Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA MALOTO: Mbowe, Lissu wameitumbukiza Chadema vita ya pembe tano

Vita ya hatima ndicho kinaendelea Chadema. Siyo vita na hatima kama simulizi ya familia ya Ku, Asia Mashariki, kwenye tamthiliya ya War and Destiny, bali Chadema, hali ilivyofikia, kinachopambaniwa ni hatima.

Uamuzi wa Makamu Mwenyekiti Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, kugombea uenyekiti dhidi ya mwenyekiti aliye ofisini kwa sasa, Freeman Mbowe, umetengeneza pembe mbili za hatima. Hatima ya Lissu, vilevile Mbowe.

Hatima za wanasiasa hao wawili, hazihusu kesho yao Chadema pekee, bali pia mustakabali wao wa kisiasa baada ya uchaguzi. Lissu atakuwa mwanasiasa wa namna gani baada ya kushindwa? Je, Mbowe atatazamikaje kisiasa baada ya kuangushwa Chadema?

Mbowe na Lissu, kila mmoja ana historia kubwa na Chadema. Baada ya yote ambayo wamefanya, je, nani angependa mwisho wake uwe kuangushwa kwenye uchaguzi? Swali hili ndilo linaloleta uamsho wa ari ya kupambana kwa ajili ya hatima.

Lissu, amekuwa alama ya Chadema tangu aliposhinda ubunge jimbo la Singida Mashariki, akawa Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, na alisimama mstari wa mbele nyakati zote kila chama hicho, viongozi wake au wanachama walipopata changamoto za kisheria.

Dar es Salaam, mahakamani Kisutu mpaka Mahakama Kuu, kisha Mahakama ya Rufaa chemba kwa chemba. Mkoa hadi mkoa, Lissu alifika kuhakikisha anaitetea Chadema, viongozi na wanachama. Lissu, bila shaka anajifahamu kuwa yeye ni rasilimali muhimu kwenye chama.

Sauti yake bungeni, kwenye mikutano ya hadhara au na waandishi wa habari. Lissu anafahamu ni kwa kiasi gani amejitoa kwa ajili ya Chadema. Uhusika wake kwenye mapambano ni sababu ya ulemavu alionao leo. Hatembei kikamilifu kama zamani. Mwilini anaishi na risasi.

Tanzania inajua, dunia inafahamu kuwa shambulio la risasi 38 dhidi ya Lissu Septemba 7, 2017, sababu ni uhusika wake kisiasa. Risasi 16 zilipenya mwilini na kumfanya awe na ulemavu leo. Kila alichokuwa anapambania, kilikuwa na faida ya moja kwa moja kwa Chadema.

Tafakari, Lissu anashindwa uchaguzi Chadema katikati ya ushindani wa sasa ambao mayowe ya upande wa pili, yanavyosikika, utadhani hajawahi kuwa na mchango wowote kwenye chama. Zingatia, Lissu ni binadamu, ana moyo na anazo hisia.

Ukishajenga tafakuri yenye kina cha kutosha, utabaini kuwa uchaguzi wa uenyekiti Chadema, umemtumbukiza Lissu kwenye mazingira ya kuona kuwa hana namna nyingine zaidi ya kupambana. Mwanafasihi mmoja alipata kusema, kupambana linapobaki chaguo la pekee, basi pambana kama vile uhai wako unategemea ushindi wa hilo pambano.

Mapambano ya Lissu yana sura mbili muhimu. Mosi, mustakabali wake ndani ya Chadema. Je, ataishi kwenye mazingira gani, akizungukwa na kundi ambalo lilimtweza na kumshusha hadhi kipindi chote cha kuelekea uchaguzi? Vipi kuhusu kesho yake ya kisiasa? Lissu yupo vitani. Tena vita kali kupigania hatima yake.

Mbowe, kabla hajawa mwenyekiti, Chadema haikuwa na nguvu kuongoza siasa za upinzania Tanzania. Mwaka 1995 mpaka 2000, Chadema kilikuwa chama cha tatu, kwa nguvu ya upinzani, nyuma ya NCCR-Mageuzi na CUF. Tena, Chadema ililingana na UDP kwa idadi ya wabunge.

Mwaka 2000 kwenda 2005, Chadema ilisalia nafasi ya tatu, nyuma ya CUF na TLP. Hiyo nafasi ya tatu, Chadema ililingana na UDP kwa idadi ya wabunge. Mwaka 2004, Mbowe alishika usukani wa chama, kisha mwaka 2005, Chadema kikawa chama cha pili kwa nguvu ya upinzani nyuma ya CUF, halafu mwaka 2010, Chadema ikasimika uongozi wake wa kambi ya upinzani.

Chadema haikupanda ngazi kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania kwa bahati au upepo wa kisiasa uliovuma katika uchaguzi mmoja. Maarifa makubwa, uwekezaji na mikakati endelevu. Chadema ilisukwa. Mbowe ndiye msusi mkuu.

Katika ususi wake, aliweza kuibua vipaji vingi vya kisiasa. Chama kilipotoa ahadi njema ya kisiasa, kikavutia wanasiasa wengine mahiri, kutoka vyama vingine, wakajiunga Chadema. Kila kitu kilichofanyika kuijenga Chadema, Mbowe anakijua na anajua yeye ni rasilimali ya namna gani.

Mbowe kwa miaka 10 (mwaka 2010 mpaka 2020), aliongoza kambi ya upinzani yenye wabunge wengi, ambao upatikanaji wake yeye binafsi na kama kiongozi wa taasisi, alicheza karata mali jimbo baada ya jimbo ili kufanikisha ushindi.

Safari ya kujenga upinzani imara Tanzania, imekuwa na gharama nyingi kwa maisha binafsi ya Mbowe. Kukaa jela miezi hadi miezi, hata kuhukumiwa kifungo, kupoteza mali zake, jengo lililokuwa na Club Bilicanas, Posta, Dar es Salaam, halafu shamba lake la greenhouse, likaharibiwa Hai, Kilimanjaro.

Tafakari; Mbowe anajua amejitoa kiasi gani kwa chama na anafahamu maumivu ya kujitoa kwake. Katika hali hiyo, homa ya uchaguzi wa mwenyekiti Chadema imepanda juu. Mbowe anasikia mayowe ya upande wa pili yakimsiliba, katika namna ambayo utadhani hajawahi kuifanyia Chadema chochote cha maana.

Kama binadamu lazima awaze, ikiwa bado yupo kwenye kiti anasemwa, anazongwa na kushushwa hadhi kwa kiwango hicho, je, akishindwa uchaguzi itakuwaje? Swali hilo ndilo linalochochea wito wa mapambano. Lazima kupambana kulinda heshima, historia aliyoiandika na hatima yake.

Ikiwa anasakamwa namna hii sasa hivi, Mbowe akishindwa uchaguzi, mchango wake utakumbukwa? Upo wakati ataitwa kwenye vikao vya chama ili kuchota busara zake? Maswali hayo bila shaka ndiyo ambayo Mbowe anajiuliza. Na kwa nafasi yake, utaona ni kiasi gani hana jinsi zaidi ya kupambana kubaki kwenye kiti.

Pembe tano

Tayari pembe ya kwanza na ya pili ni vita ya hatima za Lissu na Mbowe. Pembe ya tatu ni hatima ya Chadema. Sura ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Chadema, inatoa picha ya mgawanyiko mkubwa. Kwa vyovyote vile chama hakitabaki imara.

Hivi sasa, chama hakina wa kukipigania, ingawa Lissu na Mbowe, kila upande unaona upo sahihi na kile wanachofanya ndiyo kukipigania chama. Chadema ambayo Mbowe ataondoka kwa masimango, haitabaki salama. Chadema ambayo Lissu atawekwa pembeni akiwa na kinyongo cha mashambulizi makali dhidi yake, haitakuwa na uimara ilionao sasa.

Chadema, kama chama, kwa ustawi na uimara wake, bila shaka inawahitaji Mbowe na Lissu kwa pamoja. Bahati mbaya, uchaguzi wa mwenyekiti, umefanya wakosekane watu wanaopigania masilahi ya Chadema, isipokuwa Mbowe na Lissu.

Pembe ya nne ni timu ya Mbowe. Wapo kwenye mapambano makali kuhusu hatima zao. Wanajua kuwa Lissu akishinda, hawatakuwa na chao. Vivyo hivyo, timu Lissu, wanapigana kufa au kupona kuhakikisha mtu wao anashinda ili kutetea hatima zao.

Ingewezekana Mbowe na Lissu kumaliza tofauti zao kwa masilahi ya Chadema, kama kusingekuwa na mwangwi wa timu zao. Watu wa timu Lissu wanaona si salama kwao, kama mtu wao ataelewana na Mbowe, halafu ajitoe kuwania uenyekiti. Timu ya Mbowe inaona hatari kubwa mbele, endapo Mbowe atakubali kujitoa kwenye uchaguzi na kumuunga mkono Lissu.