Mahakama yaridhia Wamarekani kumuasili mtoto mchanga aliyetupwa Geita

Morogoro. Tunamrudishia tabasamu, ndio kauli unayoweza kuelezea uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kuridhia ombi la raia wa Marekani la kumuasili mtoto wa Kitanzania aliyetupwa na mama yake akiwa kichanga.
Raia hao ambao ni mume na mke, waliwasilisha ombi mbele ya Mahakama Kuu kanda ya Morogoro ya kumwasili mtoto huyo wa kike aliyezaliwa huko Geita, Septemba 26, 2023, sasa akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi tisa.
Katika uamuzi huo uliotolewa leo Jumatano, Julai 9, 2025, Jaji Aisha Sinda ametamka, kuanzia sasa raia hao wa Marekani watakuwa wazazi wa kuasili na anatakiwa kukataa jina lake la zamani na ajulikane kwa jina jipya kama waombaji walivyoomba.
Mahakama imetumia herufi za RCV na SMV kuwatambulisha waombaji hao raia wa Marekani na mtoto akipewa ufupisho wa ZS kuficha utambulisho wao, ili kulinda maadili na utambulisho wao kwa mujibu wa sheria.
Katika uamuzi wake huo, Jaji Sinda ameamuru tarehe ya kuzaliwa kwa mtoto huyo iandikwe katika kumbukumbu kuwa ni Septemba 26, 2023 na amri hiyo ya kuasili mtoto huyo ipelekwe kwa Msajili wa Vizazi na Vifo kwa hatua zaidi.
Jaji alisema baada ya kusikiliza ombi la raia hao wa Marekani na kupitia taarifa ya uchunguzi na mawasilisho ya mawakili wa pande zote mbili, ameridhika kuwa masharti yote ya kisheria yanayotakiwa ya kumuasili mtoto huyo yametimizwa.
Mtoto alivyotupwa na kutunzwa
Kulingana na taarifa iliyopo katika ripoti ya uchunguzi ya Ustawi wa Jamii na mlezi aliyekuwa akimlea, inaonyesha mtoto mchanga ambaye ni msingi wa shauri hilo, alizaliwa Septemba 26, 2023 katika Wilaya ya Geita mkoani Geita.
Mtoto huyo alitelekezwa na mama yake baada ya kuzaliwa na baadaye alipelekwa kituo cha kulea watoto cha Neema House Drop In Centre kilichopo Geita, jitihada za Polisi kumpata mama wa kichanga hicho hazikufanikiwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, raia hao walichukua jukumu la kuwa wazazi, walezi kwa mtoto huyo Aprili 2024 kufuatia kupitishwa kwa ombi lao na Kamishna wa Ustawi wa Jamii la kumlea mtoto huyo kwa barua ya tarehe 8 Novemba 2023.
Kuanzia hapo raia hao wa Marekani ndio walikuwa walezi pekee na wanawajibika kwa ustawi wa mtoto huyo mchanga na wameishi nchini kwa zaidi ya miaka mitatu na wana mazingira mazuri nyumbani kwao ya kumlea mtoto huyo.
Mmoja wa Wamarekani hao ameajiriwa katika taasisi ya Pioneer Bible Translators na kipato chake kinatosheleza kwa ajili ya kumlea mtoto huyo na wote wawili, wako tayari kuwajibika kwa matunzo sawa sawa na mtoto wao wa kumzaa.
Wakati maombi hayo yalipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa mbele ya Jaji Sinda Julai 3,2025, waombaji waliwakilishwa na wakili Ignus Punge ambapo Ofisa Ustawi wa Jamii, Janeth Mbelwa na ndiye aliyewasilisha ripoti ya uchunguzi ya mtoto huyo.
Katika hoja zake kuunga mkono ombi hilo, wakili Punge aliomba kwamba kama ombi hilo litakubaliwa , basi jina la mtoto libadilishwe na kuwa lile lililopendekezwa na raia hao wa Marekani, ombi lililoungwa mkono na Mbelwa.