Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mageuzi wanayotamani wananchi kwenye korosho, Makalla awatuliza

Baadhi ya wananchi wa Newala wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla.

Muktasari:

  • Wakulima wa Lindi na Mtwara wanalalamikia ucheleweshaji wa pembejeo, hasa dawa, jambo linaloshusha tija na ubora wa korosho. Wanaamini tatizo linatokana na usimamizi dhaifu wa vyama vya ushirika licha ya juhudi za serikali kuboresha sekta hiyo muhimu ya uchumi.

Mtwara. Licha ya mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya kilimo cha korosho nchini, wakulima wa mikoa ya kusini hasa Lindi na Mtwara bado wanalia na changamoto kadhaa zinazowakwamisha kufikia manufaa ya juu ya ‘dhahabu’ hiyo ya kusini. Zao la korosho limekuwa nguzo muhimu ya uchumi wa wananchi wa maeneo haya, lakini matumaini yao ya kuona mageuzi halisi bado hayajatimia ipasavyo.

Baadhi ya wakulima wameeleza kile walichokiita changamoto kuhusu ucheleweshwaji wa pembejeo, hasa dawa, ambao umekuwa kikwazo kikubwa katika kuongeza tija na ubora wa mazao. Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wananchi hao akiwamo, Asha Salehe Hussei, mkazi wa Nachingwea mkoani Lindi Newala, alisema kucheleweshea pembejeo ni moja ya changamoto kubwa.

“Zao hili linahitaji sumu mapema, kuanzia mwezi wa sita tunapaswa kupulizia dawa. Lakini pembejeo zinakuja mwezi wa tisa au hata wa kumi, wakati korosho zimeshaathirika.”

Kwa mujibu wa Mwajuma Salum Issa wa Legeza, wilayni Newala mkoani Mtwara alisema, kuna hisia kwamba ucheleweshaji huo unatokana na usimamizi hafifu baadhi ya watu waliko katika vyama vya ushirika.

“Inawezekana serikali inaleta pembejeeo mapema, lakini baadhi ya waopewa mamlaka ya kusambaza huko kwenye vyama vya ushirika ndiyo wanatukwamisha. Sisi hatujui kinachoendelea nyuma ya pazia.”

Diwani wa Viti Maalum, Faiza Kahamba, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kutoa wito kwa serikali kuona namna ya kuimarisha mfumo wa usambazaji:

“Wakulima wanahangaika, hali hii inavunja morali. Serikali isimamie vyama na wakala wake wahakikishe pembejeo zinapatikana kwa wakati.”

Mfumo wa mnada: Faida ya wengine, hasara ya mkulima

Kando na kuchelewa kwa pembejeo, wakulima wamelalamikia mfumo wa mnada wa ununuzi wa korosho ambao kwao unaonekana kuwapa faida zaidi wafanyabiashara wa kati kuliko wakulima halisi.

Upande wake, Dotto Ngwada wa Mtama alisema: “Mnada wa kwanza huwa na bei nzuri, ambayo ni zaidi ya Sh4,000 kwa kilo moja ya korosho, lakini sisi hatunufaiki. Korosho nyingi zinazouzwa kwenye mnada huo si za wakulima – ni za kangomba. Sisi tunasubiri hadi mnada wa tatu ambapo bei inakuwa tayari imeshashuka,”.

Kwa wakulima kama, Subira Hamis wa Naipanga, anaamini kuwa suluhisho ni kufanya bei ya juu ya mwanzo iwe ya kudumu msimu mzima.

“Tukiambiwa bei ni Sh4,000 basi ibaki hivyo. Isiwe kwa mnada wa kwanza tu ambao hatunufaiki nao,” alisema Subira.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Said Nyegedi, alisema kuwa serikali imeajiri maafisa wapya 500 waliofunzwa mahususi kusimamia ugawaji wa pembejeo:

“Wale waliokuwa wakifanya kazi hii zamani hawataendelea. Wamekuwepo wanaojiona wakubwa kuliko wakulima, sasa tumewaondoa,” alisema.

Mbunge wa Mtama, Nape Nauye, alisisitiza kuwa changamoto hizo si za Rais Samia bali ni uzembe wa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika.

“Tatizo ni kwetu wenyewe. Huko kwenye ushirika kuna watu wasiojua thamani ya wakulima, hawa ndiyo tunapaswa kushughulika noa,” alisema Nape.

Serikali inalima na wananchi

Hamidu Bobali, kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alieleza kuwa mwelekeo mpya wa serikali chini ya Rais Samia ni wa kuwashirikisha wakulima moja kwa moja katika mnyororo mzima wa thamani wa korosho.

“Sasa hivi, serikali haikusanyi kodi tu, inalima na wakulima. Kwa mfano, wataalamu zaidi ya 450 wameletwa kusaidia mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Tanga – ni mageuzi ya kweli.”

Aliendelea kueleza kuwa mfumo wa sasa unatoa nafasi ya ushuru wa serikali kuendana na bei ya soko, tofauti na zamani ambapo bei ilikuwa ya kudumu hata ikishuka sokoni.

Makalla: Korosho siyo siasa, ni hoja

Katika ziara ya kuhamasisha sera za CCM mkoani Mtwara, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, alitoa msimamo wa chama kuhusu sekta ya korosho huku akiwataka wananchi kuwapuuza wapinzani wanaosema kuwa wakulima wananyonywa.

“Leo hii mnauza korosho kwa Sh4,000 kutoka bei ya zamani ya chini, halafu mtu anakuja kusema mnanyonywa? Mtu huyo hajawahi kulima korosho wala hajui uchungu wake.”

Makalla alisisitiza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani ni kielelezo cha mafanikio ya sera ya CCM inayolenga kuimarisha ushirika na kuongeza kipato cha mkulima.

“Tuna mfumo unaolinda wakulima, unawapa nafasi ya kushindaniwa na wanunuzi sokoni – siyo kuuza kiholela. Mfumo huu umeleta mageuzi halisi,” alisema Makalla.

Aliwataka wakulima kutambua kuwa serikali ya CCM imepeleka pembejeo, ruzuku, wataalamu na kufanikisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata korosho kama hatua ya kuongeza thamani ya zao hilo, huku akiahidi kuwa watu wanaoleta ujanja kwenye  ugawaji wa pembejeo siku zao zinahesabika.

“Hawa watu wanaoleta ujanja ujanja wakati wa ugawaji wa pembejeo kwa wananchi siku zao zinahesabika, kwani tayari serikali imeandaa wataalamu 500 ambao wanagawiwa kila kata kwenye mikoa inayolima korosho kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima wanaondokana na adha ya kucheleweshewa pembejeo hususan dawa,” alisema Makalla.

Aliongeza kuwa, serikali ya Rais Samia na CCM inasimamia dhamira yake ya kuleta mabadiliko yanayoonekana na yanayogusa maisha ya wananchi.

“Hatua zinazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kubadili mfumo wa usambazaji pembejeo, kuongeza ruzuku, na kuimarisha ushirika zinamaana kwamba serikali ya CCM haipo sokoni tu, bali “inalima pamoja na wananchi,” alisema Makalla.

Kwa mujibu wa Bodi ya Korosho, ruzuku ya pembejeo imeongezeka kutoka Sh59.4 bilioni mwaka 2021 hadi Sh281 bilioni kwa mwaka 2024/25 ikiwa ni ongezeko la mara nne.