Kesi ya akina Mdee yakwama

Muktasari:
- Kesi ya kina mdee kupinga kufukuzwa uwananchama imeshindwa kuendelea baada ya mashahidi wawili wajumbe wa bodi ya wadhamini kushindwa kufika Mahakamani.
Dar es Salaam. Kesi iliyofunguliwa na waliokuwa wanachama wa Chadema, Halima Mdee na wenzake 18 dhidi ya chama hicho, wakipinga kufukuzwa uananchama, imeshindwa kuendelea baada ya wajumbe wawili wa bodi ya wadhamini, waliotakiwa kuhojiwa kushindwa kufika Mahakamani.
Wajumbe hao walitakiwa kuhojiwa leo Jumatano Julai 26, ikiwa ni ombi la waleta maombi baada ya wao kumaliza kuhojiwa.
Mdee ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dar es Salaam, wakipinga kufukuzwa uanachama kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).
Wakili wa wajibu maombi, Hekima Mwasipu, ameieleza kuwa kuwa, mashahidi waliokuwa wanawategemea leo mmoja anaumwa na mwingine yuko njiani kuja Dar es Salaam.
"Shahidi Mary Joachim amepata udhuru, anaumwa lakini shahidi mwingine Ahmed Rashid Hamis yuko njiani akitokea Zanzibar, tumeomba ahirisho hadi kesho," amesema Wakili Mwasipu.
Tayari wajumbe wawili wa bodi ya wadhamini ya Chadema, wameshahojiwa akiwemo Ruth Moleli na Profesa Lwaitama.
Wajumbe wengine ni wanopaswa kuhojiwa ni, Mary Joseph Mushi, na Maulida Anna Komu.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Cyprian Mkeha, imeiahirisha hadi kesho Julai 27, kwaajili ya waleta maombi kuendelea kuhoji maswali ya dodoso.