Mabilioni yatengwa kusambaza maji Same na Mwanga

Muktasari:
Zaidi ya Sh3.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kusambaza maji katika vijiji 12 vya Wilaya ya Mwanga na Same ambavyo havina huduma ya maji safi na salama tangu kuanzishwa kwake.
Moshi. Zaidi ya Sh3.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kusambaza maji katika vijiji 12 vya Wilaya ya Mwanga na Same ambavyo havina huduma ya maji safi na salama tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza leo Jumatatu Machi 8, 2022 meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) mkoani Kilimanjaro, Weransari Munis amesema wameendelea kuweka katika bajeti vijiji ambayo havina huduma ya maji kabisa
Amesema wamejiwekea mikakati ya miaka mitatu kuhakikisha wanaweka maji katika vijiji 32 ambavyo havijawahi kuwa na maji na kwa mwaka 2020/21, vijiji 12 vya wilaya ya Mwanga na Same vitapata maji.
Amebainisha kuwa wilayani Same kuna vijiji 14 ambavyo havina huduma ya maji na 18 kwa Wilaya ya Mwanga, “ yapo maeneo mengine ambayo tayari yalishakuwa na miradi ya maji lakini kunahitaji uboreshaji.”
"Vijiji 12 vilivyo na wakazi 26,232 Wilaya ya Mwanga na Same vimewekewa makadirio ya bajeti ya zaidi ya Sh3.7 bilioni kwa ajili ya kusambaziwa maji katika mwaka wa fedha 2021/22.”
Amebainisha kuwa mwaka wa fedha 2020/21 kupitia Ruwasa mkoa umetengewa Sh6.9 bilioni zitakazotumika katika kukarabati na kupanua miradi ya maji iliyopo.
Mbunge wa Moshi vijijini, Professa Patrick Ndekidemi aliwataka Ruwasa kuhakikisha wanasambaza maji safi katika maeneo ya shule kwa kuwa nyingi hazina maji safi na salama.