Ma-RC kuimarisha ulinzi bwawa la Nyerere
Muktasari:
- Wakuu wa mikoa ya Pwani na Morogoro waahidi kuimarisha ulinzi muda wote katika utekelezaji wa bwawa la kufua umeme la JNHPP lililopo katika mikoa hiyo.
Dar es Salaam. Wakuu wa mikoa ya Morogoro na Pwani kunakotekelezwa mradi wa Bwawa wa Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), wamemuhakikisha Rais Samia Samia Suluhu Hassan ulinzi na usalama katika mradi huo.
Wameeleza hayo leo Alhamisi, Desemba 22, 2022 katika hafla ya kufunga njia ya mchepusho wa maji na kuanza kujaza maji katika bwawa la JNHPP. Shughuli hiyo ilishuhudiwa Rais Samia, marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na baadhi ya viongozi wengine na wananchi.
“Mimi na dada yangu (Fatma Mwasa- Mkuu wa mkoa wa Morogoro), hatutakuangusha tunakuhakikisha ulinzi na usalama kitakuwa kipaumbele chetu, Mungu ilimpendeza bwawa hili lijengwe katika mikoa hii,”
“Bwawa hili lipo hapa lakini maji yake yanatoka katika mikoa mingi, tumejipanga pia katika ulinzi wa mazingira hasa vyanzo vya maji ili bwawa kupata maji na kuleta tija. Umeme sio starehe tena ni sehemu muhimu ya mwananchi,”amesema Abubakar Kunenge mkuu wa mkoa wa Pwani akitoa salamu za mkoa huo.
Naye, Mwasa amesema bwawa hilo likianza kutoa huduma mkoa wa Morogoro utafikisha asilimia 93 ya umeme wa maji unaozalishwa mkoani humo kupitia mabwawa mengine ya Kihansi, Kidatu.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa bwawa hilo mkoa wa Morogoro umejipanga kuulinda mradi huo wakati wote ikiwemo ukianza kutoa huduma.
“Tunakushukuru kwa kuendeleza kutekeleza mradi huo hadi kufikia hatua ya leo, haya ni mafanikio makubwa sana na Watanzania hatuna budi ya kukupongeza na kukushurukuru,”amesema Mwasa