Maduka ya fedha za kigeni Kariakoo yafungwa

Muktasari:
- Jana, Mwananchi ilipita maeneo mbalimbali Kariakoo na kubaini maduka hayo yakiwa hayatoi huduma, hata yaliyokuwa wazi juzi nayo yalisitisha huduma.
Dar es Salaam. Maduka ya kubadilisha fedha katika soko la Kariakoo yamesitisha kutoa huduma hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kubainisha kuwa imeanza utaratibu wa kufuta leseni za maduka hayo ambayo yanaendesha biashara hiyo bila kufuata masharti ya leseni zao.
Jumatano iliyopita, BOT ilifanya ukaguzi wa maduka hayo na kubaini maduka mengi yanaendesha biashara hiyo bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji huduma ya kubadilisha fedha za kigeni.
Jana, Mwananchi ilipita maeneo mbalimbali Kariakoo na kubaini maduka hayo yakiwa hayatoi huduma, hata yaliyokuwa wazi juzi nayo yalisitisha huduma.
Wateja walipokuwa wakifika, walinzi waliwaambia waende benki kupata huduma hiyo.
“Hapa leo (jana) hakuna huduma, nendeni benki, hapo jirani tu,” alisema mlinzi wa duka moja la kubadilishia fedha lililopo Kariakoo na kumweleza kila mteja aliyefika katika duka hilo kubadilisha fedha.
Katika eneo la posta, duka moja la kubadilishia fedha la UAE ndilo lilikuwa likitoa huduma hiyo lakini nalo lilikuwa limejaa watu ambao walifuata huduma hiyo baada ya kuikosa katika maeneo ya jirani.
Mfanyabiashara wa vitenge Kariakoo, Alex Silwamba alisema alitoka Kariakoo kufuata huduma hiyo Posta lakini alishangaa kukuta watu wengi wamejaa kwenye duka hilo wakitaka kubadilisha fedha.
“Hii kitu kaka ni shida, yaani maduka mengi yamefungwa, nimezunguka Kariakoo sijapata, imebidi nikimbie hadi hapa. Nashukuru nimekamilisha lakini kuna usumbufu mkubwa, wangetoa muda wa kutekeleza jambo hili,” alisema Silwamba.
Wakitoa maoni yao juu ya uamuzi uliochukuliwa na BOT, wafanyabiashara na wananchi wamesema maduka ya kubadilishia fedha yanatoa huduma muhimu kwa wananchi, hivyo yawekewe utaratibu mzuri bila kusababisha kero kwa wananchi.
Mfanyabiashara wa simu za mkononi, Juma Awadh alisema uamuzi wa Serikali ni mzuri lakini ilitakiwa kuwapa muda wamiliki wa maduka haya ili wajiandae ama kutafuta biashara nyingine au kufuata masharti.