Majaliwa: Wafanyakazi hawana deni na Rais

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiwa na Makamu wa Rais Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, Spika wa Bunge, DkTulia Ackson pamoja na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Tumaini Nyamhokya wakiimba wimbo wa mshikamano (Solidarity Forever) kwenye Maadhimisho ya Siku wa Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Bombadia mkoani Singida.
Muktasari:
- Leo Alhamisi ni Siku ya Mei Mosi. Sherehe hizo kitaifa zimefanyikia Mkoa wa Sindida ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wametoa ujumbe wao mbele ya wafanyakazi.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema wafanyakazi wanafurahishwa na maboresho wanayofanyiwa na Serikali ya awamu ya sita.
Ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 1, 2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ yanayofanyikia kitaifa mkoani Singida ambapo mgeni rasmi ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Sherehe hiyo ina kaulimbiu isemayo “Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na masilahi ya wafanyakazi sote tushiriki,” ikiwa ni ujumbe unaosisitiza kushiriki uchaguzi mkuu huo.
“Jana wakati nakagua maandalizi ya Mei Mosi nilitembelea ofisi za Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ofisi ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Mkoa wa Singida.
“Nikapata nafasi ya kuzungumza na viongozi na baadhi ya wafanyakazi kwa pamoja wakanipa salamu zako wakasema wanafarijika na maboresho unayowafanyia wafanyakazi hapa nchini, na hawana deni wanalokudai ila wewe unawadai muda ukifika watakulipa,” amesema.
Amesema juhudi za Rais Samia kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza fursa za ajira na mazungumzo kati ya Serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi zinanufaisha wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema hatarajii kuona wafanyakazi wanabaki nyumbani siku itakapowadia.
Amesema wafanyakazi wana nguvu ya kuiweka Serikali madarakani hivyo wanapaswa kujiandikisha kisha kupiga kura ifikapo Oktoba.
“Niwasihi sana wafanyakazi asibakie hata mmoja wa sekta ya umma au binafsi ambaye hatajiandikisha kwenye daftari la kudumu na siku ya uchaguzi asibakie hata mmoja nyumbani twende wote tukapige kura,” amesema.
Aidha mbali na nguvu ya kisiasa ameelezea nguvu ya wafanyakazi kiuchumi akisema utendaji wao unakuza uchumi nchini.
“Uchumi wa Tanzania umeimarika sana katika kipindi hiki ukilinganisha na nchi nyingine zinazolingana na sisi, hivyo pongezi za dhati kwa wafanyakazi wa Tanzania” amesema Dk Mpango.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri nchini (ATE), Oscar Mgaya amehimiza uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025 kuleta viongozi wanaojali haki na masilahi ya wafanyakazi, akihimiza ushiriki wa kila mmoja.
“ATE inaunga mkono kaulimbiu ya mwaka huu, ya ‘Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki, masilahi ya wafanyakazi, wote tushiriki’ kwa imani kuwa viongozi wanaojali haki za watu wote watadumisha amani ya nchi yetu, wataweka mazingira bora ya biashara yatakayochochea tija na kuimarisha sekta ya kazi na ajira nchini kwa masilahi ya watu wengi,” amesema Mgaya.