Ma- DC wawili wapata ajali msafara wa Waziri Mkuu Morogoro

Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Agosti 14, 2021 majira ya mchana.
Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando na mwenzake wa Ulanga, Ngolo Malenya wamepata majeraha baada ya gari walilokuwa wamepanda wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa kugongwa na gari lingine mali ya Wizara ya Afya lililokuwa likitokea Mkoani Dodoma.
Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Agosti 14, 2021 majira ya mchana.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fotunatus Musilimu amesema ajali hiyo imetokea eneo la Dakawa, wakati wakuu hao wa wilaya wakiwahi kwenye msafara wa Waziri Mkuu uliokuwa ukitokea kwenye Kiwanda cha Sukari cha Mbigiri, kilichopo Wilayani Kilosa na kuelekea kiwanda cha Nyama cha Nguru Hills Ranch kilichopo Wilayani Mvomero.
Kamanda Musilimu amesema gari walilokuwa wamepanda wakuu hao wa wilaya lilikuwa nyuma ya msafara na hivyo dereva alilazimika kuyapita magari yaliyokuwa yameruhusiwa na trafiki na ndipo gari hilo lilipogongwa.
“Wao walikuwa nyuma zaidi na gari lao liliachwa na msafara, askari aliyekuwa akisimamisha magari alipoona msafara umepita alianza kuyaruhusu magari mengine kuendelea na safari, ndipo dereva wa gari walilokuwa wamepanda viongozi hawa aliamua kuyapita magari mengine kwa lengo la kwenda kuungana na msafara, ghafla gari la wizara lilitokea kwa mbele na kugongana nalo uso kwa uso,” amesema Kamanda Musilimu.
Amesema wakuu hao wa wilaya walipelekwa katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Kusirye Ukio amesema tayari wameshawapatia matibabu ya awali na utaratibu wa kuwahamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu na vipimo zaidi vya uchunguzi zinafanyika.