Maisha ya Feri ni zaidi ya biashara ya samaki

Muktasari:
Mojawapo ya maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu katika jiji la Dar es Salaam ni soko la kimataifa la feri (Magogoni).
Dar es Salaam. Mojawapo ya maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu katika jiji la Dar es Salaam ni soko la kimataifa la feri (Magogoni).
Soko hilo ambalo ni maarufu kwa biashara ya samaki nchini, huwakutanisha pamoja wavuvi na wafanyabiashara wa samaki wa jumla na rejareja ambao, wanakwenda kununua bidhaa hiyo kwa ajili ya biashara au chakula.
Hata hivyo, sio biashara ya samaki pekee inayofanyika sokoni hapo, zipo biashara nyingine nyingi ambazo zimebuniwa na watu kulingana na mahitaji katika eneo hilo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu sasa.
Biashara ya pilipili
Bishara ya pilipili ni miongoni mwa biashara zinazofanyika, wanawake wengi wanajishughulisha na biashara hiyo kwa kuandaa pilipili na ndimu ambayo inatumika kwa chakula maarufu cha chachandu.
Hawa Amri ni mjasiriamali anayetengeneza pilipili na ndimu katika soko hilo na kuwauzia wafanyabiashara wanaokaanga samaki na kuuza mitaani. Yeye hujaza pilipili katika makopo au chupa na kuiuza kwa bei tofauti kulingana na ujazo wake.
Mwanamke huyo anasema alianza kufanya biashara hiyo mwaka 1999, wakati huo alikuwa soko la Kariakoo, lakini miaka saba iliyopita alihamia feri ambako anasema biashara ni nzuri tofauti na alikokuwa awali.
“Hapa kuna mzunguko mzuri wa biashara na wateja wangu wakubwa ni wauza samaki, wakitoka kununua samaki wanapitia kwangu kuchukua pilipili,” anasema mwanamke huyo ambaye kazi hiyo inamwezesha kumudu maisha yake.
Hawa anasema biashara yake inategemea kwa kiasi kikubwa biashara ya samaki, hivyo, kama hakuna samaki katika soko hilo naye hatofanya biashara yake, kama samaki wapo wengi naye anauza zaidi pilipili yake anayoitengeneza kwa njia za kienyeji.
Katika biashara hiyo, alisema anaumia malighafi za kawaida ambazo ni mbilimbi, pilipili na vitunguu. Anasema anavichanganya kwa pamoja kisha anachemsha kupata mchanganyiko wake, baada ya hapo anajaza kwenye chupa na kuuza kuanzia Sh400 hadi Sh1,500.
Biashara ya vifungashio
Katika soko hilo wapo pia wafanyabiashara wanaouza vifungashio mbadala kwa wauza samaki na wauza vyakula.
Gaspar Samike ni muuzaji wa mifuko mbadala ambayo imetengenezwa kwa kutumia magazeti, kalenda na karatasi mbalimbali ambazo zimetumika.
Anatumia karatasi hizo kuzalisha mifuko aina ya bahasha kwa ajili ya kufungua bidhaa ndogo ndogo.
“Hii mifuko sitengenezi mimi, ninainunua kwa watu wengine, nakuja kuiuza hapa. Nauza kuanzia Sh200, Sh500 mpaka Sh1,000 kulingana na ukubwa wa mfuko wenyewe,” anaeleza.
Wauza utumbo wa samaki
Mbali na biashara hizo, kuna biashara ya utumbo wa samaki pia inafanyika katika soko hilo tena imeshika kasi kwelikweli.
Utumbo wa samaki ambao zamani ulikuwa unatupwa kama uchafu na kuliwa na kunguru, sasa ni biashara muhimu kwa baadhi ya watu.
Salum Ulende ambaye anajihusisha na biashara hiyo, anasema wao wanafanya kazi ya ukataji wa samaki na kuwasafisha kabla mteja hajaondoka sokoni hapo.
Baada ya kuwasafishia wateja wao, wanakusanya utumbo na kwa ajili ya kuuza kwa wafugaji.
Anasema ndoo moja ndogo ya utumbo wa samaki inauzwa kati ya Sh200 na 300 na wateja wao wakubwa ni wafugaji ambao, wanatumia bidhaa hiyo kwa ajili ya kutengeneza chakula cha kuku, bata au nguruwe.
“Huu utumbo tunawauzia wafugaji wa kuku, wanachukua na kwenda kuuanika, kisha wanasaga na kuwa chakula cha kuku. Wengine wanakwenda kuuchemsha na kuwa chakula cha nguruwe,” anasema Ulende.
Biashara ya barafu
Biashara ya mabarafu nayo imekuwa muhimu katika soko hilo kutokana na umuhimu wake katika kuhifadhi samaki ili wasiharibike.
Vijana wengi katika soko hilo wanafanya biashara ya mabarafu na kuyauza kwa wafanyabiashara wa samaki katika soko hilo.
Abdallah Shaweji amefanya biashara hiyo katika soko la feri kwa zaidi ya miaka 10 na biashara hiyo imemfanya amudu kuendesha maisha yake sambamba na kusomesha watoto wake na kutunza familia.
Anasema wananunua mabarafu hayo kutoka viwandani huko Keko au Kigamboni yakiwa ni mabonge makubwa, kisha wanakuja kuyauza rejareja kwa wauza samaki wa feri ambao wanayatumia kwa ajili ya kuhifadhia samaki wasiharibike.
“Biashara hii inakwenda vizuri kama kuna samaki wengi, tunauza mpaka Sh200,000 kwa siku. Kwa sasa hapa hakuna samaki kwa sababu ya hali ya hewa, kwa hiyo na biashara yetu pia inakuwa sio nzuri,” anasema mfanyabiashara huyo.