Majaliwa: Watanzania fanyeni mazoezi kuepuka magonjwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa Maendeleo Bank Marathon 2023 jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote nchini kujenga na kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoefu ya kuimarisha viungo vya mwili kwa lengo la kupunguza ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa nchini.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote nchini kujenga na kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoefu ya kuimarisha viungo vya mwili kwa lengo la kupunguza ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa nchini.
Majaliwa ameshauri kila familia kuweka utaratibu wa mazoezi hayo kwa kukimbia au kutembea angalau kuhakikisha mkimbiaji anatoka jasho.
“Mazoezi ni afya, faraja, kujenga urafiki na furaha ya pamoja, familia zifanye mazoezi ya kukimbia, kutembea angalau utoke jasho,”amesema Majaliwa leo Septemba 2, 2023 wakati wa Maendeleo Bank Marathon 2023, iliyohusisha mbio za kilometa 21, 10, 5 na kilometa mbili na nusu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa benki hiyo, mbio hizo zimekusanya zaidi ya Sh120 milioni kati ya Sh200 milioni zitakazohangia huduma kwa watoto wenye changamoto za mtindio wa ubongo Kituo cha Diakonia cha Kilutheri cha Mtoni jijini Dar es Salaam na Njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC).
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, kila watoto 11 kati ya 100 vizazi hai huzaliwa kabla ya muda (njiti), sawa na watoto 230,000 kati ya milioni 2.4 wanaozaliwa kila mwaka huku watoto wenye utindio wa ubongo (usonji) takribani 50,000 wakizaliwa na changamoto hiyo kila mwaka.
Majaliwa amesema hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kuimarisha usalama wa watoto hao ni pamoja na kujenga wodi maalumu, huduma za vifaa tiba ngazi zote, hospitali zote za wilaya kutoa huduma za watoto hao, mafunzo ya muda mfupi ya kuimarisha huduma hiyo.
“Lakini pia tunaendelea na mafunzo ya muda mfupi, kusaidia watoto wenye usonji ili waweze kuongea, kusaidia mtoto afanye matendo mablimbali, kuimarisha mifumo ya elimu, vifaa vya kidigitali kwenye shule, vifaa visaidizi na viti mwendo, tumeagiza kila halmashauri kutenga bajeti,” amesema Majaliwa.
Tukio hilo limehudhuriwa na zaidi ya washiriki 4,000 wakiwamo Mkuu wa Kanisa mteule wa KKKT, Dk Alex Malasusa, Mkuu wa Kanisa anayemaliza muda wake, Dk Fredrick Shoo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank, Ibrahim Mwangalaba amesema benki hiyo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) inaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013 ikiongeza mtaji kutoka Sh7 bilioni mwaka 2013 hadi Sh114 bilioni mwaka huu.