Prime
Lissu atoa msimamo baada ya uchaguzi, Mbowe asema…

Muktasari:
- Mbowe asisitiza nidhamu na umoja ndani ya chama, akiwataka viongozi wapya kudumisha maadili na kuimarisha demokrasia.
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, amesema kwa vyovyote itakavyokuwa katika uchaguzi wa chama hicho, atakuwa pamoja na wengine kukijenga chama hicho.
Kauli hiyo ya Lissu, inajibu uvumi wa baadhi ya wadau wa siasa waliosema kuna nafasi ndogo ya mwanasiasa huyo kubaki Chadema iwapo atashindwa uchaguzi.
Uvumi huo, ulitokana na kauli mbalimbali za mwanasiasa huyo, dhidi ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akimtuhumu kuingia kwenye maridhiano na Serikali bila kuwashirikisha viongozi.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akizungumza katika baraza kuu la chama hicho. Picha na Sunday George
Lissu, Freeman Mbowe, na Charles Odero wanachuana kuusaka uenyekiti wa chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mbali na kauli hiyo ya Lissu, Mbowe naye amesisitiza chama hicho hakitavunja umoja wake, licha ya mapito wanayoyapitia, na tofauti zao zitazimwa.
Viongozi hao wamesema hayo leo Jumanne, Januari 21, 2025, kwa nyakati tofauti kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Lissu alikuwa akitoa salamu za kuaga nafasi ya uongozi baada ya kuongoza kwa miaka mitano, huku Mbowe akifungua mkutano huo.
Lissu amesema kwa namna chama hicho na wanachama wake walivyompenda, vyovyote itakavyokuwa katika uchaguzi huo ataendelea kuwa pamoja nao kukijenga.

Makamu Mwenyekiti Chadema Bara, Tundu Lissu akizungumza katika baraza kuu la chama hicho. Picha na Sunday George
"Vyovyote itakavyokuwa leo, tutakuwa pamoja kujenga chama chetu," amesema Lissu na kuibua shangwe kutoka kwa wajumbe.
Sambamba na hilo, amesema ni imani yake ataendelea kuwa na urafiki na Mbowe bila kugombana kama ilivyokuwa kwa miaka 20 iliyopita.
Amesema amekuwa karibu na Mbowe kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita na hawakuwahi kugombana, zaidi ya kutofautiana msimamo.
"Katika kipindi chote hicho, hatujawahi kugombana, hatujawahi kukosana mimi na yeye binafsi, ndiyo tumetofautiana kimsimamo, lakini hatujawahi kugombana," amesema.
Amesisitiza hakuwahi kuwa na ugomvi na Mbowe na matumaini yake hali hiyo itaendekea hata baada ya uchaguzi.
Lissu amesema maneno hayo pia atayasema kwa viongozi wengine, pamoja na kutofautiana msimamo lakini hawakuwahi kugombana.
Kadhalika, mwanasiasa huyo amewaaga wanachama akisema huo ni mkutano wa kwanza kuhudhuria tangu mwaka 2014.
Ameeleza hilo ni kwa sababu, uchaguzi wa Desemba 2019 alikuwa anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji baada ya jaribio la mauaji yake Septemba 7, 2017 jijini Dodoma aliposhambuliwa kwa risasi.

Amesema siku hiyo pamoja na kutokuwepo, aliwaomba kura na walimchagua kuwa makamu mwenyekiti kwa kura asilimia 98.8.
"Tulipokutana mara ya mwisho kwenye ukumbi huu nikiwepo mimi katika mkutano wetu wa mwaka 2020 niliwaomba ridhaa ya kugombea urais nanyi mlinipigia kura zote za ndiyo," amesema.
Amesema wajumbe hao wa mkutano mkuu, wamekuwa wema kwake na kwamba wamethibitisha kuwa na imani naye.
Lissu amesema anamaliza miaka mitano ya uongozi wake na anaamini amewatumikia kwa namna ambayo ana haki ya kujivunia.
Baada ya kumaliza kutoa salamu zake, alirejea mbele ya meza kuu na kusalimia kwa kukumbatiana na Mbowe, hali iliyoibua shangwe ukumbini huku wao nyuso zao zikionyesha tabasamu.
Kauli ya Mbowe
Katika hotuba yake, Mbowe ametaka yeyote atakayerithi nafasi ya uongozi ndani ya chama hicho, iwe yeye kuendelea ama Lissu, ahakikishe anarejesha nidhamu, maadili na kutambua kwamba hakuna matusi katika utamaduni wa Chadema.
"Minyukano iliyojitokeza si ya kufurahia na hatupaswi kuiacha iendelee. Ni lazima kuna watu walikuwa wanatukana, tabia hizo inapaswa idhibitiwe. Hivyo, yeyote atakayechukua kijiti anapaswa kwenda kubadilisha hilo na atakayekengeuka ajulikane si mwenzetu," amesema.
Mbowe katika hotuba yake amesema chama hicho ni taasisi lazima ienziwe kwa nidhamu, huku akiviomba vyama vingine vikaimarike ili kujenga demokrasia kwa makini.
"Tusijenge taasisi kwa utaratibu wa kutukanana na kufanya mengine yanayobomoa haiba yetu. Ni lazima yarekebishwe na watakaochukua mikoba, siku ya leo wajue wanalojukumu hilo," amesema.
Amesema siasa si utani bali ni maisha ya kila siku na kuna watu wamesafiri kutoka mikoani kuja Dar es Salaam kujadili kwa kutambua kuna mambo hayako sawa.

"Tuko Chadema tunahitaji kuona mabadiliko ya matumaini na chama mbadala dhidi ya chama tawala. Malengo yetu hayajengwi katika kubadilishana madaraka," amesema.
Amesema Chadema lazima ije na sera mbadala ya kurejesha furaha kwenye mioyo ya watu waliokata tamaa, huku akieleza mbinu mbadala inahitajika.
"Najua tumetumikia na tunategemea siku ya leo ikatujengee matumaini mapya, na katika kipindi chote mlitupa ushirikiano lakini safari yetu haijaisha bado tunahitajiana kwenda mbele," amesema.
Amesema wanapoadhimisha miaka 32 ya chama hicho tangu kilipopata usajili wa kudumu Januari 21, 1993, itahitimishwa kwa kupata viongozi wapya.
"Uchaguzi huu haupaswi kuwa vita bali inapaswa kuwa furaha ya demokrasia. Yapo maneno mengi leo mnakwenda kupasua chama, lakini tofauti zetu leo tunakwenda kuzizika," amesema.
Amesema katikati ya tofauti zao bado umoja wao ni nguvu, hivyo ni lazima umoja udumishwe kwa kumaliza tofauti zao baada ya uchaguzi.
"Chama hiki kimebeba ndoto ya Taifa. Wako Watanzania mamilioni hawana kadi za Chadema lakini wanaamini maisha yao yataboreshwa na sera na nguvu ya Chadema. Kwa hiyo, kila mtu anapaswa kukilinda chama hiki kwa kujenga maadili na nidhamu," amesema.
"Hadi kufika hapa ni juhudi za wote, waliopo madarakani na waliotoka madarakani. Chama kimejengwa kwa hatua, na kwakuwa Mungu alitaka tuwe hapa, tumepitia mapito mengi na dhoruba kwa sababu ya Taifa letu," amesema.
Alichokisema Mohamed
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, amesema sifa inayoonekana ndani ya Chadema imejengwa na wanachama na sifa yeyote aliyonayo kiongozi wa chama hicho kimetokana na wanachama.
Amesema endapo atashindwa kukiheshimu chama hicho, yeye si chochote, akisisitiza kiongozi ambaye hatokiheshimu chama kilichompatia sifa ataporomoka kwenye jamii.
Makamu huyo mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, amesema sababu ya ukimya wake ni kulinda heshima ya chama, juhudi zilizofanywa na wanachama waliopoteza maisha kupigania chama hicho.
"Nimekuwa kimya ndani ya chama kulinda heshima ya chama na juhudi zilizofanywa na wenzetu kulinda chama chetu kwa kupoteza maisha yao. Nitakuwa nanyi ndani ya Chadema, nikiwa ndani ya uongozi na nje ya uongozi, sintakibeza chama changu," amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi.