.

“Niwashukuru Watanzania wa Kariakoo wameonyesha ushirikiano mkubwa kwa kusaidia kuhamisha vitu vyao, hatujapokea taarifa ya wizi wa mali kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo,” alisema.

Hata hivyo, Chalamila alitoa rai kwa wamiliki wa majengo, kujikinga na majanga ya moto kama maelekezo yanavyotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuwa upo utaalamu unaoelekeza vitu vinavyopaswa kuwepo.

“Tuhakikishe hivyo vitu vinakuwepo, jambo lingine tuchukue tahadhari ya moto unaoweza kuwa hatarishi.Wale wote walioziba vipenyo kwa mujibu wa ramani wachukue hatua kuvifungua wenyewe ili kujidhatiti na majanga kama haya.

“Mtakumbuka hili ni tukio la pili kutokea, tukio la kwanza lilikuwa Soko la Kariakoo na leo hapa barabarani, ukiangalia hakuna hata vichochoro vya kuingia huko, sasa waanze kubomoa wao wenyewe kwa mujibu wa michoro ya mipango miji,” alisema.