Lukuvi: Nyumba zinazouzwa na NHC ziondolewe VAT

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii jana. Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Angelina Mabula. Picha na Omar Fungo
Muktasari:
· 55.12bil: Kiwango cha fedha ambacho wizara ya ardhi ilikusanya katika mwaka wa fedha 2015/16 sawa na asilimia 78.74 ya lengo la kusanyaji maduhuli ya Serikali.
· 38.5% : Sehemu ya bajeti ya Sh54.3 bilioni ambayo wizara ya ardhi ilipokea hadi Machi mwaka huu kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Dar es Salaam. Wizara ya Ardhi imependekeza kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kwa nyumba zisizozidi Sh40 milioni zinazouzwa na taasisi za umma.
Waziri wa Ardhi, William Lukuvi aliieleza Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuwa ameshapeleka pendekezo kwa Baraza la Mawaziri kuondoa kodi hiyo kwenye nyumba zinazouzwa na Shirika la Nyumba (NHC) na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) iwapo zitauzwa kwa gharama isiyozidi Sh40 milioni ili kuwapatia wananchi unafuu.
“Nilipowauliza wataalamu wangu kikomo cha nyumba ya bei nafuu ni shilingi ngapi, walinitajia Sh49.9 milioni, lakini niliona haiwezekani. Ndiyo maana nilipendekeza serikalini VAT iondolewe kwenye nyumba zisizozidi Sh40 milioni,” alisema Lukuvi. Wajumbe wa kamati hiyo kwa umoja pia waliikomalia wizara hiyo kuisimamisha kwa muda Mamlaka ya maendeleo ya mji wa Kigamboni (KDA), kwa sababu haipatiwi fedha za kutosha na mradi husika unasuasua.
Aomba Sh62 bilioni
Lukuvi aliomba kupatiwa Sh61.83 bilioni katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo, ikiwa ni ongezeko la Sh7.2 bilioni kutoka kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016.
Aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa kati ya Sh61.83 wanazohitaji, Sh16.35 bilioni zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa wizara hiyo. Wizara hiyo inaomba kutumia Sh25.48 bilioni kutoka katika fungu hilo kwa ajili ya matumizi mengineyo, ambayo yanajumuisha Sh10 bilioni za kuziwezesha halmashauri kusimamia upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye alisema baada ya kusikiliza mapendekezo hayo wataanza kuijadili leo kwa kina kuona iwapo ni halisi au la.