Lissu, Jamhuri wavutana nyongeza ya ushahidi mpya
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akiwa katika kisimba cha Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Muktasari:
- Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, anakabiliwa na kesi ya uhaini inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali kuhusiana na hatima ya Uchaguzi Mkuu 2025.
Dar es Salaam. Malumbano makali ya hoja yameibuka mahakamani katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kuhusiana na ushahidi mpya wa Jamhuri, huku Lissu akitahadharisha kuwa yuko tayari kujadili yaliyotokea kwenye Uchaguzi Mkuu 2025 ili dunia ijue.
Malumbano hayo yametokana na notisi iliyowasilishwa na Jamhuri mahakamani ya kuongeza ushahidi mpya kwa mmoja wa mashahidi wake, unaotokana na upelelezi wa matukio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambayo Lissu ameipinga vikali kuwa si halali na kwamba itaibua matatizo makubwa.
Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusu kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko..., kwa hiyo tunaenda kikinukisha..., sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kweli kweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana...”
Kesi hiyo inasikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Leo, Jumatatu, Februari 23, 2026, upande wa mashtaka umeieleza Mahakama kuwa Februari 18, 2026 uliwasilisha mahakamani kwa njia ya mtandao notisi ya kuongeza ushahidi katika kesi hiyo.
Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema Jamhuri imewasilisha notisi hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 308(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023.
Katuga amesema katika notisi hiyo hawaombi kuongeza shahidi mpya, bali ushahidi mpya katika ushahidi wa shahidi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Amin Mahamba, na kwamba wameambatanisha kiini cha ushahidi huo mpya.
“Ushahidi huo haujawa committed (haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi kwenye Mahakama ya ukabidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu) katika shauri hili,” amesema Katuga.
Hivyo, amesema notisi hiyo inakuja kukidhi matakwa ya kifungu hicho cha 308(1), kinachoeleza kuwa hakuna ushahidi wa shahidi unaoweza kutumika kama haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.
“Kama ambavyo notisi hii inajieleza na kiambatanishi chake, substance (kiini) cha ushahidi huo ni kwamba ACP Mahamba alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wakati wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025 na baada ya uchaguzi,” amesema Katuga.
“Kile kilichoonekana baada ya upelelezi hakikusomwa wakati wa mwenendo kabidhi.”
Katuga amesema ushahidi huo umetambulika kwa upande wa mashtaka wakati wa maandalizi ya shahidi huyo, ACP Mahamba, alipoitwa kuja kutoa ushahidi katika kesi hiyo Februari 16, mwaka huu.
Baada ya upande wa mashtaka kumaliza kutoa ufafanuzi wa notisi hiyo na msingi wa ushahidi unaokusudiwa kuongezwa, Lissu amepewa nafasi ya kuwasilisha rasmi pingamizi lake dhidi ya notisi hiyo.
Hoja za pingamizi la Lissu
Katika hoja zake, Lissu amedai msingi wa pingamizi lake umejikita katika kifungu cha 308(1) cha CPA (kilichotumiwa na Jamhuri), ambacho kinazungumzia shahidi ambaye maelezo yake hayakusomwa katika mwenendo kabidhi, na si ushahidi mpya ambao haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.
Lissu amesema ushahidi wa shahidi ACP Mahamba ambao Jamhuri inataka kuuongeza ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi.
Amefafanua kuwa jina lake na taarifa zake zimetajwa na upande wa mashtaka katika ukurasa wa 134 wa rekodi ya mwenendo kabidhi, katika orodha ya mashahidi, akiwa shahidi wa 26.
“Sasa hiyo nyongeza ya maelezo ya shahidi huyo inaingiaje, wakati maelezo yake yalishasomwa kwenye committal? Hii notice inakuwa ya halali?” amehoji Lissu.
Lissu amedai hatua ya Jamhuri kutaka kuongeza ushahidi mpya kwa shahidi ambaye tayari ushahidi wake umeshasomwa kwenye mwenendo kabidhi ni sawa na kutaka kubadilisha hati ya mashtaka.
“Wanataka kubadilisha maelezo ya shahidi kwa kuleta mambo ya uchaguzi mkuu, na hiyo hairuhusiwi kwa mujibu wa kifungu cha 308 chote. Kifungu cha 308 kinahusu shahidi ambaye hakuwepo kabisa, na si kuongeza maelezo ya baada ya matukio,” amesema Lissu na kusisitiza:
“Kama wanataka kubadilisha, waende kwenye kifungu cha 213; watajua cha kufanya, na si kwenda kwa mlango wa uani,” amesema Lissu. “Kwa sababu hiyo, na ni rai yangu kwenu, hiyo notice na yaliyomo muyafutilie mbali.”
Lissu amesema kuwa notisi hiyo, ikiachwa ikakubaliwa na kuingia mahakamani, itafungua mlolongo wa matatizo.
Amesema kitendo cha upande wa mashtaka kutaka kuongeza ushahidi wa shahidi huyo, ambaye Jamhuri imedai alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wa matukio ya kabla na baada ya uchaguzi, wanataka kuzungumzia mambo ya uchaguzi, na kwamba katika hilo naye yuko tayari huku akihoji Jamhuri kama iko tayari.
“Kwa sababu wanataka kuzungumza ya uchaguzi wa mwaka 2025, mtakuwa mmefungulia mabaya. Mimi nipo gerezani, nimeambiwa watu wengi wamekufa kwenye uchaguzi,” amesema Lissu na kusisitiza:
“Waheshimiwa majaji, mkifungulia huo mlango, tutazungumzia mauaji ya kimbari, tutaulizia nani aliua. Hivyo, mkikubaliana na notisi hii, mimi niko tayari kuendelea nayo, na nitataka dunia ijue.”
Kutokana na hoja hizo, Lissu ameiomba Mahakama itupilie mbali notisi hiyo.
Hata hivyo, akijibu hoja hizo, Wakili Katuga amesema notisi hiyo ni halali kwani ipo kwa mujibu wa sheria, kifungu cha 308 cha CPA, ambacho ni mlinzi au msisitizo wa kifungu cha 263 (zamani 242) cha CPA, ambacho msingi wake ni kumfanya mshtakiwa afahamu kikamilifu ushahidi atakaokutana nao wakati wa usikilizwaji.
Kwa mujibu wa Wakili Katuga, kifungu cha 308(1) cha CPA kinazungumzia notisi ya shahidi mpya au ushahidi wake ambao haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi.
“Kwa maana hiyo sasa, ushahidi unatakiwa uwe umewekwa wazi, na kama sivyo, ni busara kwa upande wa Jamhuri kuuomba uongezwe kama nyongeza,” amesema Wakili Katuga na kusisitiza:
“Sisi kazi yetu ni kuiomba Mahakama, na Mahakama kazi yake ni kuamua, lakini isiogope kupokea na kukubali notisi yetu kwa kuogopa maelezo ya mwenzetu aliyedai kuwa atataka dunia ijue. Sisi tunaona hiyo si sahihi,” amesisitiza Wakili Katuga.
Kwa kuzingatia sababu walizoziainisha, ameiomba mahakama ikubaliane na notisi hiyo ili shahidi akiletwa mahakamani, mshtakiwa asidai kuwa ameshtukizwa, na akaiomba itupilie mbali pingamizi la mshtakiwa.
Majibu ya Lissu
Akijibu hoja za Wakili Katuga, Lissu amesisitiza kuwa kifungu cha 308 cha CPA kinazungumzia shahidi mpya, na si ushahidi mpya wa shahidi, shahidi mpya ni yule ambaye maelezo yake au ushahidi wake haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.
Amedai kuwa, kutokana na kifungu hicho, ushahidi wa ACP Amin Mahamba hautoruhusiwa kwa sababu ushahidi wake ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi.
“Waheshimiwa majaji, mlango wa Amin Mahamba ulishafungwa kwenye committal (mwenendo kabidhi), na kama Jamhuri wanataka maelezo hayo yazungumzwe, basi wamtafute shahidi mwingine azungumzie, na si Amin Mahamba,” amedai Lissu na kusisitiza:
“Kifungu cha 308 kinaelekeza maelezo ya shahidi mpya ndiyo yanayoweza kukubaliwa, lakini kwa ushahidi wa Mahamba milango yake imefungwa, na kama ukikubaliwa, madhara yake ni kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka.”
Akizungumzia kiini cha ushahidi huo unaobishaniwa, Lissu amedai kuwa Aprili 3, 2025 ndiyo tukio lilitendeka, na Aprili 10, 2025 alishtakiwa mahakamani na kupelekwa mahabusu, lakini maelezo hayo ya nyongeza yanahusu kabla na baada ya uchaguzi.
“Waheshimiwa majaji, ya Oktoba ni magumu, hayahusiki kwa sababu ni maafa na hayatakiwi kuingia hapa. Najaribu kuwasaidia majaji kwa sababu yatatupeleka kusiko. Hivyo, naomba majaji msikubaliane na notisi hii, yangu ni hayo tu, waheshimiwa majaji,” amedai Lissu, lakini akasisitiza utayari wake:
“Kama wanataka kujadili ya Oktoba, mimi niko tayari. Je, watayaweza? Maana ya Oktoba kuna machafuko na mauaji ya halaiki, siyo hayo yanayozungumzwa na Amin Mahamba tu. Je, mko tayari?”
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya uamuzi.