Lissu: Viongozi wa dini, mabalozi wawe watazamaji uchaguzi Chadema

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu ametaka uchaguzi wa ndani wa chama hicho utazamwe na viongozi wa dini na mabalozi wa nchi marafiki.
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadem-Bara, Tundu Lissu amependekeza viongozi wa dini na mabalozi wa nchi marafiki, waalikwe kuwa sehemu ya watazamaji wa uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Pendekezo hilo limetokana na kile alichofafanua, kwa sasa chama hicho kina idadi ndogo ya wazee wastaafu ambao kikatiba ndio wanaopaswa kupendekezwa na Kamati Kuu kuusimamia uchaguzi huo.
Sambamba na hilo, ameeleza kusikitishwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho waliopinga pendekezo lake la kuwekwa ukomo wa madaraka, akisema hilo ni moja ya doa katika harakati za upinzani kudai mfumo bora na wa kidemokrasia wa utawala.
Lissu anakuja na mapendekezo hayo, ikiwa ni siku 20 zimebaki kuelekea kufanyika mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chadema, Januari 21, mwaka huu ambapo atachuana na mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Freeman Mbowe na wagombea wengine wawili ambao ni Romanus Mapunda na Charles Odero.
Lissu ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Januari mosi, 2025, alipozungumza mubashara kutoka nje ya nchi, kuelekea uchaguzi wa ndani wa chama hicho na mambo mbalimbali ya kukumbukwa mwaka 2024.
Amesema kwa miaka 10 iliyopita, chama hicho kimepoteza wazee kwa baadhi kufariki na wengine wanaugua, huku wakiwepo wale wenye majukumu ya ndani ya Chadema, hivyo wanakosa sifa ya kuwa wasimamizi.
“Katika mazingira haya ni muhimu kwa Kamati Kuu kutafakari suala hili kwa kina na kwa muda muafaka, ili kulitafutia suluhu inayofaa na muda unaotosha kabla ya siku ya uchaguzi,” amesema.
Hata hivyo, amependekeza pamoja na wazee wastaafu watakaopatikana, Kamati Kuu inapaswa kuwaomba viongozi wa kidini na mabalozi wa nchi za kigeni kuhudhuria mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho, kama wageni waalikwa na watazamanji wa uchaguzi huo.
Amesema kufanya hivyo kutazuia mipango ya waovu ya kuvuruga uchaguzi na kuongeza uzito wa uchaguzi husika.
Mnyika ajibu
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kujibu hilo, amesema mamlaka ya usimamizi wa uchaguzi wa chama hicho, yamewekwa wazi katika kifungu cha 7 (31) cha kanuni za Chadema.
Amesema kifungu hicho kinasema uchaguzi wa ndani wa chama hicho utasimamiwa na wazee wastaafu kama watakavyopitishwa na Kamati Kuu ya chama.
“Kwa sababu hiyo, kama kuna mgombea yeyote ana mapendekezo yoyote anayotaka yatafakariwe kuhusu usimamizi wa uchaguzi, ayawasilishe rasmi kwa Katibu Mkuu, ili naye ayapeleke mbele ya Kamati Kuu,” amefafanua.
Mnyika amesema mgombea huyo anapaswa kuwasilisha mapendekezo hayo kwa kuandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu, akidokeza hajapokea barua yoyote mpaka sasa.
Katika hotuba yake hiyo, Lissu pia amependekeza fedha zilizopangwa kwa ajili ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi, zitumike kugharimia malazi yao kwa kipindi chote watakachohudhuria mkutano.
Fedha za chakula, ametaka zilipwe kwa wajumbe watakaosafiri au baada ya kuwasili katika eneo utakapofanyika mkutano mkuu wa uchaguzi.
“Mambo haya yakifanyika kama inavyopendekezwa, mianya mingi ya rushwa kwenye uchaguzi itazibwa na tutaweza kufanya uchaguzi wa chama ulio huru na haki,” amesema.
Ukomo wa madaraka
Lissu amesema anashangazwa na mapokeo ya baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho kuhusu pendekezo lake la kuwekwa ukomo wa madaraka ya uongozi ndani ya Chadema.
Lissu ameeleza kutokana na mapokeo hayo, kinachopaswa kuhojiwa ukomo wa madaraka unawahusu marais pekee?
“Tangu tuingie kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi, ni viongozi wa upinzani tu ndio wameng’ang’ania madarakani kwenye vyama vyao kwa muda mrefu zaidi, hili ni moja ya madoa makubwa katika harakati za kudai mfumo bora na wa kidemokrasia wa kiuchaguzi na utawala wa nchi yetu,” amesema.
Amekwenda mbali zaidi na kueleza wanasiasa wa upinzani ni mashahidi wa namna CCM ilivyowatukana kwa vyama vyao kuwa mali binafsi za viongozi na familia zao kwa sababu ya kukaa madarakani muda mrefu.
“Kama hoja kuu ya kupinga ukomo wa madaraka kwenye vyama ni kwamba uongozi wa vyama vya siasa ni kujitolea, wanaopalilia hoja hii wamenyamaza kuhusu pendekezo langu la kuwekwa ukomo wa madaraka kwenye nafasi za udiwani na ubunge wa viti maalumu ambazo zote si kazi za kujitolea, ukimya huu una kishindo kikubwa,” amesema.
Kwa sababu ya kukosekana ukomo wa madaraka kwenye viti maalumu, amesema wanawake wengi wanashindwa kuwezeshwa na wachache waliofanikiwa wanaendelea kujihakikishia umalkia.
Amani kuelekea uchaguzi wa ndani
Desemba 19, mwaka jana, Mnyika alitoa taarifa katika mitandao ya kijamii akidai kuna watu wanataka kutengeneza vurugu kwenye uchaguzi huo.
Alisema ni wajibu wa wagombea kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa amani ambacho ni kigezo cha uchaguzi huru na haki.
Ili kutimiza wajibu huo, aliwaasa wajumbe wa timu yake ya kampeni na wafuasi wake wote, kuchukua kila hadhari kulinda maisha na usalama wao, huku akisisitiza waepuke vishawishi vya kuwa chanzo cha vurugu.
“Tutashinda na chama chetu kitashinda kwa kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na kwa hiyo unakuwa huru, haki na wa kuaminika,” alisema.
Alisema hatua za uchaguzi zifanyike katika saa za mchana na kwa vyovyote zisifanyike usiku, ili kuondoa uwezekano wa watu wenye nia mbaya kutumia nafasi hiyo kuharibu uchaguzi.
Alitaka uwazi katika kuhesabu na kutangaza matokeo na kuhakikisha wanaoruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa mkutano ni wajumbe halali, wageni waalikwa na wahudumu maalumu watakaokuwa na vitambulisho.
Mawakala wa wagombea, alitaka wapewe taarifa zote mapema za maandalizi ya uchaguzi na kutambulishwa na wahudumu wote watakaokuwepo.
Sambamba na hayo, Lissu amesema kwa sababu ya changamoto zilizoshuhudiwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, ni wazi nchi ipo katika utawala wa kiimla usiokubali siasa za ushindani.
Kutokana na yaliyotokea, Lissu ameeleza iwapo wataendelea kushiriki chaguzi zijazo, ukiwemo uchaguzi mkuu mwaka huu, bila Katiba mpya hali itakuwa ile ile.
“Kwa sababu hizi zote na kama ambavyo Kamati Kuu imeelekeza, msimamo wetu kwa sasa unatakiwa kuwa, bila mabadiliko hakuna uchaguzi na msimamo huu unawezekana tu iwapo kutakuwa na uongozi mpya, fikra mpya na mbinu mpya za mapambano ya kidemokrasia,” amesema.
Baada ya miaka 21 madarakani, amesema wasidanganyane kwamba miaka mitano tena itawaletea mambo mapya ambayo hawakuyaona katika miongo miwili ya awali.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.