Majaliwa aunda kamati kuwachunguza Polisi mauaji Mtwara

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Muktasari:
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameunda kamati maalumu ya watu tisa ya kuchunguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi, Tanga.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameunda kamati maalumu ya watu tisa ya kuchunguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi, Tanga.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Ijumaa Februari 4, 2022 na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema kuwa timu hiyo itaanza kazi kesho Jumamosi.
Waziri Mkuu ameunda kamati hiyo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassana ambaye leo wakati akiwa Magu njiani kwenda mkoani Mara kuhudhuria kilele za maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) la kumtaka Majaliwa kuunda kamati itakayochunguza tuhuma za mauaji mkoani Mtwara yanayodaiwa kufanywa na askari polisi.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Rais kwa umma imesema kuwa "Kamati hiyo inapaswa kuanza kazi yake kesho na inatakiwa iwe imekamilisha ripoti yake ndani ya siku 14,"
“Mheshimiwa Rais amesema anatambua Jeshi la Polisi limeunda kamati ya uchunguzi lakini ameagiza iundwe kamati hiyo hum iii ikafanye uchunguzi wa mauaji ya Mtwara yaliyofanywa na askari polisi. Mauaji ya Mtwara yalitokea Januari 05, 2022 na mauaji ya Kilindi yaliyotokea Januari 30, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kamati hiyo ina maafisa wenye dhamana kutoka mamlaka tofauti za Serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, Takukuru, Ofisi ya Mwanansheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro awasimamishe kazi maafisa wa Polisi wa Mtwara na Kilindi iii kupisha uchunguzi wakati timu aliyoiunda ikifanya kazi yake.
"Viongozi hawa wanapaswa wakae pembeni, watahojiwa na hii timu wakiwa nje ya ofisi," amesema Waziri Mkuu na kuwataja maafisa hao kuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara (RPC), Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mtwara (RCO) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara cha eneo alilofia mfanyabiashara Mussa Hamisi Hamisi na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Greyson Mahenge anayedaiwa kujinyonga.
“Waziri Mkuu ameagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kilindi na Ofisa Upelelezi wa Wilaya nao pia wakae pembeni kupisha uchunguzi” imesema taarifa hiyo