Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Chadema ni kimbilio la Watanzania wengi'

Baadhi ya wafuasi wa Chadema wakiwa nje ya ukumbi wa Mlimani City ambapo uchaguzi wa chama hicho kwa viongozi wa juu unatarajiwa kufanyika leo. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Hotuba za viongozi wa kisiasa zimeibua shangwe katika mkutano mkuu wa Chadema, unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Ally Khatibu, amesema Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinavuta hisia za Watanzania wengi na kimekuwa kimbilio la Watanzania wengi, hivyo ni lazima wachague kiongozi makini.

"Chadema kimegusa hisia za Watanzania, ni lazima uchaguzi ufanyike kwa amani kwa kuwa Chadema ni kimbilio kwa Watanzania,” amesema Khatibu huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema.

"Fanyeni mkutano kwa amani mkiwa wamoja na iwapo kutakuwa na changamoto, tunaamini mmekuwa na viongozi mahiri mtayaweza kutatua kwa kuzingatia weledi na amani," amesema Khatibu.

Khatibu amesema hayo leo Jumanne, Januari 21, 2025, wakati akitoa salamu za baraza hilo kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chadema waliofika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama.

Khatibu amewataka wajumbe wa mkutano huo wa Chadema kufanya uchaguzi kwa amani na kuchagua viongozi, na mwisho wajumbe watoke wakifurahi.

Khatibu amesisitiza kuwa Ofisi ya Baraza la Vyama vya Siasa linawatakia uchaguzi wenye amani katika kuwampata kiongozi wa kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo.

Katika mkutano huo, uenyekiti unawania na Tundu Lissu, Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo pamoja na Charles Odero.


Hotuba ya Nyahoza

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amelazimika kusimamisha hotuba yake mara mbili, alipotaja 4R za Rais Samia Suluhu Hassan na aliposalimu kwa salamu ya mkuu huyo wa nchi.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo, Nyahoza ameanza kwa kuwasalimia wajumbe kwa salamu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo aghalabu hutumiwa na Rais Samia.

Badala ya kujibu kazi iendelee kama ambavyo salamu hiyo hujibiwa, wajumbe walisimama na kuanza kuipinga, wengine wakisema hawaitaki na wapo waliokuwa wanazomea.

Nyahoza ameendelea kueleza jinsi anavyoona chama hicho kimejiandaa vyema na anatarajia mkutano utakwenda vema.

Amesema ni jukumu la ofisi ya msajili kuhudhuria mikutano ya vyama vya siasa ili kuhakikisha chaguzi na teuzi ndani ya vyama vya siasa zinafanyika kwa kuzingatia sheria.

Amesema kwa sababu vyama vya siasa ni taasisi na vinapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia sheria.

"Tulivyokuwa tunaona kwenye mitandao huko kwa kweli Chadema mnatuonyesha demokrasia ipo. Na hilo nikupongeze Mwenyekiti (Mbowe) kwa dhati kabisa," amesema na kuibua shangwe kutoka kwa wajumbe.

Amesema katika mkutano huo, wamekwenda kuonyesha demokrasia namna ilivyo.

"Katika chama ambacho mmeelewa zile 4R za Mheshimiwa Rais basi ni ninyi," amesema na kuibua shangwe kutoka kwa wajumbe wakiimba 'Mbowe...! Mbowe...! Mbowe...!'

Utawala wa Rais Samia unatumia falsafa za 4R ambazo ni Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahamilivu), Reforms (Mageuzi), na Rebuilding (Kujenga upya Taifa).


Katikatika ya umeme

Kabla na baada ya mkutano huo kuanza, umeme ulikuwa ukikatika mara kwa mara na kuibua shangwe na kauli za hapa na pale kwamba zinaweza kuwa hujuma kuelekea uchaguzi utakaofanyika baadaye.

Umeme huo ulikuwa ukikatika mara kwa mara hata pale viongozi wakizungumza, akiwemo Lissu. Kutokana na hilo, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, akawatangazia wajumbe wa mkutano huo kuwa wamezungumza na uongozi wa ukumbi wawashe jenereta ili kuhakikisha uwepo wa umeme wakati wote.


Mkutano rasmi

Saa 6:08 mchana viongozi wa Chadema, akiwemo Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Naibu Katibu Mkuu bara Chadema, Benson Kigaila, walifika na kuingia ukumbini na kuketi meza kuu.

Ujio wa viongozi hao uliambatana na muziki ambao wajumbe waliucheza kwa kunyanyua kofia zao juu, wimbo wa tume huru na katiba mpya ukigonga nyoyo za wajumbe hao.

Kabla ya ujio wa viongozi hao, tayari ugeni wa Chadema uliingia ukumbini, msafara ukiongozwa na Naibu Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Ally Khatibu pamoja na wajumbe wa bodi ya wadhamini wa Chadema na mabalozi wanaoiwakilisha nchi mbalimbali nchini Tanzania.

Uwakilishi wa mabalozi waliowasili kwenye mkutano huo ni kutoka Marekani, Uingereza, mwakilishi wa Balozi wa China, Sweden, Finland, Norway, Ufaransa, na uwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya.

Baada ya kuwasili kwa wageni hao pamoja na viongozi waliopaswa kuketi meza kuu, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, alianza ratiba kwa kuwatia viongozi wa dini kufungua kwa dua.

Baada ya Mrema kukamilisha kazi yake, Katibu Mkuu John Mnyika alishika hatamu akatangaza idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu waliopaswa kufika ni 1,069, lakini waliofika ni 906 sawa na asilimia 84.5, akitoa ruksa kuendelea kwa mkutano kwa akidi kutimia.

Mnyika alitamatisha kazi yake hiyo na kukirejesha kijiti kwa Mrema, ambaye naye aliendelea kwa kutambulisha wajumbe waliopo ndani ya mkutano huo kwa kila kanda, wasimamizi wa uchaguzi, wajumbe wa udhamini wa chama hicho, pamoja na wajumbe wa sekretarieti.

Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Bernadetha Kafuko, Mkurugenzi wa Shirika la Sukita, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga, ni baadhi ya wageni walioshiriki mkutano huo.

Wageni wengine ni wawakilishi wa vyama vya siasa ACT Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha ADC, na NLD.

Pia, Mrema amemtambulisha mwakilishi wa chama rafiki cha siasa kutoka Denmark.


Endelea kufuatilia Mwananchi