Mafuta kukaangia zaidi ya mara moja hatari

Muktasari:
Kutumia mafuta ya kukaangia vyakula kama kuku, viazi na samaki, zaidi ya mara moja kunaweza kusababisha ugonjwa wa saratani, wataalamu wameonya.
Dar es Salaam. Kutumia mafuta ya kukaangia vyakula kama kuku, viazi na samaki, zaidi ya mara moja kunaweza kusababisha ugonjwa wa saratani, wataalamu wameonya.
Habari hiyo inaweza kuwa si nzuri kwa wananchi ambao wamezoea kujipatia chakula kwa wafanyabiashara wadogo wa vyakula, hasa chips, kuku na samaki, ambao hutumia mafuta hayo bila ya kubadilisha kupunguza gharama.
Wataalamu wanasema mfuta yaliyotumika yanapohifadhiwa na kuyumika tena, hutengeneza sumu inayozalisha kemikali ambayo hukaa ndani ya utumbo na baadaye hutengeneza uvimbe ambao hugeuka saratani.
Ofisa muuguzi muelimishaji, Elizabeth Likoko alisema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu magonjwa yasiyoambukiza wakati wa mkutano wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) uliofanyika Dar es Salaam jana.
Elizabeth alisema ulaji wa chipsi, samaki, kuku waliokaangwa mitaani si salama kwa kuwa waandaaji wengi wanayatumia zaidi ya mara moja.
“Chipsi za mitaani mafuta yanachemka kuanzia asubuhi hadi jioni; na kinamama tumekuwa wavivu tunaona ni bora kumnunulia mtoto chipsi au kununua samaki ameshakaangwa bila kujua mafuta yaliyotumika.
“Unatarajia inatengeneza nini? Zaidi ni sumu? Na zile kemikali zinaingia kwenye leya ya utumbo kila siku baadaye inajizidisha inatengeneza uvimbe ndiyo saratani tayari umeshaipata kwa hiyo tuache kabisa kununua vyakula vilivyoandaliwa,” alisema Elizabeth.
Pia, alisema mafuta ya wanyama yana athari za moja kwa moja kwa binadamu.
“Mafuta yenye asili ya wanyama hayachanganyiki na damu yanajibandika tu kwenye damu, mwishowe sehemu ya kupitisha damu imebaki ndogo moyo unaanza kufanya kazi kwa bidii, kinachotengenezwa mafuta yamejaa yamesiriba kwa hiyo ndiyo wale ambao wakipigwa X Ray wanaambiwa moyo umetanuka na kwanini, sababu ya moyo ulitumia nguvu kubwa kufanya kazi na misuli inakuwa imetanuka.”
Kauli ya Elizabeth iliungwa mkono na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Tatizo Waane ambaye alisema mafuta yanapotumika zaidi ya mara moja husababisha kuzalishwa kwa kemikali hatari mwilini .
Dk Waane alisema kemikali hizo ni chanzo cha magonjwa mengine yasiyoambukiza ikiwemo saratani ya utumbo mpana.
Hata hivyo Dk Waane ambaye alikuwa Mwenyekiti wa TANCDA awamu ya pili, alisema mafuta ni muhimu mwilini, lakini yanahitajika kwa kiasi kidogo.
Mmoja wa wauza chipsi, Raymond Ndimbo alisema hubadilisha mafuta kila baada ya wiki moja, “usipobadilisha huwa meusi”.