Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magari aliyobuni Kipanya sasa kuingia sokoni rasmi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Magari hayo ni matokeo ya Kipanya ya kuzindua gari la kwanza la kutumia umeme nchini Aprili 2, 2022 lililotengenezwa na mafundi wa hapa nchini

Dodoma. Takribani magari 20 yanayotumia umeme ya mtangazaji na mchora katuni, Masoud Kipanya yataingia sokoni hivi karibuni.

Magari hayo ni matokeo ya Kipanya ya kuzindua gari la kwanza la kutumia umeme nchini Aprili 2, 2022 lililotengenezwa na mafundi wa hapa nchini.

Kipanya siyo wa kwanza kufanya ubunifu wa kuunda gari, miaka ya nyuma fundi gereji wa Buguruni alitengeneza lililopelekwa kwenye maonyesho na baadaye likawa linatumiwa na mmliki.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kiliwahi kufanya ubinifu wa kuunda gari la kutumia umeme lililoonekana kwenye maonyesho ya biashara nchini na baadaye halijulikani lilipo.

Tofauti na hao, Kipanya baada ya uzinduzi huo aliendelea na mchakato wa kutengeneza magari na mengi na sasa magari 20 yanatarajiwa kuingia sokoni wakati wowote mwaka huu.

Kilichofanywa na Kipanya ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye wakati wa maonyesho ya Wakulima ya Nanenane yaliyofanyika jijini Mbeya mwaka mmoja uliopita alionyesha kushangazwa na ng’ombe bora na walionenepeshwa kuwepo wakati wa maonyesho tu na mtu akihitaji kununua hata 10 hawapatikani.

Majaliwa aliagiza kwamba bidhaa zote bora zinazoletwa kwenye maonyesho ziwe kwa wingi ili mtu akitaka kununua aweze kupata, badala ya kuwa bidhaa za maonyesho pekee.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Juni 25 jijini hapa, Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Kaypee Motors inayotengeneza magari hayo ya Kipanya yanayoitwa Kaypee Motor, Shadrack Kikoti amesema magari 20 yataingia sokoni wakati wowote.

Awali, akizungumza katika kongamano la tatu la Taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT), Kikoti amesema lina  kauli mbiu isemayo: “Uvumbuzi uwe biashara kwa mfumo endelevu wa chakula.”

Kongamano hilo linaloshirikisha watafiti, wavumbuzi na wadau wa kilimo zikiwamo wizara tatu za kilimo, uvuvi na biashara na viwanda, limezinduliwa na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu.

Gari hilo ni wazo la ubunifu lililotolewa na Kipanya  lililomchukua miezi 11 kukamilika na ni rafiki kwa mazingira kwa sababu halitumii nishati ya mafuta linaitwa Kaypee Motor na linachajiwa kwa saa sita kabla ya kutumika.

“Hili ni gari la nguvu sana ambalo ukinunua unapata na chaji yake,” alisema Kipanya wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Hoteli ya Dar es Salaam Serena na kuhudhuriwa na baadhi ya wafanyabiashara nchini.

Kwa mujibu wa Kipanya gari hili linatumia umeme na lina uwezo wa kubeba kilo 500.

Alisema changamoto iliyopo wabunifu wengi wanafanya vema, lakini wanaishia kwenye maonyesho, hawaendi mbele na kumuomba ashirikiane na wafanyabiashara kuingiza sokoni ubinifu huo.

Kipanya alisema kila kitu wametengeneza wenyewe ikiwamo kuchonga mabati na kuyapinda dashibodi na plastiki.

 “Kama ilivyo viwanda vingine vya magari tairi, vioo, betri na mota tumenunua kutoka sehemu nyingine,” alisema.

Alisema wapo kwenye mchakato wa kujisajili Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kama wawekezaji wa ndani huku akieleza tayari wametengeneza gari nyingine mbili za aina tofauti ambazo zitakuwa kubwa kuliko iliyozinduliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ushirika wa wahitimu wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA-SUGECO), Revocatus Kimarro akizungumza kwenye kongamano hilo amesema suala la ubunifu limekuwa na changamoto nyingi.

Amesema kijana anapofanya ubinifu kitu cha kwanza kitaulizwa kiwango chake cha elimu na kama hana shahada au shahada ya uzamivu uvumbuzi wake unawekewa maswali mengi.

Mtendaji Mkuu wa AMDT, Charles Ogutu alimuomba Naibu Spika Zungu kuwa Bunge na Serikali liwaangalie wabunifu  kwa kuwapa ruzuku ili waendeleze ubunifu wao.

Hata hivyo, Zungu amesema  Bunge liko tayari kushirikiana nao ikiwamo kupokea na kuyafanyia kazi mawazo yao.

Pia, amewaomba wananchi kubadili mtindo wa maisha kwa kutumia fedha zao kwenye uwekezaji na kufanya biashara badala ya kufanya matumizi ya anasa.