Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvutano pande mbili NCCR-Mageuzi msajili atoa msimamo

Muktasari:

  • Chama cha NCCR-Mageuzi kinakabiliwa na mvutano wa kiuongozi baada ya James Mbatia kudai kurejeshwa madarakani. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesisitiza kuwa haitambui uongozi wake, bali inautambua Haji Hamis aliyechaguliwa Machi 2025.

Dar es Salaam. Chama cha NCCR-Mageuzi kimekumbwa na mvutano wa kiuongozi, kufuatia madai kuwa aliyekuwa mwenyekiti wake, James Mbatia, alivamia ofisi za chama hicho kwa nia ya kurejesha madaraka.

Hata hivyo, Mbatia na wafuasi wake wamekanusha tuhuma hizo, wakizitaja kuwa ni za kupotosha.

Kutokana na mvutano huo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kupitia kwa Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, imethibitisha kuwa imemwandikia barua James Mbatia ikieleza wazi kuwa ofisi hiyo haiumtambui uongozi wake, kwani NCCR-Mageuzi tayari ina uongozi halali unaotambulika na mamlaka hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 9, 2025, Nyahoza amesema ofisi ya msajili inautambua uongozi wa Mwenyekiti Haji Hamis, aliyechaguliwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Machi 2025 kuiongoza NCCR-Mageuzi.

Uongozi huo uliingia madarakani baada ya Septemba 2022, ambapo Mkutano Mkuu wa chama hicho pamoja na viongozi wengine kumvua uanachama na uenyekiti wake aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mbatia.

Hata hivyo, Mbatia alifungua shauri mahakamani, akipinga hatua hiyo kwa madai hakupata nafasi ya kujitetea.

Mei mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa uamuzi kufuatia kesi hiyo, ikifuta maamuzi ya kumvua uanachama na kuondolewa kwake katika nafasi ya uenyekiti. Mahakama ilitafsiri hatua zilizochukuliwa kuwa batili kisheria.

Kupitia mkutano na waandishi wa habari jana Julai 8, 2025, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Evaline Munisi, alisema Mbatia alisimamishwa uongozi na kikao cha Halmashauri Kuu na hajapinga hatua hiyo.

“Hata kama Mbatia angekuwa hajamaliza miaka mitano ya uongozi wake, bado angekuwa Mwenyekiti aliyesimamishwa. Mei 5, 2022, alisimamishwa uongozi na kikao cha Halmashauri Kuu.

“Hadi sasa hajapinga hatua hiyo kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 14(2), kupinga hatua ya kufukuzwa uongozi kwa kukata rufaa kwenye kikao cha juu iwapo hakuridhika na maamuzi ya kikao cha chini,” alisema Munisi.


Mvutano ulioibuka

Naibu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Zanzibar, Ameir Ali Mshindani, akizungumza na Mwananchi leo Julai 9, 2025, amesema jana, , ofisi zao zilivamiwa na watu aliodai ni upande wa Mbatia wakitaka kutwaa ofisi.

“Vurugu zilitokea juzi kwa upande wa Mbatia kuvamia ofisi kinyume cha sheria na uongozi. Tayari uchaguzi umefanyika na tuna uongozi mpya, wanapaswa kuheshimu uongozi uliopo.

“Kama ameshinda mahakamani, uchaguzi umeshafanyika na ofisi ya msajili inatambua uongozi uliopo madarakani. Walituomba tukae nao meza moja, lakini sisi hatutakubali kwa sababu hatujui lengo lao,” amesema.

Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana Taifa NCCR-Mageuzi, Nicholaus Jovin, aliyesema hakuna vurugu waliyosababisha wao na hakuna mtu aliyepigwa. Jovin ni mmoja wa viongozi waliokuwa kwenye uongozi wa Mbatia.

“Nilikuwa nasimamia shughuli zote zilizoendelea pale. Hakuna ukweli katika hicho kinachoelezwa, hakuna vurugu wala mtu yeyote aliyepigwa,” amesema Jovin.


Msimamo wa Ofisi ya Msajili

Nyahoza amesema wamemwandikia Mbatia barua kuwa ofisi hiyo haimtambui, kwani alipokwenda mahakamani hakwenda kuharamisha mkutano mkuu wa chama hicho uliomvua uanachama.

“Tumemtumia barua jana na amepokea. Sisi tunautambua uongozi uliopo na si yeye. Alipokwenda mahakamani hakwenda ‘ku-challenge’ mkutano mkuu uliomvua uanachama, hivyo muda wake umekwisha; uongozi uliopo ndiyo tunautambua,” amesema.

Muda ambao uongozi wa Mbatia ungekoma, ulioanza Julai 27, 2019, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, ulipaswa kuwa Julai 27, 2024

Hiyo ni kulingana na Katiba ya NCCR-Mageuzi, Sura ya 11, inayozungumzia mambo ya jumla ya chama hicho, Ibara ya 30(1) – uchaguzi mkuu wa viongozi wa chama hicho utafanyika kila baada ya miaka mitano au vinginevyo kwa azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa.

Kifungu (3) kinaeleza kuwa ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na aliyekuwa ameshikilia nafasi hiyo kujiuzulu, kufariki, au kufukuzwa kwa mujibu wa Katiba hii, uchaguzi unaweza kufanyika wakati wowote bila kungoja kipindi cha miaka mitano cha uongozi uliopo katika chama kupita.