Prime
Maaskofu Katoliki: Wanaotaka mabadiliko sheria za uchaguzi wasikilizwe, wasipuuzwe

Muktasari:
- Romanus Mihali amewekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa ujumbe kwa mamlaka kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan amesema ameupokea ujumbe wao na ataufikisha sehemu kunapohitajika.
Iringa/Dar. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limezitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa uchaguzi kusikiliza sauti za wanaotaka mabadiliko ya Katiba na sheria, ili kuruhusu uchaguzi mkuu kufanyika kwa haki na usawa.
Maaskofu hao wamehoji kwa nini kauli za viongozi mbalimbali juu ya hakikisho la kufanyika uchaguzi kuwa huru na haki kutofuatwa wakisema: “Vilio vya watu wanaotaka mabadiliko hayo ya Katiba na sheria visikilizwe na visipuuzwe.”
Wito huo wanautoa kipindi ambacho kumekuwa na sauti za makundi mbalimbali hususan ya kisiasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakitaka kufanyika kwa mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.
Chadema kimekwenda mbele hadi kuanzisha operesheni ya No reforms no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ na chama hicho kimepoteza sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 baada ya kutosaini kanuni za maadili uchaguzi.
Kanuni hizo zilizoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilisainiwa Aprili 12, 2025 na vyama 18 za siasa, Serikali na Tume yenyewe na tayari zimechapishwa kwenye Gazeti la Serikali (GN), Aprili 18, 2025.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima amenukuliwa akisema Chadema kwa kutosaini fomu hizo kimepoteza sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu na chaguzi zingine ndogo kwa kipindi cha miaka mitano.
Wito huo wa TEC wanautoa ikiwa imepita wiki moja tangu Rais wa baraza hilo, Wolfgang Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, kusema ni muhimu Serikali kukaa na wadau wa uchaguzi, kuruhusu mabadiliko ya lazima kabla ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Askofu Pisa alitoa wito huo usiku wa kuamkia Aprili 20, 2025 katika mahubiri ya misa ya mkesha wa Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Andrea Kaggwa, mkoani Lindi.
Moja kati ya mapendekezo yake manne kuelekea uchaguzi, Askofu Pisa alisema wahusika wakae na wadau wote kuruhusu mabadiliko ya lazima kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Alisema sauti na vilio vya wengi vinapaswa kusikika akisisitiza:"Kasoro zilizojitokeza zinapaswa kurekebishwa haraka. Kukiwa na nia ya dhati kutoka kwa wahusika muda unatosha kabisa kufanya hayo marekebisho kabla ya uchaguzi mkuu."
Akizungumzia amani, alihoji nani anayeiharibu kati ya anayetumia nguvu kusisitiza uchaguzi uende anavyotaka na yule anayeshauri kukaa mezani kufanya mabadiliko ya mifumo.
Ujumbe wa Maaskofu
Akitoa salamu za Maaskofu, Makamu wa Rais wa TEC, Eusebius Nzigilwa ameanza kwa kumpongeza na kumkaribisha kwenye uaskofu Romanus Mihali ambaye amesimikwa kuwa Askofu wa Jimbo la Iringa.
Mihali aliteuliwa na Papa Francis Januari 28, 2025, kuchukua nafasi ya Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, baada ya kuridhia ombi lake la kustaafu. Awali Askofu huyo alikuwa Makamu wa Askofu kwa Waklero wa Jimbo la Mafinga.
Maadhimisho ya misa hiyo yamefanyika viwanja vilivyopo pembeni ya Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu Jimbo Kuu Katoliki la Iringa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali akiwamo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Misa hiyo ya kuwekwa wakfu imeongozwa na Askofu Mkuu mstaafu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo.
Katika salamu hizo za TEC, Askofu Nzigilwa amesema mwaka huu ni wa uchaguzi ambapo viongozi wa Serikali katika nyakati tofautitofauti wamesikika wakiwahakikishia wananchi uchaguzi utafanyika kwa misingi ya haki, usawa na uhuru.
“Tunaomba kauli hizi nzuri za kututia moyo za viongozi wetu zionekane kwa vitendo katika hatua zote za uchaguzi, kwani baadhi ya matukio tuliyoyashuhudia kwenye jamii yetu hayaoneshi watendaji au wasimamizi wa sheria wanatekeleza kile kinachoahidiwa na viongozi wetu,” amesema.
Huku waamini wakimsikiliza kwa utulivu, Askofu Nzigilwa amesema: “Kinachoahidiwa hakiendani na kile kinachotendeka. Ndugu mgeni rasmi (Dk Biteko) kwa muda mrefu kumekuwa na sauti zinazotaka Katiba na sheria zinazosimamia uchaguzi wetu zifanyiwe marekebisho ama maboresho ili ziendane na hali ya demokrasia ya vyama vingi.”
“Inavyoonekana ni kuwa wanaonufaika na upungufu wa sheria za sasa hawana haraka ya kufanya maboresho hayo, na wale wanaojiona wanaathirika na upungufu huo ndio wanapaza sauti kutaka mabadiliko ya Katiba na sheria.”
“Wito wetu sisi maaskofu kwa mamlaka zinazohusika ni kuwa sauti na vilio vya watu wanaotaka mabadiliko hayo zisikilizwe na zisipuuzwe,” amesema Nzingilwa ambaye ni Askofu wa Jimbo la Mpanda.
Akihitimisha salamu za Maaskofu amesema:“Tunaomba maboresho stahiki kwenye mifumo ya uchaguzi yafanyike ili kuruhusu ufanyike kwa uhuru na wa haki katika nchi yetu, vinginevyo chaguzi zetu zitaendelea kugubikwa na dosari nyingi kama zilivyoshuhudia kwenye chaguzi za hivi karibuni.”
Alichokisema Dk Biteko
Dk Biteko akizungumza kwenye sherehe hizo amempongeza Askofu Mihali na Askofu Ngalalekumtwa kwa kazi kubwa ya kitume aliyoifanya kwa miaka zaidi ya 30.
Akigusia suala la uchaguzi kama lilivyozungumzwa na maaskofu, Dk Biteko amesema: “Kama mlivyoahidi na mimi nitakwenda kumwambia Rais ahadi ya kanisa kuendelea kuliombea Taifa ili uchaguzi umalizike kwa amani.”
“Taifa letu linaweza kutofautiana mitazamo, namna ya kuangalia mambo lakini tusitofautiane na kuligawanya Taifa letu. Tubaki kuwa wamoja na imani yangu kila mmoja atatimiza wajibu wake,” amesema.
Dk Biteko amesema: “Ujumbe alioutoa Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu, jamani Askofu akisema jambo hajibiwi.” Kauli hiyo iliibua shangwe kisha Dk Biteko akasema: “Hapana ni amina, baba nimepokea. Lakini jambo moja ambalo nina amini ni Rais wetu anatamani Watanzania tuwe kitu kimoja.”
Amesema hata katika hotuba ya miaka 61 ya Muungano aliyoitoa Rais Samia aligusia suala hilo la uchaguzi akisisitiza Serikali itahakikisha unafanyika kwa amani na kila mmoja kuheshimu Katiba na sheria.
“Niwaombe wote kwenye siasa, nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa sheria hivyo tuzizingatie na Baba Askofu yote uliyoyasema nitayachukua na kuyapeleka kwake na yaliyopo chini yangu nitayachukua na kuyafanyia kazi,” amesema.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba akimkaribisha Dk Biteko amesema Serikali mkoani huo itahakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na uhuru na kila mmoja anashiriki pasipo bughudha yoyote.
Aprili 25, 2025, katika hotuba ya Rais Samia alisema ni matumaini yake amani iliyopo itaendelea kudumisha sifa ya kuwa ni kitovu cha amani na nchi ya kidemokrasia iliyojengeka juu ya misingi ya uhuru na haki.
“Serikali imejipanga kuhakikisha mahitaji yote ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yanapatikana kwa ukamilifu na kwa wakati.
Aidha, tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya utulivu na amani katika kipindi chote cha matayarisho hadi wakati wa uchaguzi, ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki,” alisema Rais Samia.
Mbali na Dk Biteko wengine waliokuwapo ni Waziri wa Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, Naibu Waziri wa Mambo ya nje Cosato Chumi na Naibu Waziri wa Tamisemi, Zainabu Katimba na wakuu wa wilaya za mkoa huo.
Maelezo ya Kardinali Pengo
Kardinali Pengo wakati wa kumuweka wakfu, amesema maana ya Uaskofu ni jina linalomaanisha utumishi na Askofu anapaswa kutumika kuliko kutawala kadiri ya agizo kutoka kwa mwalimu wao.
Amesema Askofu huyo anatakiwa kuhubiri neno wakati unaofaa na usiofaa, kuonya kwa uvumilivu na mafundisho na asiache kuomba kutoka katika utimilifu wa Kristo ambaye ni mwingi wa neema kwa ajili ya watu anaokabidhiwa.
"Uwe mgawaji wa mafumbo ya Kristo msimamizi na mlinzi mwaminifu katika kanisa mnalokabidhiwa, umeteuliwa na baba ili uiongoze familia yake umkumbuke zaidi mchungaji anayewajua kondoo zake na wao wanamjua," amesema Kadinali Pengo.
Pia, amemtaka kuwapenda wote aliokabidhiwa na Mungu kwa upendo wa kibaba na kindugu wakiwemo mapadri, mashemasi, maskini, dhaifu, wasafiri na wageni na kuwahimiza waumini wote kushirikiana nao kwa njia ya kitume.
Awali, akisoma hati ya uthibitisho wa uteuzi, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Askofu Mkuu, Angelo Accattino amesema Askofu Mihali daima anatakiwa kuwaombea kondoo aliokabidhiwa na kuwatia moyo kumfuata bwana Yesu Kristo.
Askofu Romanus Mihali ametoa shukurani kwa Dk Biteko kwa hotuba nzuri ya kutumia mazingira yaliyopo na kuzungumza kwani huo ni ubunifu wa pekee.
"Mungu akutie nguvu katika uongozi wako na malezi uliyopata kwa kanisa ambayo yamejaa hekima na upendo katika kulitumika Taifa letu," amesema Askofu Mihali.
Pia, Askofu amesema habari watakayoitoa kwa Serikali ni kanisa kuendelea kumlea mwanadamu katika utume wake, awe mtu kamili mwenye hofu ya Mungu katika kutafuta haki na amani.
"Tutaendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma bora za kijamii kwa Watanzania wote," amesema.