Mahakama yafunga dhamana ya Kombo, aendelea kusota rumande

Muktasari:
- Mahakama ya Wilaya ya Tanga imefunga dhamana ya kada wa Chadema, Kombo Mbwana kwa maombi ya Polisi kutokana na upelelezi unaoendelea. Kesi imeahirishwa hadi Septemba 12, 2024.
Tanga. Baada ya mvutano wa siku kadhaa kuhusu dhamana ya kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, Kombo Mbwana, Mahakama ya Wilaya ya Tanga imeuhitimisha kwa kufunga dhamana yake.
Uamuzi wa kufunga dhamana umetolewa Alhamisi, Septemba 5, 2024 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tanga, Moses Maroa kutokana na maombi ya Jeshi la Polisi.
Kombo ambaye ni Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Wilaya ya Handeni Vijijini, anakabiliwa na kesi ya jinai, akidaiwa kutumia vifaa vya mawasiliano ikiwemo kadi ya simu ya mkononi isiyosajiliwa bila kutoa taarifa.
Licha ya mashtaka yanayomkabili kuwa na dhamana, mahakama leo imeifunga dhamana hiyo baada ya Jeshi la Polisi kupitia kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) wa Tanga kuwasilisha pingamizi la dhamana kwa hoja ambazo mahakama imekubaliana nazo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 19759 ya mwaka 2024, Kombo anadaiwa kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume cha kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.
Anadaiwa Julai 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi wilayani Tanga, alikutwa akimiliki laini ya Tigo iliyosajiliwa kwa jina la Shukru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umiliki wa laini hiyo.
Pia anadaiwa kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine na kushindwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya laini ya simu.
Kabla ya kufunguliwa kesi hiyo, Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kijiji cha Kwamsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga na kupelekwa mahali ambako hata ndugu zake hawakupafahamu.
Julai 14, 2024, siku 29 baadaye ndipo Jeshi la Polisi kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Zakaria Bernard lilipotangaza linamshikilia kwa tuhuma hizo na Julai 16, 2024 akapandishwa kizimbani.
Kuhusu dhamana
Baada ya kusomewa mashtaka ambayo aliyakana, mahakama ilisema dhamana yake ilikuwa wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja, wenye barua ya mtendaji wa mtaa wanakokaa pamoja na vitambulisho vya Taifa (Nida).
Hata hivyo, hakutimiza masharti hayo kwa kukosa wadhamini kwa kuwa alipopandishwa kizimbani ilikuwa jioni na hapakuwa na mtu wa karibu yake aliyejua.
Siku iliyofuata yake familia yake kwa kushirikiana na mawakili wale walifanya mchakato wa dhamana na walipokamilisha mahakama ilitoa amri ya kufikishwa mahakamani kwa ajili ya dhamana yake, mara mbili lakini Jeshi la Polisi halikutekeleza.
Julai 30, 2024, siku ambayo kesi ilitajwa, mawakili na ndugu zake walifika mahakamani wakiwa wamejiandaa kukamilisha masharti hayo ya dhamana lakini, RCO aliwasilisha mahakamani kiapo kuzuia dhamana hiyo.
RCO alieleza katika kiapo kuwa wanaendelea na upelelezi na wanatarajia kuwaongeza washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao wako katika maneo mbalimbali nchini.
Mawakili wa mshtakiwa, Michael Rugina (aliyekuwa kiongozi wa jopo), Deogratias Mahinyila na Rachael Sadick walipinga kiapo hicho wakidai kiliwasilishwa kinyume cha utaratibu wa kisheria.
Walidai RCO hana mamlaka ya kuzuia dhamana, tena mahakama ikiwa imeshatoa uamuzi wa masharti ya dhamana.
Hakimu Maroa alitengua amri ya masharti ya dhamana akapanga kusikiliza maombi ya polisi ya zuio la dhamana Agosti 12, 2024, akiutaka upande wa utetezi kuwasilisha kiapo kinzani kujibu cha RCO, kabla ya tarehe hiyo.
Siku hiyo maombi hayo yaliposikilizwa upande wa mashtaka ulidai RCO anataka mshtakiwa asipewe dhamana kwa kuwa anaweza kuingilia upelelezi ambao bado unaendelea.
Pia ulidai anakabiliwa na kesi nyingine zilizofunguliwa Dodoma na Morogoro yeye na wenzake wengine, hivyo akipewa dhamana anaweza kuwasiliana nao na kuvuruga upelelezi.
Mawakili wa Kombo walipinga hoja hizo wakidai dhamana ni haki ya mshtakiwa na mashtaka yanayomkabili yanadhaminika.
Katika uamuzi, hakimu Maroa amekubaliana na hoja za upande wa mashtaka kutaka Kombo asipewe dhamana kwa sababu ataingilia upelelezi.
Ameamuru Kombo arejeshwe mahabusu na kusalia huko mpaka pale Jamhuri itakapokamilisha upelelezi ndipo anaweza kupewa dhamana ikiwa ataomba.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 12, 2024 kwa ajili ya kutajwa.