Mahakama ya EACJ: Tanzania imetekeleza maamuzi yetu magumu

Muktasari:
- Baadhi ya majaji na maofisa wa Mahakama ya Tanzania wamepatiwa mafunzo kuhusiana na utawala bora na utawala wa sheria, kutoka Mahakama ya Afrika Mashariki, ambayo imeeleza kuridhishwa na uhusiano wake na Tanzania na jinsi inavyotekeleza hukumu zake.
Dar es Salaam. Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) imeelezea kuridhishwa na uhusiano na ushirikiano inaoupata kwa Tanzania, kuwa ni mzuri ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa hukumu zake zikiwemo zenye maamuzi mazito ilizokwisha kuzitoa katika kesi zilizoihusisha Tanzania.
Hayo yamebainishwa na Jaji Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Nestor Kayobera, kutokana nchini Burundi, alipoulizwa na gazeti hilo baada ya kufungua mafunzo ya siku moja kwa baadhi ya majaji na maofisa wa Mahakama ya Tanzania jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, Oktba 20, 2023 kuhusiana na utawala bora na utawala wa sheria.
“Kwanza kabisa tunaishukru Serikali ya Tanzania na Mahakama ya Tanzania na hasa Mahakama ya Tanzania, kwa sababu mahusiano kati ya Mahakama ya Afrika Mashariki na mahakama zingine za nchi wanachama ni mazuri lakini kwa Tanzania ni mazuri zaidi,” amesema na kufafanua:
“Kwa sababu kama mnavyojua tumepewa sehemu ya usajili katika Mahakama Kuu ya Tanzani, lakini sasa hivi tumepewa ofisi nzuri kule Dodoma ambayo nafikiri ni ofisi nzuri kuliko ofisi zote tulizo nazo katika nchi wanachama.
Kuhusu utekelezaji wa hukumu za mahakama hiyo Jaji Kayobera ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Burundi amesema kuwa nchi zote zinatekeleza ikiwemo Tanzania.
“Tumeshachuka maamuzi mazito lakini mazuri ambayo pia yalihusisha Serikali ya Tanzania na maamuzi yetu hayo Serikali ya Tanzania imetekeleza. Itakuwa ni aibu kwa mfano nchi isitekeleze wakati ni maraisi wenyewe ndiyo wanaoteua (majaji wa mahakama hiyo),” amesema na kusisitiza:
“Burundi yenyewe katika kesi ilizozhusishwa imetekeleza na mimi nilikuwa mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Burundi ambaye nilikuwa nawakilisha Serikali ya Burundi kwenye mahakama ya Afrika Mashariki kabla ya kuteuliwa. Kwa hiyo ni kwamba sisi mahusiano ni mazuri, Tanzania ni mazuri zaidi.”
Hata hivyo, naibu msajili wa mahakama ya EACJ, Christine Wekesa amesema kuwa zaidi ya asilimia 75 ya hukumu za mahakama hiyo zimeshatekelezwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akifafanua zaidi, Jaji Kayobera amesema kuwa tangu mahakama hiyo ianzishwe mwaka 2001 mpaka sasa wameshapokea zaidi ya kesi 700 kutoka nchi zote wanachama, amesema kuwa ni nyingi zaidi zinazoifanya kuwa mahakama ya kwanza ya kikanda kupokea kesi nyingi kuliko mahakama yoyote ya kikanda duniani.
Hata hivyo hakubainisha kama kuna utafiti uliowahi kufanyaika katika mahakama zote za kikanda katika kipengele hicho cha upokeaji wa mashauri mengi.
“Kwa hiyo kwa sasa hivi tumeshapokea kesi hizo na tuna kesi zaidi ya 270 katika Mahakama ya Awali (ya mahakama hiyo) ambazo ni kesi nyingi,” amesema Kayobera na kufafanua:
“Ni kesi nyingi kwa sababu wananchi wa Afrika Mashariki wameshaelewa kwamba haki yao wasipoipata katika nchi yao watakenda kuipata katika Mahakama ya Afrika Mashariki.
Amesema kuwa uzuri zaidi ni kwamba Makataba wa Afrika Mashariki umeonesha kwamba si lazima mwananchi aende katika mahakama ya nchi yake.
Hivyo, amesema kuwa mwananchi anaweza kwenda moja kwa moja katika Mahakama ya Afrika Mashariki bila hata kupitia kwa nchi yake ili mradi tu liwe ni shauri linalolingana na mkataba wa Mahakama ya Afrika Mashariki.
“Pia tunashukru kwamba nchi zote maamuzi ya mahakama yetu kwa kweli hayana matatizo yoyote katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tunashukuru pia kwamba watu wanaokuja Mahkama ya Afrika Mashariki sasa hivi ni watu wenye uelewa.
Kuhusu mafunzo hayo kwa majaji na mahakimu, Jaji Kayobera amesema kuwa ni kwa ajili ya uelewa kuhusiana na utawala bora na utawala wa sheria.
Amesema kuwa masuala ya utawala bora na utawala was sheria ni muhimu katika kutenda haki katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Jaji wa Mahakama Kuu, Isaya Arufani akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kutumia sheria za ndani kwa ajili ya utawala wa sheria.
Jaji Arufani amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia zaidi majaji na mahakimu katika kufanya kazi zao katika kushughulika na mashauri mbalimbali hasa yanayohusiana na utawala bora na utawala wa sheria kwa kuwa huo pia ndio msingi wa Mahakama ya Tanzania.
Amesema kuwa baada ya mafunzo hayo anatumaini kuwa washiriki watakuwa makini sana hasa kuamua mashauri yanayohusiana na utawala wa sheria na utawala bora, kwa sabau yako mashauri mbalimbali ambayo yanafunguliwa mahakamani hapo na wananchi wakilalamiia masuala hayo.
“Kwa hiyo kama yakitokea mafunzo haya tunaamini kuwa yanatupa uelewa mkubwa na wepesi wa kuweza kuyatolewa maamuzi,” amesema Jaji Arufani.
Naya Jaji Isaya Godfrey kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambaye pia ameshiriki mafunzo hayo amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa ya muhimu kwa kuwa kwanza yamewapa uelewa mpaka kuhisiana na Shirikisho la Afrika Mashariki.
“Kwetu sisi tumejifunza pia kuhusu sheria za Afrika Mashariki namna ambavyo tunazitumia katika mahakama zetu,” amesema Jaji Isaya.
Hakimu Mary Karome, amesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa na msaada mkubwa yatawapa uelewa mpana wa sheria katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na namna ya kutoa uamuzi usioathiri umoja huo .
“Kwa hiyo naamini mafunzo haya yataleta tija kwa Mahakama ya Tanzania na mimi kama mtekelezaji nitapata uelewa mpana wa masuala ya utawala bora na utawala wa sheria Afrika Mashariki.