Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa ateta na Waziri Mkuu wa Ivory Coast

Muktasari:

  • Tanzania na Ivory Coast wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya kilimo cha kakao, korosho na michikichi kwa kuazisha jukwaa la pamoja la wafanyabiashara.

Dar es Salaam. Waziri MKuu Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Ivory Coast, Robert Beugre Mambe na kujadiliana naye masuala ya kidiplomasia, kiuchumi, teknolojia, kilimo na michezo kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwa mwenyeji wake, Boulevard Angoulvant Plateau, jijini Abidjan.

Akitoa ufafanuzi baada ya kikao hicho jana jioni Jumanne, Mei 13, 2025, Waziri Mkuu Majaliwa amesema lengo la kikao chao ilikuwa kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia lakini pia kuhimiza haja ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ikiwemo utafiti na teknolojia za kisasa kwenye kilimo.

“Ivory Coast ina wakazi zaidi ya milioni 31 na inaongoza kwa kilimo cha kakao, korosho na michikichi. Hawa wanalima korosho zaidi kuliko Tanzania, na sisi tunalima korosho kwenye mikoa ya Pwani na kakao kule Mbeya na maeneo mengine. Tunaweza kujifunza kwao na sisi tunaiona hii ni fursa kwetu ya kuongeza uzalishaji kwenye mazao haya,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alikuwa Abidjan kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika jukwaa la siku mbili la Maofisa Watendaji Wakuu barani Afrika lililomalizika jana.

“Kakao ni zao kuu la biashara na linawaingiza fedha nyingi za kigeni. Tumekubaliana kuwa mawaziri wetu wa Kilimo wakutane na waangalie ni maeneo gani ya kuweka mikataba ikiwemo utafutaji wa masoko na masuala ya utafiti,” amesema.

Amesema mazungumzo yao yamefungua milango ya kuimarisha biashara na wamekubaliana na mwenyeji wake kwamba mawaziri wa nchi hizo wa viwanda na biashara pamoja na wa mambo ya nje wakutane na kuweka ajenda ya kwanza ya kufanyika kwa Jukwaa la Kibiashara baina ya Tanzania na Ivory Coast.

“Tumekubaliana kuwa jukwaa hilo lifanyike mapema ili wafanyabiashara wetu wakutane na kubadilishana mbinu na hapa tunataka sekta binafsi ilisimamie eneo hilo. “Kupitia TPSF (Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania), taasisi zikae pamoja na kuainisha ni maeneo yapi ya kujengeana uwezo, iwe ni teknolojia mpya au ubadilishanaji wa wawekezaji katika mazao ya kokoa na korosho,” amesema.

“Tumewahakikishia kuwa tumepunguza muda wa kupata leseni nchini, tumeongeza maeneo ya uwekezaji (EPZA) na hivi karibuni tunatarajia kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kuja Ivory Coast na Nigeria. Tunatarajia hatua hiyo itaongeza masoko lakini pia itakuza utalii,” amesema.

Mapema, Waziri Mkuu wa Ivory Coast, Robert Mambe ambaye pia ni Waziri wa Michezo na Ustawi wa Jamii, amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kushiriki mkutano huo kwa niaba ya Rais Samia ambapo amesema anatambua kwamba ana majukumu mengine ya kitaifa.

Amesema anampongeza Rais wa Tanzania kwa hatua kubwa aliyofikia katika kuiongoza nchi, huku akiipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano mkubwa wa nishati Afrika uliofanyika Januari 27 -28, mwaka huu.

Amesema anakubaliana na mambo waliyojadiliana leo kwenye masuala ya kilimo cha kakao, korosho na michikichi na kwamba wako tayari kushirikiana na Tanzania kwenye shughuli mbalimbali kadri zitakavyopangwa.

“Tunatarajia kushirikiana nanyi kwenye masuala ya zana za kisasa za kilimo. Teknolojia ya kilimo, huku kwetu iko juu sana na tunasubiri kuanza kwa jukwaa la wafanyabiashara ili watu wetu waweze kubadilishana uzoefu,” amesema.