Mahakama yatengua uamuzi Baraza Kuu Chadema kesi kina Mdee

Muktasari:
- Yasema ni kinyume cha haki asili wajumbe wa Kamati Kuu kushiriki uamuzi wa Halmashauri Kuu
Dar es Salaam. Mahakama Kuu imetengua uamuzi wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lililoidhinisha uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwavua uanachama Halima Mdee na wenzake 18.
Akitoa uamuzi leo Desemba 14,2023, Jaji Cyprian Mkeha, amesema kitendo cha wajumbe wa Kamati Kuu kuwa pia wajumbe wa Baraza Kuu na kutoa uamuzi wa rufaa ni kinyume cha kanuni za haki asili.
Mahakama pia imeamuru Chadema kuzingatia haki za asili wakati ikishughulikia rufaa za kina Mdee.
Kwa uamuzi huo, Chadema kinapaswa kusikiliza upya rufaa za kina Mdee kwa kuzingatia kanuni za haki za asili.
Mdee na wenzake 18 walikwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11,2022 wa kutupilia mbali rufaa walizokata wakipinga Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua uanachama, Novemba 27,2020.
Walivuliwa uanachama wakidaiwa walienda kuapishwa kuwa wabunge wa Viti Maalumu bila kupendekezwa wala ridhaa ya Chadema.