Chande: Bado kuna safari ndefu kufikia umeme wa viwanda

Muktasari:
- Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande amesema mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha kunakuwa na umeme wa kuendesha uchumi wa viwanda.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande amesema, licha ya juhudi za Serikali kuongeza vyanzo vya umeme likiwemo Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), bado kuna safari ndefu kufikia umeme wa uchumi wa viwanda.
Ameyasema hayo leo Desemba 21 katika mjadala wa Mwananchi- Twitter Space unaoendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited.
Amesema Mradi wa Bwawa wa Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) unaotarajiwa kukamilika mwaka 2024 ni sehemu ya hatua za kupunguza changamoto hizo.
“Mradi huu utaleta umeme mwingi kwenye gridi, lakini mradi huu ni moja kati ya hatua ya safari ndegu ambayo tunayo kama nchi ya kuzalishaji kusafirisha na kusambaza umeme,” amesema Chadema leo Desemba 21, 2022 wakati wa mjadala.
Katika ufafanuzi wake, Chande amesema utafiti uliofanyika katika majarida mbalimbali unaonyesha ili uwewe na umeme wa kutosha kwa ajili ya viwanda na kukuza uchumi kila watu milioni moja wanahutaji megawati 1,000.
“Kwa idadi ya watu milioni 60, utaona tunahitaji umeme megawati 60,000 lakini kwa sasa tuna megawati 1500, tukileta hii 2115 tutakua na takribani megawati 3,800. Tunakazi kubwa ya kuongeza uzalishaji wa umeme,” amesema Chande.
Katika hatua nyingine, Chande amesema kama hakutakuwa na changamoto, ratiba ya kukamilisha mradi huo inabaki kuwa mwaka 2024.
“Hakuna aliyetegema Covid19, utaona pia kama bwawa hilo ikitokea changamoto tutatoa taarifa lakini mambo yakienda vizuri Juni mwaka 2023 tutakuwa tumemaliza,” amesema
Kesho Desemba 22, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua hatua ya kuanza kujaza maji katika bwawa hilo lililokamilika asilimia 79 ikiwa ni matokeo ya uwekezaji wa Sh6.5trilioni zitakazokata kero kabla ya 2025.
Bwawa hilo lenye uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 33.2 za maji eneo la Mto Rufiji mkoani Pwani, lilianza kujengwa 2019.