Maana na malengo ya siku ya Idd

Muktasari:
- Walezi, wazazi watakiwa kuhakikisha familia zinasherehekea Idd katika njia ipasayo.
Miongoni mwa mambo muhimu katika Uislamu ni kuyatukuza, kuyafurahia na kusherehekea matukufu ya Allah ambayo ni nembo na heshima ya Uislamu.
Moja ya mambo matukufu hayo ni Idd mbili za al- Fitri na al-Adhwhaa, sikukuu ambazo Uislamu umehimiza mno kuzisherehekea ili kuonyesha tofauti ya wazi katika umma huu wa Kiislamu na nyingine.
Katika hadithi ya Mtume iliyosimuliwa na Anas bin Malik, Mjumbe wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuja katika mji wa Madina (na kukuta) watu wakiwa na siku mbili wanazotumia kucheza michezo ndani yake (kusherehekea).
Akasema: “Allah amewabadilishieni siku zilizo bora za Idd kuliko hizo, siku ya al-Adhwhaa (kuchinja) na siku ya al-Fitri (kufungua swaumu).” [Abuu Daud na An Nasai].
Lengo la sikukuu za Idd
Sherehe ya Idd maana yake si kufurahia kutoka kifungoni kwa kuwa mwanadamu alijizuia na kuutawala mwili wake na nafsi yake kwa kipindi cha mwezi mzima, bali ni siku ya kufanya mambo makubwa manne.
Mambo hayo ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukamilisha swaumu, kutathmini mabadiliko tuliyoyapata kwa kufunga, kukumbushana majukumu yajayo baada ya kukamilisha ibada hii adhimu na mwisho kufurahia.
Siku za shukrani
Katika kuonyesha shukrani, Waislamu duniani husali rakaa mbili za sala ya Idd ambazo huambatana na khutba (ujumbe maalumu wa siku hiyo), na adhkaar nyingine za kumtukuza na kumpwekesha Mwenyezi Mungu kama Takbira, Tasbih na Tahmiid.
Katika kuonyesha shukrani hizo, kila Muislamu huyaona yale mafanikio aliyoyapata katika kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa hiyari yake.
Hii ndiyo sababu kila Muumini hujawa na furaha isiyo kifani.
Ikumbukwe kabla ya kuswali sala ya Idd, Waislamu hutazamana hali zao na kugawiana Zakaatul Fitri, jambo linalowezesha kila mmoja kuwa na hakika juu ya mustakbali wa chakula chake na cha familia yake.
Kwa msingi huo, sikukuu za Kiislamu zinakuwa za kipekee kwa kuwa ni sehemu ya ibada.
Siku za tathmini
Suala la pili baada ya shukrani ni kufanya tathmini ya tulichokipata kutoka ndani ya Ramadhani na namna ya kukienzi.
Tathmini ni mpango wa kuhakiki ubora au udhaifu wa kazi tuliyoifanya ili kuweza kujua wapi pakurekebisha au kuimarisha huko mbeleni tukipata fursa tena.
Katika muktadha huu tathmini tunayoifanya ni ya funga zetu tukikagua mambo matatu: Mpango wenyewe (Ramadhani) watekelezaji wa mpango (Waumini) na namna ulivyotekelezwa (tumefanya yaliyotupasa kuyafanya kwa mujibu wa Quran na Sunna?).
Kukumbushana majukumu
Wapo watu miongoni mwa Waumini wa Kiislamu ambao kwao kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ndiyo mwisho wa ibada! Ni wajibu wetu kukumbushana kuwa tunatakiwa kumuabudu Mwenyezi Mungu ndani ya na nje ya Ramadhani. Desturi ya kufanya ibada katika Mwezi wa Ramadhani tu, inajenga dhana Mungu wa msimu, yaani anakuwepo ndani ya Ramadhani tu na hayupo miezi mingine.
Hii ni fikra mbaya iliyojijenga katika fahamu za walio wengi ambayo kimsingi si sahihi, kwani Allah yupo siku zote.
Allah anasema katika Quran: “Mwenyezi Mungu hapana Mungu ila yeye aliye hai, msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote vilivyomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake?...” [Quran, 2:255].
Binafsi nimepanga kukaa na familia yangu na kujadili maisha baada ya Ramadhani. MaashaAllah wanafamilia katika nyumba yangu wamejitahidi kutekeleza ibada, walau zile za faradhi tu katika mwezi wa Ramadhani, lakini je tutaweza kuendeleza ari hii ya kufanya ibada baada ya Ramadhani?
Naamini itawezekana tukikaa chini na kukumbushana majukumu yetu kwenda mbele!
Watoto wapewe fursa ya kucheza
Kutoka kwa Bi Aisha (Allah amridhie) amesema Abubakr (Allah amridhie) aliingia kwake (kwa Aisha) wakiwepo wajakazi wawili wakipiga dufu mbili na wakiimba kuhusu masiku yao huku Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akiwa amejifunika na nguo yake. (Abubakr) akawakemea kwa kuwakataza, lakini Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akafunua nguo yake akasema:
“Waache ewe Abubakr. Kwa hakika, haya ni masiku ya Idd (sikukuu).”
Wanazuoni wamefafanua kuwa kauli ya Mtume (S.A.W) inaonyesha kuwa ni jambo la kisheria kuwapa watoto wasaa wa michezo katika siku za Idd, na huwasaidia kuwapa furaha ya nafsi na kuupumzisha mwili. Pia, fursa ya kucheza inadhihirisha kuwa, furaha katika Idd ni katika alama za dini.
Uislamu ni dini inayoenda sambamba na maumbile. Katika kufanya michezo mbalimbali, kuna kuiburudisha roho na kuuchangamsha mwili na kurejesha nguvu baada ya uchovu wa ibada.
Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimwambia Abdullah bin Amr (Allah amridhie): “Hivi sikukufahamisha kuwa wewe unafunga mchana na unasimama kisimamo cha usiku?”
Akasema: “Ndiyo ninafanya hivyo ewe Mjumbe wa Allah.” Akamwambia: “Usifanye hivyo. Funga na ufungulie. Simama na ulale kwani hakika kiwiliwili chako kina haki na jicho lako lina haki na mkeo anazo haki zake juu yako.”
Alichomaanisha Mtume ni kuwa, si kwamba kila wakati ni ibada bali kuna nyakati za mapumziko, nyakati za kukaa na familia na kuna nyakati za michezo yenye manufaa.
Hata hivyo, miongoni mwa mambo yanayochangia kuharibu na kusababisha mmomonyoko wa maadili ni michezo isiyozingatia mipaka ya kisheria, kimavazi na pia katika michanganyiko ya wanaume na wanawake, ikiwemo uimbaji nyimbo ambazo zimeambatana na ala za muziki.
Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alisema: “Kutakuja kuwa na watu katika umma wangu wanahalalisha zinaa, kuvaa hariri, pombe na muziki.” [Bukhari]. Kuwakusanya watoto na kuanza kuwapigia ngoma na muziki wakiimba na kucheza ni kuwalea katika malezi mabaya ya kupenda vitu hivi vya haramu na hatimaye kuviinga.
Ukipita mitaani utakuta mabango ya vijana yakielekeza mipango na maandalizi ya safari za ufukweni katika sikukuu za Idd zinazojumuisha vijana wa kiume na wa kike na kutawaliwa na ulevi, muziki na maasi mengine.
Kufanya haya ni kuiharibu sura nzima ya sikukuu ya Kiislamu inayopingana na vitendo vyote vyenye kukiuka taratibu za dini. Si jambo jema kuandaa mazingira ya furaha kwa kumuasi Allah aliyetukuka.
Ni jukumu la walezi na wazazi kuhakikisha kuwa familia zao zinasherehekea Idd katika sura inayoonyesha utofauti mkubwa kati ya sherehe za Kiislamu na sherehe nyingine.
Kwa upande mwingine, katika sikukuu ya Idd, watu hupenda kuvaa mavazi mapya na mazuri. Hili si jambo baya wala si jambo linalopingana na sharia.
Kiuhalisia, Uislamu unatutaka tuvae nguo mpya na nzuri, kadri ya uwezo unavyoturuhusu.
Hata hivyo, tatizo lipo katika aina ya mavazi yenyewe tunayoyanunua, hasa upande wa wanawake na watoto.
Asilimia kubwa ya mavazi haya hayazingatii vigezo vilivyoainishwa katika shari.
Tusichukulie udogo wa mtoto kama kisingizio cha uhuru wa kumvalisha mavazi ya ajabu. Hii ni hatua ya malezi ambayo inataathira kubwa kwa mustakbali wa mtoto. Waswahili wanasema: “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo” na “Samaki mkunje angali mbichi”.
Tuhakikishe kuwa wake zetu na mabinti zetu wanavaa mavazi ya stara ili tupate rehema za Allah.
Imeandikwa na Mwandishi Maalumu