Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yasema kuondolewa kwa CAG Assad kulikiuka Katiba

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani, Profesa Mussa Assad

Muktasari:

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani, Profesa Mussa Assad aliteuliwa kushika wadhifa huo na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Novemba 5, 2014 na alihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitano hadi Novemba 4, 2019, baada ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kumteua Charles Kichere kushika wadhifa huo.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu imetamka kuwa uamuzi wa kumwondoa katika utumishi wa umma aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ulikiuka Katiba.


Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Desemba 5, 2022 na jopo la majaji watatu, Dk Benhajj Masoud (kiongozi wa jopo), Juliana Masabo na Edwin Kakolaki kufuatia kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

Profesa Assad aliteuliwa kushika wadhifa huo na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Novemba 5, 2014 na alihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitano hadi Novemba 4, 2019 baada ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alipomteua Charles Kichere kushika wadhifa huo.


Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Serikali mwaka 2019 ilieleza kuwa Profesa Assad kipindi chake kilimalizika Novemba 4, 2019.


Zitto aliamua kufungua kesi ya Kikatiba mahakamani hapo akipinga kuondolewa kwa Profesa Assad katika wadhifa huo na uteuzi wa Kichere kuwa CAG mpya, akidai kuwa Profesa Assad alikuwa hajatimiza muda wake wa utumishi kikatiba yaani umri wa kustaafu.

Zitto aliamua kufungua kesi ya Kikatiba mahakamani hapo akipinga kuondolewa kwa Profesa Assad katika wadhifa huo na uteuzi wa Kichere kuwa CAG mpya, akidai kuwa Profesa Assad alikuwa hajatimiza muwa wake wa utumishi kikatiba yaani umri wa kustaafu.

Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 8 ya mwaka 2020, Zitto akiwakilishwa na mawakili Dk Rugemeleza Nshala na Nyaronyo Kichere, alikuwa akipinga kuondolewa kwa Profesa Assad na kuteuliwa kwa Kichere kuwa ni kinyume cha Katiba ya nchi.

Alidai kuwa kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma namba 11 ya mwaka 2008 kinachoweka mihula miwili ya miaka mitano ya utumishi wa CAG, ambacho ndicho kilichotumika kuondolewa kwa Profesa Assad, kinakinzana na masharti ya Katiba.

Zitto alidai kuwa Ibara ya 144(1) ya Katiba ambayo inaeleza kuwa CAG atatumikia wadhifa huo mpaka umri wake wa kustaafu, yaani miaka 60 kikatiba  au miaka 65 kisheria, sawa na kifungu 62(a) cha sheria hiyo kinavyoeleza.

Hivyo, alikuwa akiiomba mahakama hiyo itamke kuwa kifungu hicho cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi, ni batili kwa kuwa kinakinzana na Katiba na kwamba kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kutimiza umri wa kustaafu ni batili na pia uteuzi wa Kichere kuwa CAG mpya ni batili.

Mahakama hiyo katika hukumu yake iliyosomwa jana ilikubaliana na hoja za Zitto kuwa kifungu hicho cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi kuweka mihula ya miaka mitano mitano ya utumishi wa CAG ni batili kwa kuwa kinakinzana na Katiba Ibara hiyo ya 44 ambacho kinaendana na Katiba.

Mahakama hiyo imesema kuwa wakati kifungu hicho kinaweka mihula ya utumishi wa CAG, Katiba inazungumzia umri wa kustaafu na si mihula.

Hivyo, Mahakama imesema kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kulikuwa ni batili.

Hata hivyo, Mahakama hiyo imekataa maombi ya Zitto kutamka kuwa uteuzi wa Kichere ni batili, badala yake imesema kuwa uteuzi wake ni halali kwa kuwa aliteuliwa kwa mujibu wa Katiba.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu hukumu hiyo, Wakili Nshala amesema imeacha utata baada ya kukubali kuwa kuifungu hicho cha sheria kinachoweka mihula badala ya umri ni batili na kwamba Profesa Assad aliondolewa kinyume cha Katiba lakini ikasema kuwa uteuzi wa Kichere ni halali.

Zitto katika taarifa yake kwa umma akizungumzia kipengele hicho amesema kuwa amewaelekeza mawakili wake kukata rufaa Mahakama ya Rufani kwa lengo la kubatilisha uteuzi wa Kichere.

Wakili Nshala alisema kuwa wako tayari kwa maelekezo ya mteja wao, Zitto kukata rufaa Mahakama ya Rufani katika kipengele hicho ili kupata ufafanuzi zaidi.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniface Luhende alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia uamuzi huo, hakuweza kupatikana kwa kuwa simu yake haikuwa hewani.